Tuesday, 26 January 2016
WAZIRI MAKAMBA AIAGIZA NEMC KUWASIMAMISHA KAZI WATUMISHI WAKE WATATU
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUIMARISHA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA BARAZA LA TAIFA LA HIFADHI NA USIMAMIZI WA MAZINGIRA-NEMC
Katika kikao kilichoitishwa na Mhe. January Makamba (Mb), Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira tarehe 24 January 2016, kuhusu kuimarisha utendaji ndani ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira-NEMC maamuzi yaliyofikiwa ni kama ifuatavyo:
1. Kuhusu suala la kiwanda cha kusindika minofu ya punda mkoani Dodoma, imegundulika kulikuwa na ukiukwaji mkubwa, wa makusudi na wa wazi wa miiko ya kazi kwa watumishi wa NEMC walioshughulika na kiwanda hicho. Hivyo, Mhe. Makamba ameagiza watumishi wa NEMC wafuatao wasimamishwe kazi mara moja:
a. Dkt. Eladius Makene -Afisa Mazingira Mwandamizi,
b. Wakili Heche Suguta Manchare - Mwanasheria Daraja la II
c. Mhandisi Boniface Benedict Kyaruzi, Afisa Mazingira
Hatua nyingine za kinidhamu na kisheria zitafuatia
2. Vilevile, imebainika kwamba usimamizi wa watumishi wa NEMC siyo makini na thabiti na kusababisha malalamiko mengi kuhusu utendaji wa Baraza. Hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Mhandisi Bonaventura Baya apewe barua ya onyo kalian la mwisho kwa udhaifu katika usimamizi wa watumishi wa Baraza.
3. NEMC kama chombo muhimu nchini kilichopewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira inatarajiwa kazi zake zifanyike kwa ufanisi wa kiwango cha juu kulingana na majukumu yaliyoko kwenye Sheria. Hivyo, kwa mapungufu yanayojitokeza Mhe. Makamba, ndani ya wiki moja ataunda jopo la wataalamu wasiozidi watano ili kutathmini utendaji wa NEMC na changamoto mbali mbali katika usimamizi wa hifadhi ya mazingira na kuishauri Serikali ipasavyo.
4. Ili kuimarisha ufanisi na udhibiti wa utendaji wa NEMC, ndani ya wiki moja litatolewa Tangazo litakalokuwa na mambo yafuatayo: Anwani ya barua pepe (email), Nukushi (fax), Namba ya simu, Namba ya Whatsapp ili mtu yeyote mwenye malalamiko au aliyewahi kuombwa rushwa chochote na watumishi wa NEMC ambacho ni kinyume na maadili ya kazi yao atoe taarifa mara moja ili uchunguzi ufanyike na hatua zichukuliwe.
5. Kutokana na mapungufu yanayojitokeza katika utekelezaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira, ndani ya wiki moja, NEMC ipitie upya orodha ya wataalamu na taasisi elekezi zilizosajiliwa na kufuta wataalamu na taasisi zote ambazo zimekuwa zikikiuka maadili ya kazi zao likiwemo suala la kuwasilisha taarifa zilizo chini ya viwango, kuchelewesha kazi za wateja wao na kutowasiliana na wateja wao kuhusu hatua za utekelezaji wa maombi yao.
6. Ndani ya wiki tatu uitishwe mkutano wa dharura wa Bodi ya NEMC kujadili na kufanya maamuzi juu ya changamoto za utendaji katika Baraza.
IMETOLEWA NA
IDARA YA MAZINGIRA,
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
TAREHE 24.01.2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment