Monday 1 August 2016

JPM: MSIWATOZE USHURU WAFANYABIASHARA WADOGO, LEMBELI ATAMANI KURUDI CCM


 


RAIS Dk. John Magufuli amewaagiza wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya hapa nchini, kuacha kuwatoza ushuru wafanyabiaashara ndogondogo kwa kuwa mitaji yao ni mdogo.

Amesema kufanya hivyo ni kuwarudisha nyuma kimaendeleo, hivyo
ameagiza ushuru au kodi ilipwe kwa watu wamiliki wa maduka na wafanyabiashara wakubwa, walioko katika maeneo husika.

Mbali na hilo, Rais Dk. Magufuli ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, kuhakikisha maji yaliyoanza kutoka kwenye mji wa Tinde, siku moja kabla ya yeye kufika mkoani humo, yanapatika kwa uhakika, isiwe nguvu ya soda iliyochochewa na ujio wake.

Rais Magufuli alitoa maagizo hayo jana, wakati akiwahutubia wananchi wa Mji wa Kahama, katika mkutano wa hadhara uliofayika kwenye viwanja vya Magufuli.

Mkutano huo ulilenga kuwashukuru wananchi wa wilaya ya Kahama kwa kukipigia kura na kukipa ushindi Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.

Rais Magufuli alisema aliomba urais ili kutatua changamoto za wananchi na kuongeza kuwa, ushuru au kodi ilipwe kwa wafanyabiashara wenye kipato kikubwa zaidi.

Alisema serikali yake haijaagiza wananchi wa kawaida kulipa kodi, bali alitaka wananchi waishi maisha ya amani, hasa wafanyabiashara ndogondogo, ambao ndio walio wengi katika jamii ya Watanzania.

Agizo hilo la kufuta ushuru kwa wafanyabiashara ndogondogo lilikuja baada ya Mbunge wa Kahama, Jumanne Kishimba, kuwasilisha malalamiko kwa Rais Magufuli ya kuwepo mgambo wa halmashauri ya mji huo, wanaowabugudhi wafanyabiashara hao kwa kuwadai ushuru katika biashara wanazozifanya kila siku.

Kishimba alisema mji wa Kahama una changamoto nyingi, ikiwemo ya Hospitali ya Halmashauri ya Mji kuzidiwa na wagonjwa wanaokwenda kupata huduma za matibabu, hali ambayo imechangia kutopatikana kwa dawa.

Pia, alikumbushia ujenzi wa kilomita 20 za barabara ya lami, alioahidi Rais Magufuli wakati wa kampeni za urais na kwamba, wananchi wa Kahama wanasubiri kwa hamu utekelezaji wake.

Kishimba alimuomba Rais Magufuli kuwaruhusu wafanyabiashara, hususani wa mchele, kuuza bidhaa hiyo katika nchi jirani kwa kuwa wanunuzi wab hapa nchini wamepungua.

"Tunaomba sheria ya kutouza mazao katika nchi za nje iondolewe kwani kwa sasa wakulima wamepata mavuno mengi, hususani wale wanaolima mpunga. Wanunuzi wa mchele kwa sasa wamepungua sana, hali ambayo inawaweka wakulima kwenye wakati mgumu,”alisema Kishimba.

Rais Magufuli alisema atahakikisha hakuna ahadi yoyote aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi, ambayo haitekelezeki na kuongeza kuwa, yote yaliyoahidiwa na wabunge wa wilaya ya Kahama yatatekelezwa.

UPATIKANAJI MAJI ISIWE NGUVU YA SODA

Akizungumzia tatizo la maji katika mji wa Tinde, Rais Magufuli alisema upatikanaji wake siku moja kabla ya kuwasili kwenye mji huo isiwe nguvu ya soda.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo baada ya Diwani wa Kata ya Tinde, Jafari Kanoro, kupewa ruhusa ya kuwasalimia wananchi wa kata hiyo na kumueleza Rais kuwa, changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni uhaba wa maji.

Diwani huyo alisema juzi ndipo maji yalianza kutoka rasmi katika baadhi ya maeneo, baada ya mafundi wa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kukesha wakikamilisha matengenezo ya kiufundi hadi walipofanikisha maji kutoka.

Akijibu kero hiyo, Rais Magufuli alisema kilio cha wananchi hao amekisikia na kuagiza vyombo husika kuhakikisha kama maji hayo yametoka kwa siku hiyo, isiwe nguvu ya soda, bali yawe endelevu kwa siku zote na kwamba, bado kuna mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria utakaopita Tinde kuelekea mkoani Tabora.

