WATU 18 wamepoteza maisha na wengine watatu kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari mawili, yaliyogongana uso kwa uso katika kijiji cha Nsalala, mkoani Shinyanga.
Katika ajali hiyo, dereva wa gari dogo lenye namba za usajili T 232 BQR, aina ya Toyota Noah, alikuwa akijaribu kuyapita magari mawili yaliyokuwa mbele.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Muliro Jumanne, alisema ajali hiyo ilitokea juzi, saa 1.30 usiku, katika kijiji cha Nsalala, wilayani Shinyanga Vijijini.
Kamanda Jumanne alisema Noah hiyo, iliyokuwa ikitoka Nzega kwenda Tinde, iligongana na Lori semitrailler, lenye namba za usajili T198 CDQ na tela lenye namba T283CBG.
Aliongeza kuwa Noah hiyo ilikuwa ikiendeshwa na Self Muhamed (32), mkazi wa Tinde huku lori lilikuwa likiendeshwa na Aloyse Kavishe (46), mkazi wa Dar es Salaam, ambao wote wanashikiliwa na polisi kwa hatua zaidi za kisheria kuhusiana na ajali hiyo.
“Watu waliokufa ni 18 na majeruhi watatu. Kati ya waliokufa, wanaume ni saba, wanawake tisa na watoto wawili. Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Shinyanga. Tisa kati ya hiyo imeshatambuliwa na ndugu,"alisema Kamanda Jumanne.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, ajali hiyo ilisababishwa na uzembe wa dereva wa Noah, aliyejaribu kuyapita magari yaliyokuwa mbele yake.
Aliwataja waliokufa kwenye ajali hiyo na kutambuliwa kuwa ni Daud Maja (34), mkazi wa Kishapu, Dina Masanja (20), Chausiku Kasapa (42), Specioza Dotto (23), Ester Kasapa (59), Vicent Nzamala (23), Emmanuel Jumanne, Endrew Mambosasa (33) wote wa kazi wa Tinde.
Wengine ni Maganga Lubala, mkazi wa Uyui, Tabora na Debora Maingu, mkazi wa Samuye, Shinyanga.
Kamanda Muliro aliwataka madereva kufuata sheria za barabarani ili kupunguza ajali zinazoweza kuepukika, kwani baadhi zinasababishwa na uzembe wa madereva na kugharimu maisha ya watu na mali.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga, Daniel Maguja, alithibitisha kupokea miili hiyo pamoja na majeruhi watatu, wakiwemo watoto wawili, ambao ni Hamisa Matiko (5) na Salima Kiza (mwaka mmoja), ambao mama yao alifariki katika ajali hiyo.
No comments:
Post a Comment