Wednesday, 9 November 2016

WAKUU WATATU WA SHULE ZA SEKONDARI MBARONI


Na Angela Sebastian, Bukoba

JESHI la Polisi Wilayani Missenyi mkoani Kagera, linawashikilia wakuu wa shule tatu za sekondari wilayani humo, kutokana na tuhuma mbalimbali, ikiwemo utoro katika vituo vya mitihani na kusinzia katika chumba cha mtihani.

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Augustine Ollomi, alisema jana kuwa, walimu wawili waliokamatwa, ambao ni wasimamizi wakuu wasaidizi, hawakukutwa kwenye shule zao wakati mitihani ikiendelea.

Aliwataja walimu hao kuwa ni Primus Rwejuna (53), mkuu wa shule ya sekondari Ruzinga na Richard Kagirwa (48), mkuu wa shule ya sekondari Nkenge.

Kamanda Ollomi alimtaja mwalimu wa tatu kuwa ni Mayala Samwel (33), aliyekuwa akisimamia mtihani wa shule ya sekondari Buyango, ambaye alikutwa amesinzia kwenye dawati wakati mtihani ukiendelea.

Alisema baada ya kukamatwa, wote watatu waliondolewa kwenye orodha ya walimu wanaosimamia mtihani na nafasi zao kupewa walimu wengine. Pia waliamriwa kurudisha posho walizokuwa wamepewa.

Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Limbe Moris, alisema kitendo kilichofanywa na walimu hao ni ukiukwaji wa maadili ya usimamizi wa mitihani.

Mkurugenzi huyo alisema walimu hao watachukuliwa hatua za kisheria, na kwamba hatua za awali zilizochukuliwa ni kurudisha posho walizopewa kwa ajili ya kusimamia mitihani hiyo ya kidato cha nne inayoendelea kote nchini.

No comments:

Post a Comment