Sunday 3 April 2016

WATUMISHI WOTE WA CCM KUKATIWA BIMA-LUHWAVI


Na Bashir Nkoromo,Njombe

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema, kina mpango wa kuhakikisha kila mtumishi wake anapatiwa huduma ya Bima ya Afya ikiwa ni moja ya hatua ya kuboresha maisha ya watumishi hao.

Kimesema kupitia mpango huo, kila mtumishi hadi wa ngazi za chini ataweza kupata matibabu yeye na familia yake nchini kote.

Ahadi hiyo ilitokewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa  CCM (Bara), Bara, Rajab Luhwavi alipokuwa akizungumza na watumishi wa Chama na Jumuiya zake mkoani Njombe akiwa katika ziara ya kikazi ikiwa ni pamoja na kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili watumishi wa Chama.

Luhwavi alisema kwa sasa Chama kimo katika jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya kuwapatia huduma hiyo ya bima ya afya  watumishi wake ili wapate huduma ya matibabu kwa urahisi badala ya kutaabika kupata matibabu waanapougua jambo ambalo  linawapunguzia ufanisi katika kazi.

Alisema, kwa sasa watumishi wengi wa Chama hawawezi kuingizwa katika mpango huo wa bima ya afya kutokana na vima vya mishahara yao kutokidhi viwango vinavyotakiwa ili kusajiliwa na taasisi zinazotoa huduma hiyo ya bima ya afya hivyo  chama kikishapata fedha kitajazia mishara ya watumishi wenye vima vidogo ili kila mmoja aweze kuwa na sifa za kusajiliwa.

Naibu Katibu Mkuu huyo, aliongeza kwamba mpango huo utaanza kwa watumishi wa CCM na baadaye itakwenda hadi kwa watumishi wa Jumuiya za chama ili nao wanufaike na utaratibu huo wa bima ya afya.

“Nduguzangu siyo kwamba changamoto zote hatuna uwezo wa kuzitatu, kwa kweli baadhi ya changamoto tuna uwezo wa kuzitatua isipokuwa kinachotakiwa ni namna ya kujipanga tu, hivyo nina uhakika jambo hili litawezekana”, alisema Luhwavi.

Katika hatua nyingine Chama cha Mapinduzi kimesema ili kuhakikisha mpango wake wa kuendana na mabadiliko ya sasa unafanikiwa haraka, kinasimamia viongozi wake kwa karibu zaidi ili kuhakikisha kila mmoja anawajibika ipasavyo katika kuwahudumia watumishi walio chini yake hasa wa ngazi za chini.

Akitoa kauli hiyo wakati akizungumza na watumishi wa Chama mkoani Njombe,  Luhwavi alisema, alisema ni lazima chama kiwasimamie viongozi wake kwa makini kwa sababu viongozi kutohudumia kwa haraka na kwa uadilifu mkubwa wafanyakazi ni miongoni mwa vikwanzo vinavyoweza kukwamisha utekelezaji wa haraka lengo hilo la Chama kwendana na mabadiliko ya sasa.

“Tunajua  wapo baadhi ya viongozi wa Chama chetu ambao bado wanafanyakazi zao kwa mtindo wa kimangimeza ikiwa ni pamoja na kutotoa ushirikiano watumishi walio chini yao wanapohitaji ufumbuzi wa matatizo au changamoto zinazokuwa zinawakabili kwa namna mbalimbali”, alisema Luhwavi.

Alisema, imefika wakati sasa viongozi wa Chama kuacha tabia ya baadhi yao kufanya kazi kwa mazoea badala yake wajikite katika kushirikiana na wananchi kwa karibu katika kufanyakazi za kijamii kama ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, zahanati na miraji ya maji.

No comments:

Post a Comment