Thursday, 25 August 2016

MAHABUSU AJINYONGA AKIWA SELO



MAHABUSU  Victoria Edward (51), mkazi wa Lemara, jijini hapa, amejinyonga katika mahabusu ya kituo kikuu cha polisi mkoani hapa.

Marehemu Edward, ambaye alikuwa mfanyabisahara, alifikishwa kituoni hapo kwa tuhuma za kuchoma moto nyumba yao ya familia  pamoja na duka.

Akithibithisha kujinyonga kwa mahabusu huyo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema tukio hilo lilitokea  saa 6:20 usiku, wakati wenzake wakiwa wamelala.

Alisema polisi waliokuwa zamu walisikia kelele za kuomba msaada kutoka kwa mahabusu hiyo ya wanawake, hali iliyowafanya kukimbilia huko na kufungua mlango, ndipo wakamkuta marehemu akiwa amejiyonga.

"Polisi wa zamu walisikia makelele kutoka  kwenye chumba cha mahabusu wanawake, ambapo polisi walijitahidi kuokoa maisha yake,  lakini ilishindikana kwani alikuwa ameshajinyonga, "alisema.

Kwa mujibu wa Mkumbo, mahabusu huyo alijinyonga kwa kutumia shuka lake, alilokuwa anatumia kujifunikia usiku wakati akiwa katika mahabusu hiyo.

Alisema marehemu aliletwa katika mahabusu hiyo siku nne zilizopita, ambapo alikuwa anaendelea kuhojiwa na jana angepelekwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili

"Leo (jana) ilikuwa afikishwe mahakamani kujibu tuhuma zilizokuwa zinamkabili, lakini kwa bahati mbaya amejinyonga," alisema.

Kamanda Mkumbo aliwatoa hofu mahabusu waliopo kwenye kituo hicho cha polisi kwa kuwahakikishia hali ya usalama kituoni hapo na kwamba, tukio hilo halihusiani na sababu zozote za kiusalama.

No comments:

Post a Comment