Wednesday, 9 November 2016

LEMA AENDELEA KUSOTA RUMANDE


MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), ameendelea kusota rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi mkoani hapa, baada ya polisi kutompeleka mahakamani.

Lema, alikamatwa Novemba 2, mwaka huu, katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma kabla ya kurudishwa Arusha kwa ajili ya kuhojiwa zaidi.

Mapema jana asubuhi, viongozi wa CHADEMA mkoa wa Arusha, waliwajulisha wafuasi wa chama hicho na waandishi wa habari kuwa, mbunge huyo angefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, saa nne asubuhi.

Kutokana na taarifa hizo, viogogo wa CHADEMA wakiongozwa na katibu wake Kanda ya Kaskazini, Amani Gulugwa pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Arusha, Joyce Mukya, walifika mahakamani hapo wakiwa wameongozana na baadhi ya madiwani na kumsubiri kwa zaidi ya saa saba bila mafanikio.

Wengine waliofika katika mahakama hiyo ni pamoja na wafuasi wachache wa CHADEMA, ambao hawakuwa na viashiria vyovyote kuonyesha wanamsubiri mbunge wao.

Uchache huo wa wafuasi kufika mahakamani hapo, umeonyesha tofauti kubwa inayoendelea kujitokeza kila siku, ikiashiria kwamba, wengi wameanza kumchoka Lema, baada ya kupoteza mvuto kwa wafuasi wake, ambao huko nyuma walikuwa wakifurika mahakamani, wakiwa na bendera za chama hicho huku wengine wakivalia sare za CHADEMA.

Baada  ya Mwanasheria wa CHADEMA, John Malya, kuona mteja wake haletwi mahakamani kama ilivyokuwa imepangwa awali, alifungua maombi ya jinai namba 56 ya mwaka huu, katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha yenye maombi matatu.

Malya aliyataja maombi hayo kuwa ni pamoja na kuiomba mahakama kuiamuru polisi kumleta Lema mahakamani, dhamana yake kusikilizwa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha na kulipa gharama zote za kesi hiyo.

Kwa mujibu wa Malya, maombi hayo yatasikilizwa leo, mbele ya Jaji Salma Msengi na kwamba, anahangaikia hati ya kuitwa mahakamani, Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Kati, Mkuu wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha, Mkuu wa Polisi Mkoa wa Arusha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini.

Wakili huyo alidai amefungua maombi hayo kutokana na polisi kukiuka sheria, ambapo mtuhumiwa huyo amekaa rumande kwa zaidi ya saa 175, wakati sheria inaelekeza wazi kuwa polisi wanatakiwa kukaa na mtuhumiwa kwa saa 24 pekee.

MBOWE AKWAA KISIKI
Wakati Lema akiendelea kusota rumande, jitihada za Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, kutaka kumuona mbunge huyo juzi, ziligonga mwamba baada ya polisi kumkatalia.

Mbowe alifika kituoni hapo Novemba 6, mwaka huu, kwa ajili ya kumjulia hali, lakini polisi walimgomea na kuondoka bila ya kuonana na mbunge huyo.

Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema Lema anakabiliwa na tuhuma za kutoa kauli za uchochezi na kuvuruga amani ya nchi,  wakati akihutubia wanachi wa jimbo la Arusha Mjini kwa nyakati tofauti, kupitia ambayo mikutano ya hadhara ndani ya jimbo lake.

 “Lema alikuwa na kibali cha kufanya mikutano yake katika jimbo la Arusha Mjini, kuzungumza na wananchi, lakini katika mikutano hiyo, alitoa kauli za uchochezi za kuvuruga amani ya nchi,”alisema.

No comments:

Post a Comment