Tuesday 21 February 2017

WAUZA 'UNGA' SASA WADAIWA KUWAFUATA 'MATEJA' VITUONI


NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla, amewaonya vigogo wa dawa za kulevya wanaowafuata wateja katika vituo vya tiba ya dawa za methadon.

Amelitaka Jeshi la Polisi kufanya doria katika vituo hivyo na watakaobainika kuwafuata wanaopata tiba, waunganishwe katika kesi za dawa za kulevya.

Amewataka wafanyabiashara hao kutambua kuwa, hakuna anayepigana vita na serikali akashinda.

Dk. Kigwangalla pia alisema wanasiasa wasema hovyo wanaojaribu kupingana na wanasayansi kuwa dawa hizo hazisaidii bila hoja za kitaalamu, wanatafuta umaarufu na wanatumika kwa mlango wa nyuma na wauzaji wa dawa hizo ili kupambana na vijana wanaonusurika.

Akizungumza jana, alipotembelea vituo vya tiba ya dawa za kulevya katika Hospitali za Mwananyamala na Temeke, Dk. Kigwangalla alisema amesikitishwa na taarifa za vigogo wa dawa hizo kuwafuata wateja walioacha dawa hadi katika vituo.

“Inasikitisha kuona wanasogelea hadi katika vituo hivi. Naagiza sasa watoa huduma na wateja wenyewe, muwasiliane na jeshi la polisi kitengo maalumu na waweke kambi vituo vyote kuwafuatilia vigogo hao,”alisema.

Aliongeza kuwa vita hiyo ni kubwa kwa kuwa mtumiaji mmoja wa dawa za kulevya anatumia sh. 10,000 hadi sh. 150,000, kwa siku hivyo watumiaji zaidi ya  3,351, waliopo katika vituo, wameondoa sokoni zaidi ya sh. bilioni 70 kwa siku.

“Ni lazima watengeneze mbinu mpya ya soko lao ili kuwarudisha wateja hao, lakini tunawaambia hakuna anayepigana vita na serikali akashinda, tutahakikisha tunashinda,”alisema.

Dk. Kigwangalla alisema msingi wa huduma hiyo ni kuwaondoa watumiaji wa dawa za kulevya na kuwa sawa, mpango ambao ni wa kipekee Afrika Mashariki na Tanzania inafanya vizuri.

Alisema huduma ya kuwaunganisha wagonjwa hao na jamii bado inalega kutokana na changamoto zilizopo.

Alisema serikali inatambua katika kipindi hiki cha kudhibiti biashara ya dawa za kulevya, matumizi ya dawa za methadon yataongezeka na kuadimika sokoni, hivyo ni lazima kuboresha huduma na miundombinu katika vituo vilivyopo.

“Wote tunafahamu mtu anapokosa dawa za kulevya, anachanganyikiwa, ni lazima kupata tiba kwa haraka. Ifanyike tathimini ya haraka na kila kanda kuhakikisha kuna kituo na kila hospitali ya mkoa ndani ya miezi sita,”alisema.

Pia, alisema wizarani kwake ni lazima kuimarishwe kitengo cha tiba ya dawa za kulevya kwa kuongeza  wataalamu wa tiba, kinga na madaktari wa akili ili kuboresha huduma na kila mkoa kuwa na daktari bingwa mmoja na kila kanda wasiopungua watatu.

Alisema serikali pia imeongeza dawa hizo kutoka 90 hadi 120, kutokana na kuelemewa na wagonjwa wengi kwa sasa.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Afya ya Akili, Cassian Nyandindi, alisema kituo hicho kinakabiliwa na uchache wa watoa huduma, ambapo kati ya wagonjwa 1,388, wanaokula dawa kila siku, 100 wanahitaji kuonwa na daktari ambapo madakati hao ni wawili.

Alisema kituo hicho kina changamoto pia kwa wagonjwa wa akili, ambao wakipata matibabu na kubadilika, wanashindwa kuendelea na maisha ya kawaida kutokana na kutokuwa na kazi, kuwa tegemezi na kutengwa na jamii na kujikuta wakishawishika kurudia maisha ya awali.

No comments:

Post a Comment