Monday, 22 May 2017

WASOMI, WACHUMI WAWASHANGAA WABUNGE NA WANASIASA





NA JACQUELINE MASSANO, WILLIAM SHECHAMBO
BAADHI ya wasomi na wachumi nchini, wamesema suala la Tanzania kuwa nchi  ya uchumi wa viwanda linawezekana, ingawa litachukua muda mrefu kukamilika.
Wamesema sio sahihi kudai kwamba, itakuwa ndoto kwa Tanzania kuwa ya viwanda, kama baadhi ya wabunge walivyokaririwa wakisema bungeni, wiki iliyopita.
Kauli za wasomi na wachumi hao, zimekuja siku chache baada ya baadhi ya wabunge kudai kuwa, itakuwa ni ndoto kwa Tanzania kuwa ya uchumi wa viwanda, bila kufungamanisha sekta za kilimo na uzalishaji wa malighafi.
Wabunge hao walitoa kauli hizo walipokuwa wakichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, kwa mwaka wa fedha 2017/18.
Walidai kuwa, Tanzania bado haijafungamanisha sekta hizo, ambazo muhimu wa ukuaji wa sekta hiyo.
Wakizungumza na Uhuru, jana, baadhi ya wasomi na wachumi walisema, suala la Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda sio la bajeti moja, bali inahitajika uvumilivu kwa sababu linawezekana.
“Jambo kama hili limefanyika hata Ghana na limewezekana, sio jambo ambalo ni la Tanzania tu, ni kwa watu wenye muono wa mbali. Nadhani lengo la Rais Dk. John Magufuli ni kuhakikisha kuwa tunajenga uchumi wa viwanda. Ni azma nzuri kwa watoto wetu na vizazi vijavyo,” alisema Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Banna.
Profesa Banna alisema mtu yeyote anayepinga azma hiyo ya Rais Magufuli, Utanzania wake utakuwa na utata. 
“Lakini kama mtu anauelewa mpana wa uchumi wa viwanda, sidhani kama atapinga,” alisema.
Alisema suala la viwanda sio la mwaka mmoja wa fedha, bali ni la miaka mingi, hivyo aliwaomba kuwa wavumilivu na kuwaamini wataalamu waliopo kwenye Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwani wana uelewa mkubwa.
“Ujenzi wa viwanda haujengwi kwa mwaka mmoja wa fedha, utatuchukua muda na tunachotakiwa ni kuwa wavumilivu,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Francis Michael alisema: “Kama kweli tuna nia ya kupata maendeleo na taifa hili litoke kwenye nchi maskini, ni lazima tuwe na viwanda.”
Alisema viwanda ni muhimu kwa Tanzania ndiyo maana nchi nyingine zinaendelea kwa kuwa na viwanda.
“Hakuna taifa linaloendelea bila ya kuwa na viwanda. Ni lazima kuwa na viwanda kwa sababu sisi ni wakulima na tunalima matunda, pamba, korosho na kila aina ya mazao, kwa nini tusiwe na viwanda na tukasindika wenyewe na kuwauzia wanaohitaji?” Alihoji.
Dk. Michael aliongeza: “Huyo anayeponda viwanda, anatakiwa kujifikiria mara mbili, hakuna nchi inayoendelea bila viwanda.”
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Dk. Timothy Lyanga, alisema ili taifa litoke kwenye umaskini, viwanda ni muhimu.
Dk. Lyanga alisema viwanda ni muhimu kwa Tanzania kwa sababu wakulima na Watanzania kwa ujumla watapata ajira kupitia sekta hiyo.
“Kinachotakiwa sasa ni serikali kutengeneza mazingira ambayo yatatusaidia kufikia katika Tanzania ya uchumi wa viwanda,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa Joseph Mbwiliza, alieleza kusikitishwa kwake na wanasiasa wanaotumia nafasi zao kuikatisha tamaa serikali, akiwafananisha na wahujumu uchumi.
Profesa huyo aliiambia Uhuru kuwa, dhamira ya serikali ya sasa ya kufufua viwanda inapaswa kuungwa mkono na makundi mbalimbali, hasa wanasiasa, ili itimie.
Alisema kwa mwanasiasa aliyepewa ridhaa na wananchi kuwawakilisha bungeni, hastahili kupinga mambo ya maendeleo dhahiri, kwa kigezo chochote hata kama cha upinzani.
Mbwiliza, ambaye pia aliwahi kuwa Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere cha Dar es Salaam, alisema Tanzania kuwa na uchumi wa viwanda sio mara ya kwanza.
"Tanzania tuliwahi kuwa na viwanda lukuki, tukajikwaa, sasa kitendo cha serikali ya awamu hii kutaka kurudia asili yetu ni jambo jema, kuikatisha tamaa mapema sio busara," alisema.
Pia, alisema inashangaza kwa mtu kusema akiwa anajiamini kuwa uchumi wa viwanda nchini hautafikiwa kwa sababu uhalisia ni kuwa hauna mwisho.
Alifafanua kuwa, Uingereza kama nchi ya kwanza kuendelea kwenye uchumi wa viwanda, haikufikia ilipo sasa kwa miaka mitano bali kwa miaka mingi.
"Kama wenzetu walitumia miaka mingi kuwa na uchumi thabiti wa viwanda, kwanini sisi ambao hata kiteknolojia bado tuko chini tuanze kukatishana tamaa wakati hata miaka mitano haijafika?
"Uchumi wa viwanda ni mchakato na ndio umeanza ili kurekebisha pale Tanzania ilipojikwaa kwenye sekta hiyo, hakuna mashiko kwenye ukosoaji wowote. Mtu unakatisha tamaa ili iweje, kwa manufaa ya nani?" Alihoji.

No comments:

Post a Comment