Na Joseph Ishengoma
Serikali imesema kuwa imedhamiria kwa dhati kupambana na rushwa za kila aina ili kujenga jamii yenye maadili na inayochukia vitendo vya rushwa.
Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Mwandisi Balozi John Kijazi amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha matembezi ya watumishi wa taasisi zinazosimamia maadili, uwajibikaji, utawala bora, haki za binadamu na mapambano dhidi ya rushwa.
Matembezi hayo yameanzia katika viwanja vya Karimjee hadi Mnazi Mmoja na kuzishirikisha taaasisi zinazohusika na masuala ya utawala bora.
Taasisi hizo ni Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa, mamlaka ya kudhibiti manunuzi ya umma, na ofisi ya Taifa ya ukaguzi wa hesabu.
Taasisi nyingine ni Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Tume ya Utumishi wa Umma, na Tume ya Haki za Binadamu.
“Ipo mifano ya sehemu ambazo rushwa imekithiri kutokana na vitendoi vya rushwa na ufisadi. Kiongozi mkubwa anashindwa kumsimamia mtu aliyechini yake kama sheria ya maadili inavyomtaka kwasababu yeye mwenyewe mikono yake si misafi,” amesema na kuongeza kuwa , “matokeo yake hata mtu awe na mali nyingi, bado ataendelea kula rushwa bila kikomo”.
Balozi Kijazi amesema, “serikli ya awamu ya tano imedhamiria kupambana na rushwa ya aina zote kwa lengo la kujenga jamii yenye maadili inayochukia vitendo vya rushwa na ufisadi.”
Kwa mujibu wa Balozi Kijazi, jitihada za serikali ni kuondokana na hulka ya ubinafsi na uroho na kujenga utamaduni na tabia ya kijitolea.”
Aidha Katibu Mkuu Kiongozi ametoa wito kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari kuonyesha uzalendo kwa kuielimisha jamii kuhusu maswala ya maadili nchini.
“Natoa wito kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari kuonyesha uzalendo kwa taifa letu kwa kuielimisha jamii kuhusu kujenga, na kukuza maadili, haki za binadamu, uwajibikaji, utawala bola na mapambano dhidi ya rushwa,” amesema.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Kamishna Valentino Mlowola ameeleza kuwa lengo la matembezi hayo ni kutuma ujumbe kwa wananchi kuhusu kujenga na kukuza maadili, haki za binadamu, uwajibikaji, utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa.
Kamishna Mlowola amesema, kuanzia Jumatatu ijayo, taasisi zinazohusika na masuala ya utawala bora zitakuwa na wiki ya utoaji huduma katika viwanja vya Mnazi Mmoja ili kupokea kero na malalamiko ya wananchi na kisha kuyashughulikia.
“Hii ni moja ya kampeini ya taasisi husika kuikataa rushwa, kujenga maadili na misingi ya uadilifu na kuhamasisha jamii kujua haki zao,” amesema.
Kampeini hii ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu iliyoanza Novemba 10 mwaka huu ambayo kilele chake ni Desemba 10, 2016.
No comments:
Post a Comment