RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema hakuna mahakama yoyote au Jumuia ya Kimataifa, ambayo ina uwezo wa kubadilisha matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar, yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Machi, mwaka huu.
Amesema uchaguzi huo ulifanyika kwa mujibu wa katiba ya nchi na kwamba, serikali iliyoko madarakani itaendelea kuwatumikia wananchi wa Zanzibar, kwani imechaguliwa kwa kuzingatia matakwa ya katiba ya Zanzibar.
Dk. Shein, aliyasema hayo jana, Micheweni, Pemba wakati akizungumza na wananchi, baada ya kukagua ujenzi wa ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya wilaya hiyo na kuwasisitiza wananchi, kupuuza kauli za kuwepo na mahakama, ambayo itatengua matokeo hayo.
Alisema ni vyema wananchi kuzipuuza propaganda zinazoendelea kusambazwa kwamba, Umoja wa Mataifa (UN), una uwezo wa kumtoa madarakani, badala yake waendelee kufanya kazi za kujiletea maendeleo, wakisubiri uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2020.
Alisema ataendelea kuwa Rais wa Zanzibar hadi mwaka 2020, ambapo kwa sasa anaendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020.
“Mimi ndiye rais halali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), hakuna mahakama yoyote, Jumuia ya Kimataifa, wala taifa la nje, ambalo lina uwezo wa kuniondoa madarakani. Cha msingi wananchi nawaomba mzipuuze propaganda hizo, badala yake jiandaeni kwa uchaguzi wa mwaka 2020, ”alisema.
Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi wa wilaya ya Micheweni kwamba, serikali yake imepanga kuwashawishi wa wawekezaji kuwekeza wilayani humo ili kusaidia kupatikana ajira kwa vijana kupitia sekta ya utalii.
Mapema, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Haji Omar Kheir, alisema ukumbi huo wa mikutano umejengwa kwa lengo la kusogeza huduma za kijamii kwa wananchi wa wilaya hiyo na wilaya nyingine jirani.
Waziri Kheir alisema ukumbi huo utakapokamilika, utapunguza tatizo la wananchi wa wilaya hiyo na kuongeza kuwa, wizara imejipanga kuhakikisha ukumbi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa.
“Kwa mujibu wa mipango, ambayo wizara imejipangia ni kwamba, ukumbi huu utakamilika ndani ya kipindi chako cha uongozi na utasaidia kuongeza mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni,”alisema.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa ukumbi huo, Katibu Tawala Mkoa wa Kaskazini Pemba, Yussuf Mohammed Ali, alisema umepangwa kutekelezwa ndani ya kipindi cha miaka mitano (2013-2018) na unakadiriwa kugharimu sh. milioni 300.
Alisema hadi kufikia hatua iliyo kwa sasa sh. milioni 122,099,088, ambazo ni sawa na asilimia 95 ya fedha hizo, ambazo ni kutoka kwenye vyanzo vya mapato vya halmashauri na asilimia tano ni mchango kutoka mifuko ya maendeleo ya jimbo.
Katika hatua nyingine, Dk. Shein alisema pamoja na kuongezeka kwa gharama za ujenzi wa barabara, serikali itaendelea kutimiza ahadi zake za kujenga barabara ili kurahisisha usafiri kwa wananchi wa maeneo mbalimbali nchini.
Dk. Shein alisema hayo wakati akizungumza na wananchi wa mkoa wa Kusini Pemba kwa nyakati tofauti, katika ziara yake inayoendelea mjini hapa, ambapo jana, alikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara mbalimbali za mkoa huo.
Katika ziara hiyo, Dk. Shein amekagua ujenzi wa barabara ya Mgagadu-Kiwani yenye urefu wa kilomita 7.6, ambapo hadi sasa kilomita 3.1 zimeshawekewa lami. Barabara nyingine ni Mgagadu–Kwautao (5.3km), Kuyuni-Ngomeni (3.0 km) na Kipapo–Mgelema (6.0km).
No comments:
Post a Comment