Thursday, 25 August 2016

MAHAKAMA KUU YAIPIGA STOP NSSF KUTIMUA WAKAZI WAKE



MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi, imetoa zuio la muda kwa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Taifa (NSSF), kuwaondoa wakazi 87, walionunua nyumba za mradi wa Mtoni Kijichi, Dar es Salaam.

Hatua hiyo imetokana na mahakama hiyo kukubali ombi lililowasilishwa jana na mawakili wa wakazi hao, Benito Mandele, akishirikiana na Baby Rwechungura.

Amri hiyo ilitolewa na Jaji Penterine Kente, wakati maombi yaliyofunguliwa na wakazi hao dhidi ya Bodi ya Wakurugenzi ya NSSF na Kampuni ya Majembe Auction Mart, yalipofikishwa kwa usikilizwaji.

Maombi hayo ya kuiomba mahakama kutoa amri ya hali ilivyo katika nyumba za wakazi hao ibaki kama ilivyo, yalipangwa kusikilizwa jana, saa mbili asubuhi.

Hata hivyo, hadi ilipofika saa 2.20 asubuhi, wakati shauri hilo linaitwa, walalamikiwa Majembe na NSSF walikuwa hawajafika.

Mawakili hao wa wakazi hao walidai kwa kuwa Majembe walishapewa taarifa ya wito kufika mahakamani hapo na NSSF walikuwa wanajua, wanaiomba mahakama iahirishe usikilizwaji wa maombi hayo hadi tarehe nyingine.

“Tunaiomba mahakama iahirishe usikilizwaji wa maombi haya, lakini itoe amri ya kuzuia NSSF isiwaondoe waleta maombi katika nyumba,” waliomba.

Jaji Kente alisema mahakama inakubaliana na ombi la wakazi hao, hivyo inatoa amri ya muda kwa Majembe na NSSF kutowaondoa katika nyumba.

Baada ya kueleza hayo, Jaji Kente aliahirisha usikilizwaji wa maombi hayo hadi Oktoba 17, mwaka huu.

Wakazi hao walifungua kesi ya msingi mahakamani hapo na kuwasilisha maombi wakiiomba iamuru hali ilivyo katika makazi hayo ibaki kama ilivyo mpaka pale kesi yao ya msingi itakaposikilizwa.

Wakazi hao waliamua kufungua shauri hilo baada ya kushindwa kupata ufumbuzi wa madai yao katika Taasisi ya Usuluhishi kutokana na walalamikiwa kutofika.

Kwa mujibu wa hati ya madai, wakazi hao wanadai kwamba mlalamikiwa wa kwanza (Bodi ya Wakurugenzi ya NSSF), ameshindwa kutekeleza makubaliano kwa mradi huo kukosa huduma za kijamii.

Aidha, wanadai nyumba hizo hazina ubora na haziendani na kiwango cha fedha wanachotakiwa kulipa na kwamba, wamekuwa wakitumia fedha zao kufanyia ukarabati.

No comments:

Post a Comment