Sunday, 23 October 2016

MANGULA AFURAHISHWA 100 KUFUKUZWA UANACHAMA WA CCM MWANZA, ASEMA ANAYEFAA KUWA KIONGOZI NI MWENYE UZALENDO WA KUJITOLEA SIYO UHODARI WA HOTUBA


Na Bashir Nkoromo, Mkuranga
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula ameelezea kufurahishwa kwake kufukuzwa kwa wanachama 100 mkoani Mwanza kwa kubainika kukisaliti chama wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

"Haiwezekani, unajiita mwanachama, halafu badala ya kujitolea kwa nguvu zako zote chama kishinde vita ya kushika dola, wewe unakisaliti,  hapo unakuwa si mwanachama bali jeshi la kukodiwa",  Mangula alisema, hayo jana, wakati akizungumza na Vijana wanaosoma na waliohitimu vyuo vikuu 20, ambao wameweka kambi ya kufyatua matofali kwa ajli ya ujenzi wa mabweni na nyumba za walimu katika shule ya Sekondari Nasabagani, Mkuranga mkoa wa Pwani.

 "Taarifa ya Chama kuwafukuza uanachama wale 100 kule Mwanza imenifurahisha sana, ni matumaini yangu kwamba hatua kama hizi zitaendelea kuchukuliwa  kila mahala nchini kote kwa waliokisaliti chama. hivi ni mchezaji gani anayempiga ngwara mchezaji wa timu yake wakati wa mechi ya kutafuta ubingwa halafu akaachwa kuendelea kuwa katika timu?" Mangula alisema na kuhoji kwa mshangao.

Mangua alisema, wakati mikoa itaendelea kuchukua hatua, lakini pia kwa ngazi ya taifa hatua dhidi ya waliokisaliti chama zitaendelea kuchukuliwa, ikiwa ni pamoja na kuwatupilia mbali watakaojaribu kuomba nafasi za uongozi wakati wa uchaguzi wa Chama mwakani, huku wakiwa wameshabainika kuwa walikisaliti chama wakati wa uchaguzi mkuu ulipita.

Mangula aliwataka vijana nchini kote hasa wasomi, kuepuka kutumiwa vibaya na wanachama watakaokuwa wanasaka uongozi wakati wa uchaguzi mkuu wa CCM unaotarajiwa kufanyika mwakani, kwa kuwa kijana yeyote atakayekubali kutumiwa vibaya atakuwa amekisaliti na kuchangia kunyong'onyesha nguvu na uhai wa Chama.

"Hili la kutumiwa vibaya hasa ninyi vijana, nawaasa sana kuepuka nalo, jambo hili ni baya sana, na si kwa Chama tu lakini hata kwa wewe uliyekubali kutumika, maana utatumiwa kama ngazi, halafu akishapita hatakuwa na manufaa kwako na hata kwa taifa maana atakuwa mvurugaji tu, badala ya kushiriki kuleta maendeleo ya chama na taifa", Alisisitiza mangula.

Alisema, vijana hao 53 waliojitolewa kufyatua matofali kwa ajili ya ujenzi huo wa mabweni na nyumba za walimu, wameonyesha moyo mkubwa wa uzalendo kwa nchi yao, na kwamba huo ndiyo uzalendo wa kweli unaopaswa kuonyeshwa na kila mwananchi hasa viongozi katika ngazi mbalimbali.

Mangula alisema, vijana hao wameoyesha mwamko ule uliokuwa umejengwa na kuwepo wakati wa Baba wa taifa Mwalimu Nyerere, ambao katika miaka ya hivi karibuni hasa baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi umetoweka kwa watu kuanza kujinasibu kwa majina ya vyama vyao vya siasa badala ya kuonyesha uzalendo kwa kuisaidia jamii kwa za kujitoea.

Alisema, umefikia wakati sasa kipimo cha kwanza kwa yeyote kupata uongozi iwe ni kutazamwa kama kweli ni mzalendo ambaye yupo mstari wa mbele kufanya kazi za kujitolea katika jamii, na siyo kutazama uwezo wake wa kuzungumza na kumwaga hotuba nzuri majukwaani.

"Sifa za mtu kupewa uongozi isiwe ukasuku wa kutoa talalila za hotuba nzuri za kisiasa majukwaani, kwanza atazwamwe kama amekuwa akitoa mchango gani kwa jamii kwa kufanya kazi za kujitolea katika kusukuma maendeleo ya taifa mbele kama ilivyokuwa wakati wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, hongereni sana vijana kwa kuonyesha moyo wa kfufua uzalendo.", alisema  Mangula.

Mapema, Katibu wa Kambi ya vijana hao, Daniel Sarungi, alisema, tangu walipoanza kambi hiyo, na kuanza kufyatua matofali Septemba 29, 2016, wameshafywatua matofali zaidi ya 30,000, kati ya lengo lao la matofali 45,000, ambalo watahakikisha wamelifikia kesho Oktoba 24, 2016.

Alisema, vijana hao wamejikusanya kutoka vyuo vikuu 20, vutatu vikiwa ni vya nchi za nje, na wamekuwa wakishirikiana vizuri, tangu kusomba mchanga na kufyatua matofali, kujipikia chakula, kufundisha wanafunzi wa kidato cha tano na sita katika shule hiyo, kutoa huduma ya afya, kushiriki michezo mbalimbali na kufanya semina na mijadala ya kukuza uwezo wa kuleta maendeleo katika jamii.

Sarungi alisema, vijana hao ambao baadhi wameshahitimu masomo na wengine bado wanasoma katika taaluma mbalimbali wameamua kujitolea kusaidia ujenzi wa mabweni na nyumba za walimu, baada ya kuguswa na adha ya kulala chini wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita katika shule hiyo huku walimu na wakiwa hawana nyumba za kutosha kuishi.

Wakati wanafunzi waliopo sasa wanalala chini katika chumba cha maabara, nyumba moja yeneye nyumba vitatu inatumiwa na walimu saba kuishi katika nyumba hiyo, haliambayo hairidhishi.

Mapema, Mangula alishiriki kufyatua matofali na baadaye kusema kwamba aliamua kwenda kuwaunga mkono vijana hao baada ya kusikia taarifa zao kwenye vyombo vya habari hatua yao ya kuamua kujitolea kusaidia shule hiyo baada ya kuhamasishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Filberto Sanga ambaye siyo tu amekuwa akiratibu bali amekuwa pia ashiriki katika ufyatuaji huo wa matofali.

No comments:

Post a Comment