Wednesday 8 June 2016

SPIKA NDUGAI YU MZIMA WA AFYA

OFISI ya Spika wa Bunge imekanusha vikali taarifa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa, afya ya Spika Job Ndugai sio nzuri.

Taarifa iliyotolewa jana na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Ofisi ya Bunge, ilisema taarifa hizo ni za uzushi mkubwa na hazina ukweli wowote.

"Kumekuwa na taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu hali ya Mheshimiwa Spika na kuzua hofu kwa viongozi na wananchi. Ofisi ya Bunge inapenda kuchukua fursa hii kuwafahamisha watanzania wote kuwa taarifa hizo ni za uzushi mkubwa na hazina ukweli wowote.

"Hali ya Mheshimiwa Spika ni njema kabisa na yupo nchini India kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake, kufuatia maelekezo ya daktari wake kumtaka afanye hivyo mapema mwaka huu.

"Aidha, amepokea salamu nyingi za kumtakia kheri wakati akiendelea na uchunguzi wake kutoka kwa viongozi mbalimbali, wakiwemo waheshimiwa wabunge na amewatakia mfungo mwema wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa wale waliofunga ili kutimiza ibada ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Mheshimiwa Spika pia amewatakia kazi njema wabunge wote ya kushughulikia Bajeti ya serikali iliyosomwa jana.

"Tunawaomba Watanzania wote wenye nia njema na Spika wetu, waendelee kupuuza taarifa zinazotolewa kupitia mitandao ya kijamii na waendelee kumwombea ili afya yake iimarike haraka na kurejea nchini mapema," imeeleza taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment