Tuesday 9 August 2016

FILAMU YA DK. KIGWANGALLA, DOKTA MWAKA YAZIDI KUNOGA

NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla amesema hana ugomvi na hakuwahi kusoma na Tabibu wa Kituo cha Tiba Mbadala kilichofungiwa na serikali cha Foreplan Clinic, Juma Mwaka.

Kauli ya Dk. Kigwangalla imekuja siku moja baada ya gazeti moja la kila siku (siyo Uhuru), kuripoti kuwa waziri huyo ana 'bifu' na Dk. Mwaka.

Wakati Dk. Kigwangalla akisema hayo, Tabibu Mwaka amezidi kusakwa kila kona huku akionekana kulicheza shere Jeshi la Polisi nchini, baada ya  kudai amejisalimisha wakati sio kweli.

Wakati polisi wakiendelea kumsaka, taarifa zinadai kwamba Tabibu Mwaka hayupo Dar es Salaam na kuna uwezekano amekimbilia nje ya nchi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Dk. Kigwangalla, taarifa zinazoenezwa kwamba amewahi kusoma na Tabibu Mwaka kidato cha tano na cha sita katika shule ya sekondari ya Kigoma hazina ukweli.

“Hizi ni habari za uongo, za kupika na zenye kupotosha ukweli ili kuwaaminisha watu kuwa tunajuana na tuna ugomvi binafsi,”alisema na kuongeza:

“Nimekuwa nikimpuuza kwa sababu sikuwahi na haitatokea kuwa na nia mbaya dhidi ya mtanzania mwenzangu yeyote kwa sababu tu mimi nina dhamana ya uongozi. Sina tabia hiyo.”

Dk. Kigwangalla alisema amelazimika kutoa taarifa hiyo kwa kuwa uongo ukirudiwa rudiwa, hubadilika na kuwa ukweli, jambo ambalo linaweza kuleta madhara.

“Leo nimeamua kukanusha ili Watanzania pia mumpuuze, tuendelee kuimarisha huduma za tiba asili na tiba mbadala kutoka kwa matabibu wa kweli, wanaofuata utaratibu na sio wasanii kama huyu. Uongo au uzushi dhidi yangu mimi binafsi kamwe hautonirudisha nyuma kutekeleza majukumu yangu kwa umma,”alisema.

Alisema ifike mahali ijengwe nchi ya watu makini, wanaofuata sheria, kanuni na utaratibu na wanaoheshimu serikali.

“Kwenye afya za Watanzania hatuwezi kuvumilia usanii,  lazima tuwalinde walaji. Hili ni jukumu tulilopewa na Mheshimiwa Rais. Tutasimamia sheria ipasavyo. Hatutalegeza hata kidogo,” alisema.

Dk. Kigwangalla alisema hakusoma kidato cha tano na cha sita katika shule ya sekondari Kigoma, bali alisoma katika shule hiyo kidato cha kwanza hadi cha nne.

“Kidato cha tano na cha sita nilisoma shule ya sekondari Shinyanga
na sikumbuki kusoma katika shule zote hizi mbili na mtu mwenye jina hilo. Kama alisoma Kigoma sekondari, labda mbele yangu au nyuma yangu.  Pia, wakati  nasoma Kigoma sekondari, hakukuwa na 'high school',” alisema.


Aidha, alisema Tabibu Mwaka hakuwahi kuwa rafiki wala adui yake na hana ugomvi binafsi na yeye.

“Nafanya kazi ya kusimamia sheria ya tiba asili na tiba mbadala ipasavyo,” alisema na kuongeza:

“Naithamini tiba asili na tiba mbadala na ndiyo maana nimeongoza Wizara ya Afya kufanya mapinduzi makubwa kwenye eneo hili, ikiwemo kuweka utaratibu mzuri na rahisi zaidi wa kusajili watoa huduma, dawa zao, mazingira wanapotunzia dawa, wasaidizi wao, viwanda vyao na pia kuweka mikakati ya uanzishwaji wa viwanda vya dawa za tiba asili na tiba mbadala, sambamba na kufanyia utafiti dawa zao na kudhibiti ubora wa dawa zenyewe na dozi wanazowapa wateja.

