Wednesday, 9 November 2016

DONALD TRUMP AWA RAIS WA 45 WA MAREKANI, DUNIA YAPIGWA NA BUMBUWAZI


WASHINGTON DC, Marekani

HATIMAYE mfanyabiashara Donald Trump, amechaguliwa kuwa Rais wa 45 wa Marekani, baada ya kumshinda mpinzani wake mkubwa, Hillary Clinton kwa kupata kura 278 dhidi ya 218, alizopata mpinzani wake katika uchaguzi mkuu uliofanyika jana.

Marekani wana utaratibu wao, ambapo kila mshindi anatakiwa kupata kura za jumla za kimajimbo, ambapo kila jimbo lina kura zake katika kupata kura 270 za majimbo yote 50 huku Washington DC, ikiwa haikuunganishwa katika mfumo huo.

Dalili za Trump kushinda kwenye uchaguzi huo zilianza kuonekana mapema, hasa kutokana na kushinda majimbo yote muhimu, ikiwemo  Georgia, Texas, Florida na North Carolina huku Hillary akishinda kwenye jimbo la Virginia.

Katika kura za jumla, Hillary alipata kura 58,875,708, sawa na asilimia 47.61, huku Trump akipata kura 58,842,289, sawa na asilimia 47.58 ya kura zote zilizopigwa na Wamarekani zaidi ya milioni 168, walioshiriki kwenye uchaguzi huo.

Kutokana na ushindi huo, Trump anatarajia kuapishwa Januari 20, mwakani, kuchukua nafasi ya Rais Barack Obama, ambaye amekuwa rais wa taifa hilo kwa miaka minane na kuliletea maendeleo makubwa
kutokana na mabadiliko aliyoyaleta.

Akizungumzia ushindi huo, Trump, ambaye ni mfanyabiashara mkubwa, alisema ushindi huo ni ushindi wa Wamarekani wote na aliwapongeza wote waliompa kura na hatimaye kufanikiwa kuwa rais wa 45 wa taifa hilo.

Trump, alisema uchaguzi huo ulikuwa wa kihistoria na kwamba baada ya uchaguzi, Marekani sasa irudi kuwa kitu kimoja.

Alisema ana furaha isiyo na kifani na kumpongeza Hillary kwa ujasiri aliouonyesha katika kampeni zao, zilizokuwa na ushindani mkubwa na mikwaruzano ya mara kwa mara.

"Nimepigiwa simu na Hillary ya kunipongeza. Namshukuru sana na ninamweleza kuwa nampenda yeye pamoja na familia nzima, walionyesha ni watu jasiri na wakakamavu katika kukomaza demokrasia ya nchi na ameonyesha kuwa yeye ni mwanamke jasiri," alisema. 

Hata hivyo, Hillary amewatangazia wafuasi wake kuwa leo, atatoa msimamo kamili wa uchaguzi mzima pamoja na shukrani kwa wale wote waliomuunga mkono huku akimpongeza Trump kwa ushindi alioupata.

Licha ya Republican kushinda kwenye uchaguzi huo, pia amefanikiwa kupata wabunge wengi katika bunge la wawakilishi kutoka chama chake, ambapo amepata wabunge wawakilishi kwenye baraza la Congress, 236 dhidi ya 191 wa Hillary.

Pia, katika upande wa maseneta, Republican wamepata maseneta 51 dhidi ya 47 wa Democratic wakati katika magavana, Republican wakipata magavana 33 na Democratic 14 na kutoa tafsiri kuwa Republican katika uchaguzi huu, wamefanikiwa kushinda katika maeneo mengi kuliko mategemeo ya watu.  

Kila mmoja hakuwa na mategemo kuwa Trump atafanikiwa kushinda kwenye uchaguzi mkuu, kutokana na kutengwa na watu wengi, ikiwemo viongozi wakuu wa chama chake na watu wenye ushawishi mkubwa nchini humo.

Jambo hilo liliwafanya watu wachache kumpa nafasi ya kuibuka na ushindi kwenye uchaguzi huo, ambapo kwa kiasi kikubwa wameweza kuamini kuwa, matumaini yao yameweza kuleta tumaini kuu kwa Trump kuibuka na ushindi kwenye uchaguzi mkuu huo dhidi ya Hillary.

Sababu ya kwanza iliyompa ushindi ni uwepo wa vuguvugu la watu weupe, ambao katika majimbo ya Ohio, Florida na North Carolina, walimpa kura nyingi Trump, kulinganisha na kipindi kilichopita, ambapo majimbo hayo yalikuwa ngome ya Democratic.

Katika majimbo hayo, watu weupe wengi walipiga kura kwa Trump, huku watu wenye asili Afrika wakimpigia kura Hillary, jambo ambalo lilionyesha wazi kuwa watu wamegawanyika katika majimbo hayo, ambayo yalikuwa yakimuunga mkono Rais Barack Obama.

Kashfa ya kunyanyasa wanawake, inaelezwa kuwa ni sababu ya pili iliyompa ushindi Trump, kutokana na kashfa hiyo haikuweza kumbadilisha mgombea huyo malengo yake ya kuwania urais na ndio maana kila mara alikuwa akijibu majibu ya hovyo walipokuwa wakimuuliza maswali ya namna hiyo.

Suala hilo lilimfanya Trump kukorofishana na watu wengi, wakiwemo watu wakubwa ndani ya chama chake, akiwemo John McCain, waandishi wa habari na kumfanya kuwa mgombea aliyesimama peke yake kwenye vita ya kuwania urais nchini humo na hatimaye kushinda.

Katika hatua nyingine, Rais Dk. John Magufuli jana aliungana na viongozi wengine duniani kumpongeza Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, kufuatia ushindi alioupata.

Katika mtandao wake wa Twitter, Rais Magufuli alisema anampongeza Trump kwa kuchaguliwa kuwa rais mteule wa taifa hilo na amemuahidi Tanzania itazidi kuendeleza ushirikiano na  Marekani.

Rais wa Russia, Valdimir Puttin alituma ujumbe mfupi wa maneno na kusema ana matumaini ataungana naye kuunganisha uhusiano baina ya Russia na Wamarekani.

Waziri wa Mambo ya Nje ya China, naye alikuwa miongoni mwa viongozi waliotuma salamu za pongezi kwa rais huyo mteule, ambapo alisema uhusiano wa kibiashara baina ya China na Marekani, utadumu zaidi na wanaamini wataendelea kuwa pamoja katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.

Pia, Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May alisema anampongeza pamoja na kuamini kuwa uhusiano maalumu baina ya nchi hizo mbili utadumu na anaamini ushindi wa Trump utazidisha uhuru, demokrasia na uendelezwaji wa wananchi kiuchumi.

Aidha, Waziri Mkuu wa India, Nahendra Moodi, naye alimpongeza Trump kwa kusema: "Nina mategemeo ya kufanya kazi zaidi na Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, katika kujenga ushirikiano na kudumisha ulinzi na ustawi wa nchi hizi mbili katika miaka ijayo zaidi"

Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, alisema anaamini ushindi wa Trump utazidisha ushirikiano baina ya Marekani na Japan kwa kuwa nchi hizo zina ushirikiano usiotingishika kwa muda mrefu.

No comments:

Post a Comment