Wednesday 3 August 2016

WANAOMILIKI ARDHI KWENYE MAKAZI HOLELA KUONDOLEWA

SERIKALI imewataka wamiliki ardhi, hususan kwenye makazi yaliyojengwa kiholela Dar es Salaam, kuwa tayari kutoa maeneo yao kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya mji.

Kutokana na hatua hiyo, imesema baadhi ya nyumba zitavunjwa ama nzima au sehemu na pia kubomolewa kwa baadhi ya kuta ili kupitisha miundombinu mbalimbali, ikiwemo ya majitaka na barabara.
 
Imesema lengo la hatua hiyo ni kutambua, kupanga na kupima vipande vya ardhi na kuweka huduma za jamii kama miundombinu ya barabara na mitaro ya maji ya mvua ili kuboresha mazingira ya makazi.

Hivyo imewataka wananchi kuwa tayari kwenye mpango wa urasimishaji wa maeneo, ambayo yamejengwa kiholela ili huduma muhimu za kijamii ziwafikie.

Mpango huo unatekelezwa katika maeneo yote yaliyojengwa kiholela pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam.

Kaimu Mkurugenzi Urasimishaji Makazi Holela wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bertha Mlonda, aliyasema hayo jana, jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu  mpango wa urasimishaji makazi yaliyojengwa kiholela.

Bertha alisema makazi holela ni yale yaliyojengwa bila kufuata sheria, kanuni na taratibu za mipango miji inayoongozwa na sheria namba nane ya mwaka 2007 na ile ya serikali za mitaa, sehemu ya mamlaka za miji ya mwaka 1982.

Alisema urasimishaji wa makazi una sehemu kuu mbii, yaani kutambua, kupanga na kupima vipande vya ardhi na kuweka huduma za jamii kama miundombinu ya barabara na mitaro ya maji ya mvua ili kuboresha mazingira ya makazi.

Sehemu ya pili, Bertha alisema ni kuongeza usalama wa wamiliki kwa kutoa hatimiliki ya muda mrefu ili kuepuka migogoro ya ardhi, ambayo imedumu kwa muda mrefu.

“Hatua ya kwanza kabla hatujaanza kurasimisha ardhi ni kuhamasisha wenye ardhi wajue umuhimu wa kuachia sehemu ya ardhi yao kwa ajili ya miundombinu na huduma nyingine za kijamii na kiuchumi.

"Mpango huu ni shirikishi, wananchi wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kushirikiana na wataalamu kubainisha mahitaji ya huduma za jamii na miundombinu, watambue kuwa si makazi yote yana sifa ya kurasimishwa,”alisema.

Aliongeza kuwa vigezo vya urasimishaji ni maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya matumizi ya makazi katika mpango wa jumla wa mji na liwe na idadi kubwa ya watu, ambao wanaishi kwa kulipia ada bila kuwa na uthibitisho wa uhalali wa umiliki.

Aidha, Bertha alisema eneo lazima liwe na ongezeko kubwa la ujenzi wa nyumba, wakazi wengi na wameishi kwa muda mrefu na linaonekana kukomaa.

Pia alisema eneo lingine lonalohusika ni lile ambalo wamiliki wanaendelea kugawanya mashamba au viwanja vyao na ujenzi wa nyumba mpya kwa ajili ya makazi na biashara na linandelea kwa kasi kubwa.

Vigezo vingine alisema ni eneo hilo liwe na idadi kubwa ya wakazi na asasi za kijamii na wameshahamasika kushiriki katika mipango ya urasimishaji kwa kuchangia gharama za kupanga, kupima na kumilikisha, eneo husika lisiwe hatarishi kama kwenye miinuko mikali, mabonde na lisiwe karibu na dampo la taka.

Aidha, alisema maeneo yasiwe yamepangwa na kupimwa kwa matumizi mengine kama viwanda, taasisi, makaburi na maeneo mengine kama ya miundombinu, lisiwe na msongamano mkubwa wa nyumba ili litoshe kwa ajili ya miundombinu  na huduma muhimu za kijamii.

“Mpango huu umeshaanza, ambapo umeanzia Kimara. Tumeweka ofisi zetu pale Kimara Baruti karibu na ofisi za serikali za mtaa na  tumeshamaliza katika kata mbili za Kilungule A na B, wiki ijayo tunakwenda Mavurunza," alisema.

Aliongeza : "Tunatoa wito kwa wanachi ambao wanaona wapo katika maeneo yanayostahili kufanyiwa urasimishaji, kutoa taarifa katika ofisi zetu na watu wote wanaohusika na masuala ya ardhi, wanapatikana katika vituo ambavyo tutakuwa tunaweka kwenye eneo husika, ambapo tunatoa na hati miliki za ardhi mara baada ya kupima.”

Kaimu Mkurugenzi huyo alisema kwenye maeneo ambayo yatarasimishwa, wakazi wake watachangia gharama kidogo kulingana na ukubwa wa eneo na vitu vitakavyochangiwa ni pamoja na  ada ya hatimiliki, kodi ya ardhi, ada ya leseni na upimaji wa eneo.

Alisema katika maeneo wanayopita, wanakutana na changamoto nyingi, ikiwemo watu kutokubali kiurahisi kutoa sehemu ya ardhi yao kwa ajii ya mindombinu ya huduma zao wenyewe na hali ya hewa kutokana na zoezi hilo lilianza rasmi Machi 4, mwaka huu, wakati ambapo mvua zilikuwa zikinyesha, hivyo kukosa sehemu ya kuweka vifaa vyao.

Aidha, alisema zoezi hilo ni endelevu kwa jiji zima la Dar es Salaam ili kuhakikisha kuwa huduma za kijamii zinapatikana kwa urahisi kwenye maeneo yote yenye sifa za urasimishaji.

No comments:

Post a Comment