Monday, 24 October 2016
PROFESA LWENGE ATOA MIEIZI MITATU KWA SERENGETI LTD
NA THOMAS MTINGE
WAZIRI wa Maji, Profesa Gerson Lwenge, ameipa miezi mitatu kuanzia sasa, Kampuni ya Serengeti Limited kukamilisha mradi wa kuchimba visima virefu 20 vya maji safi vinginevyo itapigwa faini.
Amesema serikali haiko tayari kuona mradi huo muhimu ukiendelea kuchelewa kukamilika na kuanza kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.
Waziri Lwenge alitoa agizo hilo juzi, baada ya kutembelea mradi huo unaogharimiwa na serikali, ulioko maeneo ya Kimbiji na Mpera, Kigamboni, Dar es Salaam.
Alisema mradi huo utakaogharimu zaidi ya sh. bilioni 18, ulipaswa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu, lakini umechelewa kutokana na changamoto mbalimbali alizopata mzabuni huyo.
Profesa Lwenge alisema kwa sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 56, baada ya visima vinane kukamilika huku saba vikiwa katika hatua mbalimbali za uchimbaji na vitano havijaanza kuchimbwa.
Alisema kati ya visima hivyo, 12 vitachimbwa maeneo ya Kimbiji na vinane Mpera na kuongeza kuwa, lengo la serikali ni kuchimba visima 20 hadi 40, katika maeneo hayo kulikogundulika kuwa na maji mengi.
“Uchunguzi wa awali ulionyesha dalili za uwepo wa maji mengi safi na salama katika maeneo ya Mpera na Kimbiji, hivyo iliamuliwa vichimbwe visima kati ya 20 hadi 40, kwenye maeneo hayo na kuchangia asilimia 30, ya mahitaji ya maji mkoani Dar es Salaam, mji ambao unatarajiwa kuwa na watu wapataomilioni 7.59, ifikapo mwaka 2032,” alisema.
Kwa mujibu wa Profesa Lwenge, tayari serikali imeshamlipa mzabuni huyo zaidi ya sh. bilioni 13 na kumtaka aongeze kasi ya uchimbaji ili vikamilike ifikapo mwishoni mwa Machi, mwakani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Serengeti Limited, Mehrdad Talebi, alikiri kuchelewa kukamilika kwa wakati kwa mradi huo kutokana na kuwepo kwa changamoto mbalimbali.
Talebi alimweleza Waziri Lwenge kuwa, kampuni yake ilikuwa na nia ya dhati kumaliza mradi huo kwa wakati, lakini walikwama kutokana na changamoto hizo na kuahidi kuukamilisha ifikapo Machi, mwakani kama alivyoagiza waziri huyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA), Archad Mutalemwa, alisema mradi huo ilikuwa ukamilike kama ilivyopangwa, lakini sababu alizotoa mkurugenzi huyo ndizo zilizochangia kucheleweshwa.
Hata hivyo, alisema ana imani kuwa baada ya kupatikana kwa vifaa hivyo, kazi hiyo sasa itakamilika Machi, mwakani na kurahisisha upatikanaji wa maji safi na salama Dar es Salaam.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment