MAKAMA Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula amesema
Rais Dk. John Magufuli siyo dikteta bali ni kiongozi mtiifu na mwadilifu,
anayetekeleza maagizo ya Chama yaliyoko katika Ilani ya Uchaguzi ya 2015-2020.
Amesema udikteta ni kuingia madarakani bila
demokrasia, lakini Dk. Magufuli aliingia madarakani kwa uchaguzi uliopitia
hatua mbalimbali, baada ya mchujo wa vikao vya Chama, ambapo alipatikana kutoka
katika kundi la wanachama 42, waliomba kuteuliwa na CCM.
Mangula alisema hayo jana, alipozungumza na Uhuru,
kuhusu maandamano ya CHADEMA, waliyoyabatiza jina la Umoja wa Kupinga Udikteta (UKUTA),
yaliyopangwa kufanyika Septemba Mosi.
Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM alisema, baada ya kuteuliwa
na CCM, Rais Dk. Magufuli alipita kwa wananchi kunadi Ilani ya Uchaguzi, ambapo
watu zaidi ya milioni nane walikubaliana nayo na kumchagua kuwa Rais wa
Tanzania.
“ Ushauri wangu kwa vijana wanaohamasishwa kujenga
ukuta wa kufikirika barabarani, ni bora wakajenge kuta za shule,nyumba za
walimu, watengeneze na madawati kama ilivyofanya CCM kutoa madawati zaidi ya
1,000,”alisema na kuongeza kuwa, Rais Dk. Magufuli anafanya kazi nzuri ya
kutekeleza Ilani.
Alisema katika kifungu cha 13, cha Ilani ya Uchaguzi
kinasema: “Katika kipindi cha miaka mitano, CCM itazielekeza serikali zake zote
kupambana na rushwa na kuchukua
hatu dhidi ya kiongozi yeyote atakayejihusisha na rushwa.
“Serikali zote zitatakiwa kushughulikia kwa ukali
zaidi tatizo la ubadhirifu wa mali za umma,” inaeleza sehemu hiyo ya Ilani ya Uchaguzi
ya CCM ya 2015-2020.
Mangula alisema katika kipindi kifupi, Rais Dk.
Magufuli ametekeleza maagizo hayo kwa vitendo kwa kuwachukulia hatua watuhumiwa
wa rushwa na wabadhirifu wa mali za umma, hivyo haiwezekani kumwita dikteta mtu
mwadilifu, anayetekeleza Ilani iliyokubaliwa na Watanzania.
“Sioni hoja ya msingi ya kumwita Rais Dk. Magufuli
dikteta wakati alichaguliwa kwa kura kuanzia ndani ya Chama hadi kwa wananchi.
Mgombea urais wa CHADEMA alipigiwa kura na nani na
alipata kura ngapi katika uchaguzi wa ndani ya chama chao?”Alihoji Mangula.
Alisema kwa bahati mbaya, wanaodai demokrasia
wenyewe hawana demokrasia hata kidogo, wakati CCM wanapokezana uongozi kila
baada ya kipindi fulani. Alisema CHADEMA wamekuwa wakiendesha chama kama
kampuni hadi viongozi wengine wanakerwa na kuamua kuondokana na siasa.
“CHADEMA walishindwa kutumia demokrasia kwenye
uchaguzi wa 2015, hadi Katibu Mkuu wao, Dk. Willibroad Slaa akaondoka. Nafasi
ya mwenyekiti kila wakati ni Freeman Mbowe. Hebu ajitokeze hadharani aseme kama
chama chao hakina watu wengine wenye uwezo wa kuwa wenyeviti,” alisema.
Mangula aliongeza: “Hata James Mbatia, Mwenyekiti
wa NCCR-Mageuzi, ambaye yuko kwenye kundi la UKAWA, tangu mwaka 1999 mpaka sasa
yeye ndiye mwenyekiti. CUF nako hakuko salama, ndio maana Mwenyekiti wao,
Profesa Ibrahimu Lipumba alijiuzulu baada ya kukerwa na utaratibu wa kumpata
mgombea urais.”
Mangula alisema kinachofanywa na viongozi hao
wakiwa madarakani ndiyo udikteta halisi.
Alisema CHADEMA wamekosa ajenda hivyo imekuwa
kawaida yao kuzua mambo ya kuwaunganisha pamoja
na sio mara ya kwanza kwani iliwahi kuanzishwa Operesheni Sangara, M4C
na zote hazikuwa na manufaa yoyote zaidi ya kuhamasisha vijana waingie barabarani,
lakini wenyewe wanajificha.
“CHADEMA ajenda yao kubwa ilikuwa rushwa na
ufisadi, lakini utendaji wa awamu ya tano umeshughulikia kwa vitendo kero hizo,
hivyo hawana tena ajenda, ndio wamezua UKUTA, lakini hakuna hoja ya udikteta
kwa Dk. Magufuli,”alisema.
Mangula alisema kama wana hoja ya msingi, CHADEMA
walipaswa watumie Baraza la Vyama vya Siasa, ambalo lilizinduliwa rasmi na Rais
mstafu Benjamin Mkapa, ambaye katika uzinduzi huo Julai 23, 2005, aliwasisitiza
juu ya kulinda amani.
“Nakumbuka wakati analizindua baraza hilo, Mkapa
alituleleza yafuatayo ‘Ni makosa makubwa na jambo la hatari kwa
wanasiasa kupanda mbegu za chuki na uhasama ndani ya nyoyo za vijana wa
Tanzania dhidi ya vijana wenzao wa Tanzania, eti kwa sababu za kisiasa.”
No comments:
Post a Comment