Tuesday, 9 August 2016
MAHAKAMA INAYOTEMBEA YAANZA KAZI
BODI ya Pamba Tanzania (TCB), imeanza kutumia mahakama inayotembea, kuwasaka wakulima na wanunuzi wa pamba wilayani Maswa, mkoani Simiyu wanaochafua zao hilo.
Watakaobainika na kukutwa na hatia ya kufanya hivyo, watachukuliwa hatua za kisheria ili kulinda thamani ya zao hilo.
Hayo yalielezwa jana na Mkaguzi wa Pamba Wilaya ya Maswa, Ally Mabrouk, wakati mahakama hiyo ilipoanza kazi ya kutembelea vituo mbalimbali vinavyonunua hilo katika wilaya hiyo, kutokana na uwepo wa vitendo vya baadhi ya wanunuzi kukutwa na pamba chafu.
Alisema baadhi ya kampuni zinazonunua zao hilo zimekuwa na mtindo wa kuchezea mizani kwa lengo la kuwaibia wakulima na wakulima nao kuongeza uzito kwenye pamba kwa kuweka maji na mchanga.
“Zao la pamba linapoteza thamani kila kukicha kutokana na mchezo mchafu unaofanywa na wakulima na wanunuzi. Wanunuzi huchezea mizani ili kumuibia mkulima na mkulima naye amekuwa akiweka maji na mchanga na hayo yote yanaichafua pamba ya Tanzania,"alisema.
Alisema wameamua kutumia mahakama hiyo ili kusikiliza na kutoa hukumu kwa watu wote, ambao watakutwa wamefanya makosa hayo ili
kulinusuru zao hilo kupotea katika siku za usoni.
“Atakayekutwa na makosa wakati tunafanya ukaguzi wa pamba katika maghala ya kununulia, hapo hapo tunaanza kesi dhidi ya mtuhumiwa kwani mahakama hiyo ina hakimu, karani wa mahakama, askari polisi na ukipatikana na hatia unaadhibiwa papo hapo,"alisema.
Baadhi ya wanunuzi wa zao hilo walisema hatua hiyo ni nzuri ingawa ilichelewa kuanza kutekelezwa kwani pamba ya Tanzania imekuwa ikipata bei ya chini katika soko la dunia.
“Hii Mahakama inayotembea ni nzuri ingawa bodi ya pamba ilichelewa kuianzisha kwa kuwa ingeanza mapema, hili suala la kila siku bei ya pamba ya Tanzania kushuka kwenye soko la dunia lingefutika na nina imani ingeendelea kufanya vizuri kila musimu,"alisema Peter Shikalile, mkazi wa kijiji cha Ipililo, wilaya ya Maswa.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka, akizungumzia mahakama hiyo alisema, huo ni mkakati wa mkoa wa kulinusuru zao la pamba
kutokana na wizi kukithiri, hasa kwa wanunuzi na wakulima wa zao hilo.
“Zao la pamba hatuwezi kulinusuru kwa kutoa matamko kila siku na kukaa kwenye vikao na kulipana posho, ni lazima tutekeleze kwa vitendo kama bodi ya pamba ilivyoanza katika wilaya ya Maswa, ni vizuri na wakaguzi wengine wa wilaya za mkoa huo wakaanza zoezi hilo kwani lipo kisheria na sio geni,”alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment