Monday, 31 October 2016

WATUMISHI 13 WATUMBULIWA IRINGA


KATIKA kutekeleza agizo la Rais Magufuli la kutaka kila mtumishi wa umma kuhakikisha anafanya kazi kwa uadilifu na kujituma, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa mkoani hapa, imewatimua kazi watumishi watano huku wengine wanane wakitimuliwa miezi mitatu iliyopita.

Watumishi hao wametimuliwa kwa tuhuma za kushindwa kutimiza wajibu wao wa kutoa huduma bora na kusababisha wananchi wapoteze imani na serikali yao.

Miongoni mwa sababu zilizotajwa kusababisha kutumbuliwa kwa watumishi hao ni pamoja na utoro kazini na wengine kutuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha.

Akitoa taarifa katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Robert Masunya, alisema licha ya watumishi hao kuonywa kwa barua huko nyuma, bado waliendelea na tabia ya ukiukaji kanuni, miongozo, utaratibu na maadili ya kazi zao, ndipo baraza hilo lilipotaka hatua zichukuliwe dhidi yao.

“Kwenye kikao kilichopita, tuliwafukuza kazi watumishi wanane, ambao walikiuka maadili ya utumishi wao wa kazi na leo hii tunawavua nyadhifa na kuwafukuza kazi watumishi wengine watano na hivyo kufanya idadi ya watumishi waliotimuliwa kufikia 13 katika halmashauri yetu,”alisema.

Mkurugenzi huyo aliwataja watumishi hao kuwa ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Migori, Makarius Mtati, ambaye alisema ametimuliwa kazi kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha na utoro kazini.

Masunya alisema mwingine ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Usengelindete,  God Kising’a, anayetuhumiwa kwa tatizo la utoro kwenye eneo lake la kazi huku Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mkulula, Joakhim Kisinini, naye akitimuliwa kwa utoro.

Alimtaja mwingine kuwa ni Godfrey Mwihava, anayetuhumiwa kwa kosa la utoro uliothibitika na mtumishi wa tano aliyefukuzwa ni Sakina Msafiri, mhudumu wa afya katika Zahanati ya Ihomasa, ambaye pia anakabiliwa na kosa la utoro kazini.

Diwani wa Kata ya Masaka, Mathew Nganyagwa, katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, alisema baraza lao halitamvumilia mtumishi yeyote, ambaye hatakwendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano ya yenye kaulimbiu ya 'Hapa Kazi tu.'

Aidha, Nganyagwa aliwataka watumishi wa umma kutimiza wajibu wao kwa kutenda kazi ipasavyo, ili kuleta maendeleo wanayoyatarajia wananchi na sio vinginevyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Steven Mhapa, alisema baraza la madiwani lililopita, liliwafukuza kazi watumishi wanane na sasa limewaondoa wengine watano, lengo likiwa ni kudumisha nidhamu na uwajibikaji kazini.

No comments:

Post a Comment