Wednesday 3 August 2016

MWALIMU AUAWA NA WANANCHI


MWALIMU Daniel Msalika (42), wa shule ya msingi Nyasosi, iliyoko wilayani Bariadi, mkoani hapa, amefariki dunia katika Hospitali ya Rufani ya Bugando, baada ya kushambuliwa na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Nyasosi, kwa madai ya kujihusisha kimapenzi na wanafunzi wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Onesmo Lyanga, alisema jana kuwa, mwalimu huyo alifariki dunia juzi, saa 8, usiku.

Lyanga alisema Julai 27, mwaka huu, saa 6:30 usiku, wananchi ambao idadi yao haijafahamika, walivamia nyumba ya mwalimu huyo, baada ya kupata taarifa kuwa kuna mwanafunzi, ambaye amelala nyumbani kwake jambo, ambalo halikuwa la kweli.

“Wananchi walipata taarifa kuwa nyumbani kwa mwalimu kuna mwanafunzi amelala, hivyo walimvamia kwa kuvunja mlango na kuanza kumshambulia kwa kutumia silaha za jadi na kumsababishia majeraha makubwa sehemu za kichwani na usoni, lakini binti waliyemkuta kwake ni mwenye umri wa miaka 18, hakuwa mwanafunzi,” alisema.

Alisema baada ya wananchi kuvamia nyumba ya mwalimu huyo na kumjeruhi, alikimbizwa katika kituo cha Afya cha Isanga kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Lyanga alisema hali ya mwalimu huyo iliendelea kuwa mbaya na kwamba, alipelekwa katika Hospitali ya Rufani ya Bugando, iliyoko Mwanza, ambako alifariki dunia.

Alisema tuhuma zilizoelekezwa kwa mwalimu huyo hazikuwa za kweli na aliwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi.

Kamanda huyo alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na watakaobainika watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Alisema polisi inamshikilia binti aliyekutwa kwenye nyumba ya mwalimu huyo na baba yake mzazi kwa uchunguzi zaidi.

No comments:

Post a Comment