Sunday, 23 October 2016

MAKADA 100 WAVULIWA UANACHAMA CCM



NA PETER KATULANDA, MWANZA

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa, kimewavua uanachama makada wake 100, akiwemo Meya wa zamani wa jiji la Mwanza na Diwani wa Kata ya Isamilo, Wilaya ya Nyamagana, Leonard Bihondo na mkewe, Veronica Bihondo.

Taarifa iliyotolewa juzi na Katibu Mwenezi wa CCM mkoani hapa, Simon Mangelepa, ilisema waliotimuliwa wanatoka katika wilaya za Misungwi, Kwimba na Ukerewe, ambayo imewatimua wanachama  86.

Mangelepa alisema kuvuliwa uanachama wao kunatokana na kukisaliti Chama wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.

Alisema mapendekezo ya kuvuliwa kwa uanachama, yalianzia ngazi za matawi, kata na wilaya husika na kikao cha halmashauri kuu cha mkoa kilibariki kutimuliwa kwao.

“Hatua zimechukuliwa kutoka kwenye matawi, kata na wilaya za Ukerewe, Kwimba na Nyamagana kwa kuwavua uanachama watu 96, wakiwemo viongozi wa matawi na kata, ambapo kikao cha halmashauri kuu ya mkoa cha leo (juzi) tumebariki watimuliwe na kuvuliwa uanachama,” alisema.

Aliwataja wengine waliotimuliwa katika wilaya ya Nyamagana kuwa ni pamoja na Bihondo na Bahati Selemani, ambaye ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Sokoni na Balozi Magesa Manyama.

Kwa wilaya ya Nyamagana, waliotimuliwa ni wanane, Kwimba watatu, Misungwi watatu na Ukerewe 86, akiwemo Helen Kungusi, aliyekuwa Mwenyekiti wa UWT wa wilaya hiyo.

Wengine waliovuliwa uanachama Ukerewe ni Debora Magesa , Ramadhan Mazige, Sikitu Matete (mjumbe wa kamati ya utekelezaji UWT wilaya) na Focus Katembo, ambaye alikuwa mjumbe wa mkutano mkuu wa Taifa.

Katibu Mwenezi huyo aliipongeza serikali kwa kazi kubwa inayofanya ya kutatua kero za wananchi, kukusanya mapato na kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.

Mangelepa aliwaomba viongozi wa Chama, wakiwemo madiwani na wabunge, wasimamie utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kikamilifu.

No comments:

Post a Comment