Wednesday, 9 November 2016

BUNGE LABAINI UFISADI WA BILIONI 4.3


BUNGE limegundua ufisadi mkubwa wa zaidi ya sh. bilioni 4.3 za mradi wa uwekezaji wa machinjio ya kisasa ya Gongolamboto, jijini Dar es Salaam.

Katika ufisadi huo, Meneja wa mradi huo, Benjamini Chipazi, raia wa Botswana, alilipwa zaidi ya sh. bilioni moja, licha ya mradi kutokamilika na kufanya kazi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Vedasto Ngombare Mwiru,   alisema mwaka 2005, kampuni hiyo ilimteua Chipazi na kupewa mkataba wa miaka miwili kuwa meneja wa mradi. Meneja huyo alitoka tume ya nyama nchini Botswana.

Akizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa ya LAAC, Ngombare Mwiru, alisema licha ya machinjio hayo kutofanya kazi, meneja huyo alilipwa mshahara wa sh. 532,237,414, sawa na asilimia 30 ya fedha zote zilizokusanywa kwa ajili ya mradi huku akilipiwa nyumba ya kuishi kwa  sh. milioni 40.7.

Pia, alisema meneja huyo alilipwa fedha za vifaa vya ofisi na samani za nyumbani sh. milioni 10.5 na kibali cha kufanya kazi nchini sh. milioni 2.3 na gharama za upembuzi yakinifu sh. milioni 240 na gharama za kusafiri na likizo sh. milioni 197.9.

Alisema mradi huo wa East Africa Meat Company Limited (EAMEATCO LTD) ulikusudia kujenga machinjio ya kisasa katika Kiwanja cha Kiltex, Gongo la Mboto, chenye ekari 63 na kuzishirikisha Halmashauri za Manispaa za Ilala, Temeke na Kinondoni kama wabia wa mradi na baadae walikaribishwa wabia wengine ambao ni Kampuni ya Rheinhold & Mahla (Malasyia) na Kampuni ya Uwekezaji ya Taifa (NICOL).

Ngombare alisema kampuni ya nyama ilikuwa na hisa 7,600, ambapo thamani za hisa katika uwekezaji huo katika jiji  na manispaa zake ilikuwa Dola za Marekani milioni 2.5, R $ M milioni 3.7 na NICOL Dola milioni 3.

Mwenyekiti huyo alisema licha ya mradi huo kutotekelezwa, fedha zote za mradi zilitumika na kubaki sh. 51,814, hali ambayo iliilazimu kamati kuhoji  matumizi yake katika taarifa ya mwaka wa fedha 2012/2013.

Aliongeza kuwa mali pekee iliyobaki katika mradi huo wa machinjio ya kisasa ni ardhi na kusema kamati inaishauri serikali kuhakikisha inasimamia ardhi hiyo kwa manufaa ya wabia wote.

Kutokana na hali hiyo, alisema kamati inataka miradi ya maendeleo isimamiwe kwa ukaribu ili iweze kukamilika kwa wakati na kutumika kama ilivyokusudiwa.

No comments:

Post a Comment