Sunday, 6 November 2016

WABUNGE WA UPINZANI WAONYWA

WABUNGE wa upinzani wameonywa kutowatumia vibaya wananchi na kuwachonganisha na rais baada ya wale wanaowaunga mkono kubanwa walipe kodi.

Akichangia mjadala wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/2018, uliowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alisema wapinzani wamekuwa wakiwatumia vibaya wananchi ili yale anayofanya Rais Dk. John Magufuli yaonekane hayafai.

Lugola alisema bunge limepoteza mwelekeo na kuwa la kulialia huku likimlaumu Rais Magufuli kwa kuwa amewabana waliokuwa wakikwepa kodi, licha ya rais kuwaomba wabunge wamsaidie kuyatumbua majipu.

Mbunge huyo alisema rais aliwaomba wabunge wamsaidie kutekeleza mipango mbalimbali kwa ajili ya kuijenga nchi, baada ya kuwaona wafanyabiashara waliozoea kukwepa kodi wakibanwa na kuanza kulalamika biashara zimekufa.

"Wengine walizoea kusafiri mara kwa mara, wengine kupokea posho na kula maandazi makubwa, lakini sasa hivi wanakula maandazi ya sentimita mbili, kwenye kamati tumebanwa posho, hali ambayo inatufanya kulialia baada ya kushikwa pabaya na kuwasingizia wananchi hawana fedha.

“Wewe Freeman Mbowe umepewa gari na serikali na unawekewa mafuta, unakula kiyoyozi saa 24, halafu unakuja hapa nnasema serikali imefilisika na kuwachonganisha wananchi na rais wao,” alisema Lugola.

Aliongeza kusema kuwa wapinzani wanapaswa kutumia taaluma zao vizuri kwa wananchi na kuwashauri vizuri wabunge wenzao na kumtaka Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (CHADEMA), kuutumia uchungaji wake kusema ukweli na kutumia vifungu vilivyopo katika biblia.

“Msigwa ndugu yangu, japo haupo bungeni, hebu tumia taaluma yako kuwashauri wenzako wawe katika safari hii, ambayo Rais Magufuli ndiye dereva anayetupeleka Kaanani, sehemu ambayo kuna maisha mazuri na katika nchi ya ahadi,”aliongeza Lugola.

Naye Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), alisema wapinzani wamekuwa na kazi ya kusema ‘serikali imefilisika’, wakati inalipa mishahara na madeni inayodaiwa na kusahau kuwa kiongozi wao Mbowe ndiye aliyefilisika na kushindwa kulipa madeni.

Lusinde alisema uchumi unapokuwa ni lazima uonyeshe kwenye maisha ya wananchi wake, hususan wa vijijini, tofauti na uchumi unaoonyeshwa katika takwimu zilizopo katika makaratasi, ambazo ndizo zinazopigiwa kelele na wapinzani.

No comments:

Post a Comment