Sunday, 30 October 2016

UONGOZI WA RAIS MAGUFULI UNASIFIKA DUNIANI KOTE


UCHAPAKAZI wa Rais Dk. John Magufuli umewavutia watu wengi katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake.
Hatua hiyo imewaweka katika wakati mgumu baadhi ya marais wengine kwa kupata shinikizo kutoka kwa wananchi wao, kutaka waige aina ya uongozi wa Rais Magufuli.
Ukurasa maalumu ujulikanayo kama ‘What Would Magufuli Do’, kupitia mtandao wa Twitter, ulikuwa jukwaa maalumu la kuelezea namna ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya viongozi wa Afrika na endapo Rais Magufuli angeweza kuchukua hatua.
Aidha, makala na maoni ya kumsifia Rais Magufuli na kuwaponda viongozi wa nchi nyingine za Afrika na Ulaya, zimeandikwa katika mitandao ya kijamii na magazeti maarufu duniani.
GUMZO SWEDEN
Gazeti maarufu la kila siku nchini Sweden, ‘Dagens Nytheter’,  liliandika habari ya kumsifia Rais Magufuli kutokana na mafanikio aliyoyapata ndani ya muda mfupi tangu awe rais.
Gazeti hilo limemsifu Rais Magufuli kuwa amewaweka
katika wakati mgumu marais wenzake wa Afrika, kwa sababu wananchi wao wameonyesha wivu kwa Watanzania kwa kupata
kiongozi mchapakazi.
Pia, gazeti hilo limetanabaisha kuwa, kabla ya kuingia Ikulu, tayari Rais Magufuli alikuwa ameshapata maadui mbalimbali, wakiwemo
wa ndani ya chama chake CCM, kutokana na msimamo wake wa kubana matumizi ya serikali.
AFRIKA KUSINI WAMSIFU
Kupitia mtandao wa The SouthAfrican.com, kulichapishwa habari iliyoelezea mambo 10, ambayo Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma, anapaswa kujifunza kutoka kwa Dk. Magufuli.
Mtandao huo ulielezea mambo muhimu aliyoyafanya Rais Magufuli kwa wakwepa kodi, wala rushwa na wazembe serikalini.

Pia, Desemba, mwaka jana, mtandao wa e-NCA ulichapishwa habari yenye kichwa  kisemacho ‘Rais Magufuli siyo kiongozi wa Afrika’.
Habari hiyo ilielezea aina ya utendaji kazi wa Rais Dk. Magufuli kuwa, haufanani na wa viongozi wengine kutoka Afrika, ambao wengi wao wameendekeza rushwa.

