Sunday 26 February 2017

RIDHIWANI: NATAMANI KUWA KATIBU MKUU WA CCM


MBUNGE wa Chalinze, Ridhiwan Kikwete, amesema katika ndoto zake hajafikiria wala kuota kuwania urais wa Tanzania, lakini angetamani siku moja itokee awe Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Amesema laiti asingelelewa kwenye mikono ya kisiasa na uongozi chini ya  baba yake, pengine angekuwa mtu wa hovyo,  asiyependeza au kutazamika katika mwonekano wa utii na kufuata maadili mema kama anavyoishi sasa.

Ridhiwani alisema hayo jana, wakati akishiriki kipindi cha 360, kinachorushwa na Clouds TV, Dar es Salaam, alipokuwa akijadili mada na azma ya serikali ya awamu ya tano ya Tanzania kuwa nchi  ya viwanda.

Alisema maisha yake kimsingi yanatokana na kufanikiwa kupata malezi bora, uangalifu makini, kupigwa msasa na kufundishwa miiko na kanuni katika maisha ya staha, nidhamu, heshima, siasa na uongozi.

"Maisha yangu yamepata msukomo utokanao na malezi mema ya mzazi wangu. Nimekulia katika mikono ya usimamizi na malezi ya kimaadili, heshima na nidhamu, hadi sasa najifunza mengi kutoka kwa baba yangu katika mtazamo wa nadharia ya siasa, uongozi na heshima,"alisema.

Alisema hamu, kiu na ndoto aliyonayo anatamani siku moja itokee awe Katibu Mkuu wa CCM, ingawa sio baada ya kuondoka kwa Katibu Mkuu wa sasa, Kanali mstaafu Abdulrahman Kinana.

"Katika maisha yangu sijawahi kuota wala kufikiria urais, natamani sana siku moja  itokee niwe Katibu Mkuu  wa CCM, lakini sitamani ukatibu mkuu baada ya Kinana kwa kuwa hilo kwa sasa halimo akilini mwangu,"alisema.

Aidha, akizumgumzia mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, alisema mpango mkakati huo ni jambo linalowezekana, ikiwa Rais Dk. John Magufuli ataungwa mkono na viongozi wengine katika ngazi husika, wenye uthubutu wa kubuni, kutenda na kufanikisha.

Ridhiwani alisema Rais Dk. Magufuli hana uwezo wa kupeleka viwanda katika kila kona ya nchi, bali wasaidizi wake, viongozi wa serikali, wabunge na wananchi wenyewe ndiyo wahusika wakuu katika kufanikisha lengo hilo.

Akizumgumzia juhudi za mkoa wa Pwani, katika dhima ya ujenzi wa viwanda, alisema chini ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Everist Ndikolo, kuwashirikisha wakuu wa wilaya na wataalamu husika, Pwani imeweza kuwa mfano kwa ujenzi wa viwanda vingi vya kisasa.

"Tumekuwa na timu ya mkakati ya mkoa wa Pwani, chini ya mkuu wa mkoa,  inayoainisha vipaumbele vyetu kiuchumi kwa kutazama mazingira yetu.
Mpango wetu ni kujenga viwanda bora vyenye tija, uzalishaji na kutoa ajira,"alisema.

Pia, mbunge huyo wa Chalinze, akikizumgumzia kiwanda cha vigae kilichoko katika jimbo lake, alisema kitamaliza hadithi na mazoea ya wafanyabiashara kufuata bidhaa nje ya nchi, badala yake kutokana na ubora wa bidhaa , watanunua katika kkwanda hicho.

Hata hivyo, aliwashauri  wawakezaji, ambao wana nia ya  kuwekeza na kujenga viwanda nchini, watambue umuhimu wa kuwapa kipaumbele wenyeji wa maeneo husika kwa dhumuni la kuimarisha ujirani mwema, ulinzi na mahusiano ya kijamii.

No comments:

Post a Comment