Tuesday, 5 April 2016
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) ZANZIBAR KIMEFURAHISHWA NA TAARIFA YA SERIKALI YA JAMHURI YA WATU WA CHINA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimefurahishwa na kimepata matumaini makubwa kutokana na taarifa ya Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ambayo imeelezea dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na Tanzania na Zanzibar katika jitihada zake za kuimarisha uchumi na ustawi wa jamii.
Kauli hiyo ya Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa mara nyengine tena inathibitisha imani ya kweli ya nchi hiyo katika kuendeleza ushirikiano wa kindugu baina ya nchi zetu mbili ambao umedumu kwa zaidi ya nusu karne sasa.
CCM inayo kila sababu ya kuthamini uhusiano wetu na ndugu zetu wa China siyo tu kwa sababu ya misaada ya nchi hiyo ya kiuchumi na kijamii ambayo imekuwa ikitoa msukumo mkubwa katika maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla, lakini pia kutokana na dhamiri ya kweli ya nchi hiyo katika kusaidia maendeleo ya wananchi wetu na taifa wakati wa dhiki na vile vile wakati wa faraja. Huu ndio urafiki wa kweli.
Zanzibar bado inakumbuka ya msaada mkubwa wa nchi hiyo, iliyowahi kutolewa katika kujenga na kuviendeleza viwanda mbali mbali ikiwemo kiwanda cha sukari na manukato cha Mahonda, kiwanda cha ngozi na viatu kilichokuwepo Maruhubi, usambazaji wa mabomba ya maji safi na salama katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba, uimarishaji wa kilimo Upenja, Bambi na maeneo mengine mengi.
Jamhuri ya Watu wa China kwa karibu miaka 50 sasa imekuwa ikituma madaktari wake kuja Zanzibar kusaidia huduma za matibabu kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na maradhi mbali mbali katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja na Abdalla Mzee iliyoko Pemba. Huduma za madaktari hao kwa kushirikiana na madaktari wazalendo zimekuwa zikisaidia kuimarisha afya na kuokoa maisha ya wananchi kadhaa hapa nchini.
Mradi wa ujenzi wa hospitali kubwa ya kisasa ya Abdalla Mzee huko Mkoa wa Kusini Pemba unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China pia unathibitisha dhamira ya nchi hiyo katika kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuimarisha sekta ya jamii. Ni dhahiri mradi huu baada ya kukamilika utaleta sura mpya kwa Pemba.
Ujenzi wa Uwanja wa Kisasa wa Michezo wa Amani pamoja na marekebisho yake yaliyofanywa katika miaka ya hivi karibuni pamoja na maandalizi ya Ujenzi wa kiwanja cha mpira wa miguu cha Mao Tse-tung, kiliopo Mjini Zanzibar ni miongoni mwa misaada ya China.
Vituo vya kurushia matangazo ya Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) vya Radio iliyopo maeneo ya Rahaleo na Dole vimejenga kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, kwa muda wote zimekuwa zikifaidika kwa kupatiwa nafasi za masomo kwa vijana wake ya taaluma tofauti nchini China ya muda mfupi na mrefu.
Kutokana na dhamira yake hiyo, Chama cha Mapinduzi siku zote kimekuwa kikijivunia ushirikiano wake na Chama cha Kikomunisti cha China (CCP) na kitaendelea kufanya hivyo daima kwa maslahi ya pande zote mbili, kwa kufahamu kwamba itikadi na msimamo thabiti wa CCP mbele ya mataifa mengine duniani, ndio uliyoifanya China leo kuwa moja kati ya mataifa yenye nguvu kubwa kiuchumi duniani.
Uhusiano wetu na China ambao uliasisiwa mara baada ya uhuru wa Tanganyika kwa Tanzania Bara na Mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964 kwa Zanzibar, umejengwa kwa misingi ya haki, usawa, kuheshimiana pamoja na kuzingatia na kujali maslahi ya kila upande.
Aidha, Chama Cha Mapinduzi kinatoa pongezi za dhati kwa nchi mbali mbali duniani zinaoungana na Zanzibar na Tanzania kwa kuendelea kuimarisha umoja na uhusiano mwema kwa maslahi ya wananchi walio wengi wa pande zote mbili za nchi hizo.
VUAI ALI VUAI
NAIBU KATIBU MKUU WA CCM ZANZIBAR
APRILI 4, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment