Wednesday, 9 November 2016

MWILI WA SITTA KUWASILI LEO, MUNGAI KUAGWA KARIMJEE

MWILI wa aliyekuwa Spika wa tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samuel Sitta, unatarajiwa kuwasili leo saa 8:30 mchana  kwa ndege ya Shirika la Emirates.

Mke wa marehemu, ambaye pia ni Mbunge wa Urambo, Margareth Sitta, ndiye atakayewasli na mwili wa Sitta, ukitokea Ujerumani, ambako alilazwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Taarifa iliyotolewa jana na familia yake imeeleza kuwa mwili wa Sitta, utapokelewa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Akizungumza jana, nyumbani kwa marehemu, baada ya kuhani msiba huo, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rajabu Luhwavi, alisema alimfahamu marehemu Sitta tangu miaka ya 1970, akiwa kiongozi wa umoja wa vijana wa TANU katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Alisema Sitta ametekeleza majukumu mbalimbali ya kitaifa kwa uwezo mkubwa, akiwa miongoni mwa makamanda wa vijana mkoa wa Tabora, aliyeonyesha kipaji chake ndani ya chama katika kutumikia nchi, alikuwa mkweli, mwenye maono na uthubutu wa kile anachokiamini.

Alisema Sitta alikuwa na vipaji vingi vya uongozi na uwezo mkubwa wa ushawishi na kujenga hoja,kujieleza na kuwa na wafuasi wengi waliomuamini kauli na vitendo vyake.

“Sitta pia alithibitisha uwezo wake wa kufanya kazi akiwa waziri katika wizara mbalimbali na taasisi alizopitia hadi Spika wa Bunge, ambapo ameandika rekodi ya pekee ya nchi ambayo itahifadhiwa na kudumu katika kipindi kijacho,”alisema.

Luhwavi alisema CCM imepoteza kiongozi mahili na mashughuli na kwa kutambua na kuenzi mchango wake, itahakikisha inatunza historia yake.

“CCM tunawiwa na madeni makubwa ya kutotunza historia ya viongozi wa chama chetu, lakini kwa sasa mimi naibu katibu mkuu nitalipa umuhimu jambo hili ili kuandika historia ya wanachama na viongozi waliotumikia kwa dhati,”alisema.

Alisema Sitta atabaki kuwa mfano wa kihistoria kwa vijana na CCM itamkumbuka kwa uwezo wake mkubwa wa ushauri wenye mawazo mapana na wakati wote kuwa tayari kutumikia nchi.

Kwa upande wake, mwanasiasa mkongwe, Christopher Mzindakaya alisema alianza kumfahamu Sitta, mwaka 1974,  wakiwa vijana waliolelewa na Mwalimu Nyerere katika uongozi na kufanya kazi pamoja kama wakuu wa mikoa na mawaziri.

 “Aliniomba ushauri alipotaka kugombea ubunge, nikamtia moyo kwa kuwa niliamini ni mfanyakazi mzuri aliyeiwezesha nchi kujulikana katika dunia kwa kuleta tuzo kutokana na utendaji wake uliotukuka TIC,”alisema.

Alisema marehemu Sitta alistahili kujiita mtu wa viwango kwa kuwa  ndiye aliyepandisha hadhi ya bunge na unapofanya naye kazi
siyo mtu wa kusubiri kesho kwa jambo lililokuwa katika maamuzi yake.

Waziri mstaafu wa Wizara ya Fedha, Basil Mramba, alisema kifo
cha Sitta kimempa mshtuko kwa kuwa walifahamiama tangu mwaka 1961, wakiwa wanafunzi wa Tabora Boys.

“Tulisaidiana mengi hata katika uongozi, Sitta alikuwa mahiri na ana mchango mkubwa kwa taifa, ambao bado unahitajika.
Ameondoka mapema, lakini kama nchi, tutaendelea kutumia busara zake,”alisema.

MUNGAI KUAGWA LEO

Wakati huo huo, mwili wa aliyekuwa Waziri wa Elimu na  Mafunzo  ya Ufundi na Mbunge wa  Jimbo la Mufindi, Joseph Mungai, unatarajiwa kuagwa leo, kwenye ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.

Mara baada ya kuagwa, mwili huo utasafirishwa kwenda Mafinga mkoani Iringa kwa  ajili ya maziko yatakayofanyika Jumamosi.

Akizungumza  na  waandishi wa habari, Dar es Salaam, jana, kwa niaba ya familia, mtoto wa marehemu, William  Mungai, alisema utoaji wa heshima za mwisho umepangwa kuanza saa tano asubuhi.

Alisema wameamua mwili wa baba yao uzikwe Mafinga kwa sababu alikuwa kiongozi wa jimbo hilo kwa zaidi ya miaka 35, akiwa mbunge.

William alisema baba yake alifariki kutokana na kuugua ugonjwa wa tumbo.
JPM ATUMA RAMBIRAMBI
Rais  Dk. John Magufuli, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, kufuatia kifo cha Mbunge mstaafu wa Jimbo la Mafinga mkoani Iringa na Waziri mstaafu katika Serikali, Joseph Mungai.

Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshtuko taarifa za kifo cha  Mungai, ambaye alimfahamu kama mchakapakazi, mtu aliyesimamia alichokiamini, mpenda maendeleo na aliyependa kufanya kazi kwa ushirikiano.

“Nilifanyakazi na Mungai, ambaye wakati akiwa Waziri wa Elimu na Ufundi, mimi nilikuwa Waziri wa Ujenzi, tulikuwa tukishirikiana na kushauriana kwa mambo mengi yenye manufaa kwa Taifa,"alisema.

Alisema  amesikitishwa sana na kifo chake na  kumuomba  Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, kufikisha salamu hizo kwa  familia, wananchi wa jimbo la Mufindi  pamoja na wabunge.

CCM YAMLILIA
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Abdulrahman Kinana, amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu, kufuatia kifo cha  Mungai.

Kinana alisema marehemu Mungai, ameshika nyadhifa mbalimbali za uongozi na utumishi katika Chama na serikali, akiwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Mkuu wa Mkoa wa Iringa na mbunge kuanzia miaka ya 1970 hadi 2010 na waziri katika wizara mbalimbali za serikali katika awamu ya kwanza hadi ya nne.

Kinana alisema Mungai, atakumbukwa na wana-CCM na wananchi wa mkoa wa Iringa na Tanzania, kwa kuasisi na kuendeleza shamba kubwa la miti la SAOHILL na kwamba, wataendelea kuuenzi na kuuthamini mchango wake huo.

No comments:

Post a Comment