Mtandao huo umeeleza kuwa, katika kipindi cha mwezi mmoja tangu aingie madarakani, amekuwa katika mapambano dhidi ya rushwa.
UMOJA WA VIJANA AFRIKA
Rais wa Umoja wa Vijana wa Afrika (Pan Africa Youth Union), Francine Muyumba, alifuta sherehe ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu ateuliwe kuwa kiongozi wa umoja huo, akidai anaunga mkono juhudi za Rais Magufuli.
Muyumba, ameungana na mamilioni ya watumiaji wa mtandao wa Twitter, wenye kumuunga mkono Magufuli uliobeba kauli mbiuya ‘WhatWouldMagufuliDo’.
MALAWI WAMGEUKIA MUTHARIKA
Mtandao maarufu wa Malawi 24, nao ulichapisha habari iliyobeba kichwa cha habari kuwa, Wamalawi hawavutiwi tena na Mutharika, badala yake wamemgeukia Rais Magufuli.
Habari hiyo ilielezea changamoto mbalimbali anazokumbana nazo Rais wa nchi hiyo, Peter Mutharika na kumshauri kuazima japo mbinu chache kwa Rais Magufuli ili aweze kuwahudumia wananchi.
WAZIRI MKUU AUSTRALIA
Nyota ya Magufuli pia imezidi kung’ara na kuwavuruga viongozi wa mataifa mengine baada ya Mhariri wa Gazeti la The Courier Mail la Australia, Rowan Dean, kumtaka Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Malcom
Turnbull, kumuiga Rais Magufuli.
Bila kumung’unya maneno, mhariri huyo aliufananisha uongozi wa waziri huyo katika kipindi cha miezi mitatu cha uongozi kati yake na Rais Magufuli.
Alifafanua kuwa, kiongozi wao ameshindwa kuonyesha utendaji bora baada ya kuwa karibu na matajiri hadi kukosolewa na Bunge la nchi hiyo, kutokana na deni la zaidi ya Dola za Marekani bilioni 400.
BUHARI AKALIA KUTI KAVU
Raia wa Nigeria nao wamevutiwa na uongozi wa Rais Dk. Magufuli hadi kumfanya mhariri wa Gazeti la Mail and Guardian la Afrika Kusini, Charles Onyango-Obbo, kuandika uchambuzi akisema, Dk. Magufuli,  amekuwa kiongozi asiyekuwa na tabia au hulka kama za
viongozi wengine wa Afrika, ambao hudidimiza maendeleo
ya nchi zao.
Pia, jarida la Ventures Africa, liliandika makala iitwayo “Hivi ndivyo Wanigeria wanavyoweza kuiga utekelezaji wa ahadi kutoka kwa Magufuli”.
Pamoja na kuzungumzia kauli mbiu ya ‘Hapa kazi tu’, pia jarida hilo lilimwagia sifa Rais Magufuli, kwa utendaji wake na kutoa wito kwa Rais Mohammed Buhari, kuiga mfano huo.
AIKOSHA GHANA
Rais Dk. Magufuli pia ameibuka gumzo nchini Ghana, ambapo watu mbalimbali walitoa maoni yao, wakidai ni rais wa kipekee katika kizazi cha sasa cha uongozi.
Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Taasisi ya 1Billion Africa, ambayo inajihuisha na miradi mbalimbali ya kusaidia jamii, uongozi na uandishi wa vitabu, Prince Adu-Appiah, alisema Rais Magufuli amekuwa wa pili kati ya viongozi bora Afrika, baada ya Paul Kagame wa Rwanda.
Alisema Afrika haihitaji viongozi wabinafsi ili kuimarisha taasisi za urais na uongozi kwa masilahi ya wananchi wake.
AWAVUTIA WAKENYA
Katika mitandao ya kijamii nchini Kenya, Rais Magufuli amekuwa akizungumziwa mara baada ya kuibuka mjadala unaomtaka Rais Kenyatta, ajifunze kutoka kwa Rais Magufuli.
Rais Kenyatta ametakiwa kupunguza safari za nje, kwa sababu katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake, ameshasafiri zaidi ya mara 40, tofauti na ilivyokuwa kwa mtangulizi wake.
ATOA DARASA MYANAMAR
Rais Dk. Magufuli, ameendelea kutoa darasa kwa viongozi wengine duniani la namna ya kuwatumikia wananachi pasipokujali wadhifa, ambapo Kiongozi wa Chama cha National League for Democracy, ambaye pia ni mwanaharakati wa haki za binaadamu nchini Myanmar, Aung San Suu Kyi, ameamua kufuata mienendo ya Dk. Magufuli.
Imeelezwa kuwa, maamuzi hayo ya Suu Kyi ni matokeo ya wanaharakati na wachambuzi wa masuala ya utawala bora duniani, kutaka viongozi wengine kuiga mfano wa Rais Dk. Magufuli, wa kupambana na ufisadi pamoja na kuhimiza usafi kwa kushiriki zoezi la kuzoa taka.
Katika kuonyesha kulielewa somo la Dk. Magufuli, Suu Kyi, juzi, aliwaongoza wafuasi wa chama chake pamoja na wananchi wa Myanmar, kuzoa takataka kama alivyofanya Rais Dk. Magufuli wakati wa kuadhimisha miaka 54 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Mshindi huyo wa tuzo za Nobel, alifanya usafi kutoa mfano kwa viongozi wa chama chake kilichoibuka na ushindi katika uchaguzi uliofanyika mwaka huu, namna ya kufanya usafi kwa pamoja bila kujali nafasi walizokuwanazo.
Akizoa takataka kwenye kitongoji cha Kawhim, Suu Kyi aligeuka mbogo baada ya kubaini uwepo wa baadhi ya watu wakimshangaa, badala ya kuungana nao kuzoa takataka.
Myanmar, ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kwa jina la Barma, haina mfumo mzuri wa utunzaji na uzoaji taka, hivyo chama hicho kimeamua kuanzisha kampeni maalumu ya kuzoa takataka kwenye maeneo ya umma.
Suu Kyi, aliwaomba wabunge wa chama chake waliochaguliwa hivi karibuni, waokote takataka kama sehemu ya kampeni ya kufanya usafi.
Chama chake cha NLD, kilishinda viti vingi katika uchaguzi uliofanyika mwezi uliopita, ambapo jeshi limeunda kamati maalumu kusimamia mpango wa kukabidhi madaraka kwa chama chake.
Desemba 9, mwaka jana, Dk. Magufuli alikonga vyombo vya habari vya kimataifa pamoja na wachambuzi wa masuala ya kisiasa na utawala bora duniani, baada ya kushiriki kikamirifu kuzoa taka na wananchi wa kawaida bila kujali nafasi yake.

No comments:

Post a Comment