“Muulizeni Mwaka, anaposema ana ugomvi binafsi na mimi, anamaanisha nini? Ugomvi upi? Juu ya nini? Awape taarifa kamili. Mimi sina ugomvi naye. Kwanza sikuwahi kumjua kabla ya ziara yangu ya kikazi pale Foreplan, nitakuwaje na ugomvi na mtu nisiyemjua? Si utakuwa ujuha huo?” Alihoji.

Dk. Kigwangalla aliwaomba watanzania  wanaofuatilia suala hilo kumtaka Tabibu Mwaka kuwapa majibu ya msingi ya hoja ya wakaguzi kutoka Wizara ya Afya.

“Mimi nilikuwa msimamizi, nikiwapa nguvu wataalamu wafanye kazi yao. Wataalamu walikuwepo, nao ana ugomvi nao binafsi? Mwambieni awajibu kama dawa za tiba ya kisasa kukutwa kwenye eneo lake la kazi ilikuwa halali? Alikuwa na vibali vya kutunza zaidi ya maboksi 200 ya dawa?

“Alikuwa na vibali vya kutunza zaidi ya magunia 10 ya dawa za tiba asili na tiba mbadala baada ya kufutiwa usajili? Alikuwa na uhalali wa kuendelea kutangaza kwenye vyombo vya habari kuwa wateja wake wafuate dawa pale ili wasikatishe dozi? Tena kinyume na katazo la baraza la tiba asili na tiba mbadala? Yeye yuko juu ya serikali? Yuko juu ya sheria? Ama anadhani anaweza kuidhihaki na kuiogofya serikali?” Alihoji Dk. Kigwangalla

Alisema baada ya ziara yake aliyoifanya Desemba, mwaka jana, hakutoa maelekezo ya kumfungia wala kumfutia kibali bali aliwaelekeza Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kuwaita na kuwaelekeza matabibu wote wafuate sheria, kanuni na taratibu.

“Waliitwa, wakaelekezwa.  Waungwana wakatii na yeye (Mwaka) hakutii, wakamfuta. Baada ya kufutiwa usajili, akaendelea kujitangaza na kutoa huduma, yeye ni nani?” Alihoji

Alisema kufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi na makosa hayo yana adhabu zake.

“Sisi kama serikali tumeagiza hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake. Serikali ina mkono mrefu, itamkamata. Itamtia nguvuni na atafikishwa mahakamani. Ataenda kujitetea huko kuwa ana ugomvi binafsi na Naibu Waziri Kigwangalla,” alisema.

Wakati Dk. Kigwangalla akisema hayo, taarifa za uhakika zimedai kuwa, tangu waziri huyo atoe agizo la kukamwatwa kwake ndani ya saa 24, tabibu huyo hajulikani alipo licha ya jeshi hilo kumsaka  kwa udi na uvumba katika maskani zake zote.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni, alithibitisha kutokamatwa  kwa Tabibu Mwaka na kwamba, nguvu zaidi  ya msako imeongezwa.

Alisema wanaamini kuwa kama hayupo Dar es Salaam, basi atakuwa nje ya mkoa huo, hivyo kuongeza msako  kote nchini.

“Kwa kuwa agizo la kukamatwa kwake  lilitolewa na waziri na limekuwa likitangazwa zaidi, basi makamanda wengine wanaweza kumkamata  popote, iwe ndani ya Ilala au nje ya  Dar es Salaam,”alisema Kamanda Hamduni.

Alisema wamefuatilia maskani zake na maeneo anayopenda kwenda, lakini hawajamnasa na kwamba msako unaendelea.

No comments:

Post a Comment