KESI ya kutoa maneno ya uchochezi, inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), imeshindwa kuanza kusikilizwa kutokana na kuibuka mabishano ya kisheria, baada ya upande wa utetezi kutaka kupatiwa maelezo ya mlalamikaji.
Hayo yalijiri jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Dk. Yohana Yongolo, wakati shauri hilo lilipofikishwa kwa kuanza kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa jamhuri.
Awali, Wakili wa Serikali Mkuu, Bernard Kongola, akishirikiana na Wakili wa Serikali, Mohammed Salum, walidai shauri limefikishwa kwa usikilizwaji na wanao mashahidi wawili, ambao ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Kimweri na Sajini Ndege.
Kabla ya kuanza usikilizwaji wa shauri hilo, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala, akishirikiana na mawakili John Mallya na Faraja Mangula, waliomba kupatiwa maelezo ya mlalamikaji.
Hata hivyo, Wakili Kongola alidai mlalamikaji katika kesi hiyo ni Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO), ambaye alikuwa mtoa taarifa na wameshindwa kuwapatia upande wa utetezi maelezo yake kwa kuwa hawana mpango wa kumuita kama shahidi.
“Kwa mujibu wa sheria, hatulazimiki kutoa maelezo ya mtu ambaye sio shahidi,” alidai.
Akijibu hoja hiyo, Wakili Kibatala alidai maelezo ya ZCO ndiyo yamesababisha uwepo wa shauri hilo, hivyo aitwe kama shahidi au la, maelezo yake ni muhimu kwa mshitakiwa kwa sababu hataweza kujitetea bila ya maelezo hayo.
Kibatala alidai watatumia vifungu vya 142(1) na 195(1) vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), ili hata kama upande wa jamhuri hautamuita ZCO aje kutoa ushahidi, aitwe kwa lazima wao waweze kumhoji.
Wakili huyo aliomba upande wa jamhuri ulazimishwe kuwapa maelezo hayo.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Dk. Yongolo aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 6, mwaka huu, atakapotoa uamuzi na kusema dhamana ya Lissu inaendelea.
Lissu, ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, anadaiwa kutoa maneno hayo ya uchochezi akiwa katika viwanja vya Mahakama ya Kisutu, alikokuwa amefikishwa siku hiyo kusomewa mashitaka ya kutoa chapisho la uchochezi kupitia gazeti la Mawio, lililokuwa na kichwa cha habari ‘Machafuko yaja Zanzibar’.
Mshitakiwa huyo anadaiwa kwa nia ya kushawishi na kudhalilisha wananchi wa Tanzania dhidi ya mamlaka halali ya serikali, alitoa maneno ya uchochezi yasemayo:
“Mamlaka ya serikali mbovu ya kidikteta uchwara inahitaji kupingwa na kila Mtanzania kwa nguvu zote. Huyu dikteta uchwara lazima apingwe kila sehemu. Kama uongozi utafanywa na utawala wa kijinga, nchi inaingia ndani ya giza nene.” Mwisho wa kunukuu.
No comments:
Post a Comment