“Ndugu zangu tayari tumepewa shilingi million 600 na serikali ya China, fedha hizo zitasambazwa kwenye mikoa mbalimbali yenye uhitaji wa maji. Tinde nitakuhurumieni na nitakutengeeni fungu katika fedha hizo,"alisema.

Akizungumza na wananchi wa eneo la Isaka na Kagongwa, Rais Magufuli alisema changamoto ya uhaba wa maji ataitatua, hivyo wamuunge mkono na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kutimiza ahadi alizoahidi.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, kitendo cha wanawake kuchota maji umbali mrefu, kinamsikitisha kwa kuwa hali hiyo imekuwa ikichangia maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa baadhi yao kufanyiwa vitendo vya ukatili, hasa kubakwa wakati wakitafuta maji.

Naye Mbunge wa Solwa, Ahmed Salum, aliishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kulipa jimbo lake mradi wa maji, ambao umeanzia katika Kata ya Tinde, ambapo vijiji 30, vitanufaika huku sh. milioni 400, zikitarajiwa kutumika kufaniksha hilo.

Mbunge huyo alimuomba Rais Magufuli kuwahishwa kwa fedha za miradi pale zinapoombwa ili kuhakikisha mradi unatumika kwa wakati.

LEMBELI ATAKA KURUDI CCM

Katika hatua nyingine, aliyekuwa mbunge wa Kahama na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kabla ya kusombwa na safari ya matumaini na kukimbilia CHADEMA, James Lembeli, ameanza kuonyesha dalili za kutamani kurejea CCM.

Dalili hizo alianza kuzionyesha baada ya kusema yupo tayari kurudi CCM, iwapo kasi ya Dk. Rais Dk. John Magufuli kuisafisha serikali na Chama itaendelea.

Amedai aliondoka CCM kutokana na kukithiri kwa rushwa, ufisadi pamoja na unafiki.

Lembeli, aliyasema hayo jana, mbele ya Rais Dk. Magufuli, alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Mji wa Kahama, akiwa ziarani mkoani Shinyanga.

“Iwapo Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. Magufuli atakisafisha Chama, basi naweza kurudi kundini ili niungane na wenzangu kuwahudumia wananchi,”alisema Lembeli.

Alimshukuru Rais Magufuli kwa kwenda Kahama na kusema hana kinyongo na Chama wala wana-CCM na kwamba, ataendelea kusalimiana nao kama awali, kwani 'kubadilisha msikiti sio mwisho wa uislamu.'

Alisema kama Rais Magufuli atakisafisha Chama, hana budi kurudi kundini na kwamba, hivi sasa anachosubiri ni kuona Dk. Magufuli akikisafisha Chama kwa kuwa kimejaa watu, ambao hawana sifa ya kukiongoza.

Akiwahutubia wananchi, Dk. Magufuli alisema yote aliyoahidi atayafanyia kazi na kuongeza kuwa, hatalewa madaraka ya urais. Aliwaomba Watanzania kumtanguliza Mungu katika kazi wanazozifanya kila siku.

“Wana-Kahama tambueni kuwa Lembeli ni afiki yangu wa siku nyingi na kuwepo kwake hapa, ninategemea mabadiliko makubwa kutoka kwake na ninakushauri rudi Tanzania kwa kuwa ulikokwenda ulipotea njia,’’alisema Rais Mgufuli.

Rais Magufuli alimtaka Lembeli kurudi CCM kwa kuwa aliko sasa ndiko waliko mafisadi, ambao alisema hawafai kupewa dhamana ya kuendelea kuongoza.

“Rudi kundini, nakujua unavyowapenda wananchi wa Kahama. Ukirudi sitakukata mkia. Huko ulikokwenda umepotea njia, mimi ndiye mwenyekiti ninayeongoza mapambano dhidi ya wasaliti ndani ya Chama, ambao asubuhi wapo CCM, jioni wapo upinzani,”alisema Rais Magufuli.

Akizungumza kwa niaba ya vyama vya upinzani, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Wilayani Kahama, Rajabu Yahaya, alimpongeza Rais Magufuli kwa kuibuka na ushindi mnono kwenye uchaguzi huo na kusema wanafurahishwa na utendaji kazi wake kwa kuwa ndicho kitu kilichokuwa kikipiganiwa. Alimuomba aendee kutumbua majipu.

No comments:

Post a Comment