Tuesday, 15 November 2016

VIGOGO WANAODAI NGONO MAOFISINI WAONYWA


MEYA  wa Jiji la Tanga, Muhina Mustafa, ameitaka jamii kukemea vitendo vya ukatili wa kijinsia na kudai ngono katika sehemu za kazi.

Akifungua kongamano la kujifunza kwa kubadilishana uzoefu juu ya masuala ya ukatili wa kijinsia, lililoandaliwa na Asasi ya kiraia ya Tree of Hope, juzi, Mustafa, alisema kuna baadhi ya watu hudai ngono kinyume na sheria ili kutoa msaada.

Alisema tabia hiyo imejengeka katika baadhi ya maofisi, hivyo kuitaka jamii na viongozi wa dini kwa pamoja, kulitokomeza ikiwa ni pamoja na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

“Leo nimepata faraja kuwepo hapa na makundi mbalimbali, wakiwemo viongozi wetu wa dini. Kwa kweli sote tunajua kuwa, wapo baadhi ya wakuu maofisini hawatoi huduma bila kuomba ngono,” alisema Mustafa na kuongeza:

“Kila mmoja wetu awe balozi mwema wa kukemea vitendo hivi kwani vinarejesha nyuma kasi ya maendeleo na ile fikra ya hapa ni kazi tu. Binafsi kwa nafasi yangu, nitakuwa balozi namba moja,” alisema

Aliwataka viongozi hao wa dini kwa kushirikiana na  Tree of Hope, kuhakikisha wanatoa elimu katika majengo yao ya ibada na kuwa na ada ya utoaji wa elimu ya mtaa kwa mtaa.

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Abdalla Mbena, ambaye ni kiongozi wa dini, mkazi wa Donge, alisema sheria iliyopo ya ukatili wa kijinsia ni ndogo, hivyo kuitaka serikali kuifanyia marekebisho ili kuongeza adhabu ya kosa.

Alisema uwepo huo wa sheria imekuwa ada kwa waombaji wa ngono na ukatili wa kijinsia maofisini na mahotelini, kuendelea kufanya vitendo hivyo, jambo linalotakiwa kukomeshwa.

“Ili kukomesha vitendo vya kikatili na uombaji wa ngono maofisini, ni lazima kufanyiwa marekebisho sheria kwa kuiongezea ukali wa adhabu ili  kila mmoja kusimama katika nafasi yake na kutoa huduma kwa mujibu wa sheria,” alisema Mbena

Aliwataka wajumbe wa kongamanpo hilo kurejea katika maeneo yao kwa kuazimia kila mmoja kuwa balozi wa kweli kwa kuwafichua na kuwapeleka katika vyombo vya sheria waombaji wa ngono maofisini.

No comments:

Post a Comment