Monday 1 August 2016

MBOWE AJIPELEKA POLISI, AHOJIWA KWA SAA TANO


MWENYEKITI wa CHADEMA, Freeman Mbowe, jana alijisalimisha kwa Jeshi la Polisi, ambapo alishikiliwa na kuhojiwa kwa saa tano kisha kuachiwa kwa dhamana.

Mbowe anatuhumiwa kutoa kauli za uchochezi zenye lengo la kusababisha uvunjifu wa amani ya nchi kwa kutoa taarifa ya kuwepo kwa maandamano ya kupinga udikteta nchi nzima Septemba Mosi, mwaka huu.

Mwenyekiti huyo wa CHADEMA alijisalimisha kwenye Kituo Kikuu cha Polisi cha Kati , kuanzia saa 7.05 mchana hadi saa 10.30, jioni kabla ya kuachiwa kwa dhamana ili kwenda kushiriki mazishi ya aliyekuwa mpiga picha mkuu wa Kampuni ya Free Media, Joseph Senga, yanayotarajiwa kufanyika leo Kwimba, Mwanza.

Akitoa taarifa za kukamatwa na kuhojiwa kwa Mbowe, Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA na Mbunge wa Singida Magharibi, Tundu Lissu, alisema kukamatwa kwake kulitokana na kauli za uchochezi alizozitoa wakati akizungumza na waandishi wa habari Julai 27, mwaka huu, akitangaza operesheni ya kuzunguka nchi nzima na kufanya mikutano ya hadhara ya kisiasa.

Lissu alisema Mbowe alijisalimisha mwenyewe polisi baada ya kuitwa na Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ili kuhojiwa kutokana na kauli zake hizo.

Mwanasheria Mkuu huyo wa CHADEMA alisema, katika mahojiano hayo, polisi walitaka kujua mambo mbalimbali kuhusu kauli yake hiyo ya kutangaza maandamano na mikutano ya kisiasa, ambayo imepigwa marufuku na serikali.

"Polisi wametumia muda mrefu kumhoji Mwenyekiti Mbowe kuhusu kauli zake alizozitoa wakati akizungumza na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, naye aliwaeleza lengo na makusudio ya kauli hizo,"alisema.

Lissu alisema baada ya mahojiano hayo, Mbowe aliachiwa kwa dhamana ili aweze kuhudhuria mazishi ya Senga, ambapo walimwambia wakimhitaji tena watamwita.

Mwanasheria huyo aliwataka wanachama wa CHADEMA kutoogopa na kwamba waendelee na operesheni ukuta nchi nzima, kitendo ambacho alidai kilemenga kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alipotafutwa kuzungumzia kukamatwa kwa Mbowe, simu yake haikuwa inapokelewa.

Akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita, Mbowe alisema CHADEMA itazunguka nchi nzima na kufanya maandamano na mikutano ya hadhara, hata kama vyombo vya ulinzi na usalama havitatoa kibali kuiruhusu.

Mwenyekiti huyo, ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alidai lengo lao ni kupinga uonevu na unyanyasaji wa serikali, ikiwemo hatua yake ya kupiga marufuku mikutano ya hadhara ya kisiasa.

No comments:

Post a Comment