Wednesday 3 August 2016

MAKONDA ATEMA CHECHE

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amemuomba Katibu Mkuu wa  Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi na Kamishna wa Kazi nchini,  kuwaondoa mara moja  maofisa mipango miji wa Manispaa za Ilala na Kinondoni kutokana na uwajibikaji mbovu.

Makonda alifikia uamuzi wa kuwatumbua maofisa hao jana,  baada ya kushindwa kuwasilisha ripoti ya migogoro ya ardhi,  hususan maeneo ya wazi na yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za umma na yaliyovamiwa.

Alifikia uamuzi huo mbele ya mkutano wa madiwani wote wa mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi, makamishna wa ardhi, maofisa mipango miji  na wadau, kwenye mkutano aliouitiosha kwa ajili ya kushughulikia changamoto za ardhi.

Maofisa Mipango Miji waliotumbuliwa ni Juliana Lerata (Kinondoni) na Paulo Mbembela (Ilala), ambao walishindwa kutoa ripoti ya masuala ya ardhi, ikiwa ni pamoja  na kubainisha migogoro ya ardhi  na  hatua zinazochukuliwa.

Baada ya madiwani kueleza kero za uvamizi wa maeneo katika kata zao, huku asilimia kubwa wakidai  kuzidiwa na migogoro hiyo, ndipo Makonda alipowataka maofisa mipango miji hao kutoa ripoti kamili, ambapo ni Ofisa wa Temeke tu, aliyeweza kusoma ripoti huku wa Kinondoni akiomba aende akaiandae na wa Ilala akishindwa kuainisha  maeneo hayo.

“Namuomba Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kuwachukua maofisa hao. Sihitaji watu  wa mchakato, nataka watendaji kazi kwa vitendo,”alisema Makonda.

Alisema inasikitisha kuona ofisa mipango miji  anaitwa katika kikao kujadili suala nyeti kama la migogoro ya ardhi, ambalo ni changamoto kubwa katika  halmashauri nyingi, lakini anashindwa kueleza jambo lolote la maana, hali inayoonyesha kwamba hawawajibiki ipasavyo.

“Wawachukue waondoke haraka, siwataki katika mkoa wangu wa Dar es Salaam. Ikiwezekana waende wizarani. Haiwezekani ofisa mipango miji unaitwa na mkuu wa mkoa kwenye kikao kikubwa cha madiwani, unakuja huna ripoti yoyote ya msingi wakati idara yako ndiyo inajihusisha na masuala haya. Aina hii ya utendaji siitaki. Nataka utendaji wa ofisa mipango miji wa Temeke,”alisema Makonda.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo  wa mkoa aliwataka  watu wote waliovamia maeneo ya wazi na yaliyotengwa kwa shughuli za umma, kubomoa  kwa gharama zao kabla ya kiama kuwafikia.

Pia, amewapa siku 10  wakuu wa wilaya  na madiwani, kuhakikisha wanabaini na kuanisha maeneo yote ya wazi na yaliyovamiwa ili yaweze kurejeshwa haraka.

“Madiwani wabaneni watendaji wa kata kubaini maeneo hayo, baada ya hapo tutakaa na kuangalia hatua za kuchukua,”alisema Makonda.

Wakati huo huo, Makonda alisema mtendaji yoyote wa ardhi aliyehusika kuchezesha ramani na kubadilisha michoro  ya maeneo hayo ili kubadili matumizi au umiliki, atakiona cha moto.

“Yoyote atakayebainika atapoteza kazi yake kwa sababu hao ni wezi kama wezi wengine. Pia watarejesha gharama zote tutakazoingia  kisha mkondo wa sheria utafuata,” alionya Makonda.

Alisema tayari ameongea na Kamishna wa Jeshi la Polisi  Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,  Simon Sirro, kwamba itakapoanza operesheni ya kurejesha maeneo hayo, hakuna polisi atakayebaki kituoni, hivyo kuonya yeyote anayeamini  eneo alipo ni la wazi, aanze kuondoka haraka.

No comments:

Post a Comment