Friday, 30 June 2017

MAJALIWA: BIASHARA YA DAWA ZA KULEVYA KUWA HISTORIA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeadhimia kupambana vilivyo dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya na kuhakikisha inakuwa historia nchini.

Pia ametoa wito kwa wazazi wote nchini waendelee kufuatilia nyendo za watoto ili wasijiingize kwenye mtego wa dawa za kulevya na wala wasisubiri vijana wao waanze kutumia.

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Juni 29, 2017) kwenye maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani, iliyoadhimishwa mjini Dodoma.

Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu amesema Serikali imejidhatiti kuhakikisha kuwa uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya unadhibitiwa kikamilifu nchini.

Amesema katika kutimiza azma hiyo, ambayo pia inaelekezwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Serikali ilifanya mabadiliko ya Sheria ya Dawa za Kulevya kwa kuanzisha chombo cha kisheria cha kupambana na biashara hiyo, ambayo imeongeza adhabu kwa wanaoshiriki.

Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuimarisha chombo hicho kinachoongoza mapambano ya dawa za kulevya ili kiendelee kufanya kazi kwa weledi na kwa kutumia mbinu za kisayansi.

“Tunaponadi uchumi wa viwanda lazima tuwe na nguvu kazi yenye siha njema kuweza kushiriki kwenye kazi halali za kujenga Taifa letu na yeyote anayetaka kudhohofisha nguvu kazi ya Taifa letu au kuhujumu jitihada za uchumi wa viwanda atashughulikiwa bila huruma,” amesema.

Aidha, kauli mbiu ya maadhimisho hayo kitaifa ni ‘Tuwasikilize na Kuwashauri Vijana na Watoto ili Kuwaepusha na Dawa za kulevya.’

Waziri Mkuu amesema kauli mbiu hiyo imetokana nan a takwimu za waathirika wakubwa wa dawa za kulevya ambao ni vijana wenye umri kati ya miaka 15-35.

“Hili ndilo kundi kubwa kwenye jamii jetu na ndilo tegemeo kubwa kwa ustawi wa nchi yetu. Hili ndilo kundi litakalotoa askari wa kulinda Nchi yetu, wanasiasa wa kuongoza Taifa letu na wataalamu mbalimbali wa kuisaidia Tanzania,” amesema.

Awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu), Mheshimiwa Jenista Mhagama alisema matumizi ya dawa za kulevya yamelisababishia Taifa madhara makubwa ya kiafya na  kiuchumi hivyo kila mwananchi ashiriki katika mapambano hayo.

Mapema Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la Kituo cha Kutoa Huduma ya Tiba kwa Waathirika wa Dawa za Kulevya katika eneo la Itega mkoani Dodoma na kuwashauri wakazi wa mkoa huo kutojihusisha na biashara hiyo.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

    L. P. 980,

DODOMA.

ALHAMISI, JUNI 29, 2017

No comments:

Post a Comment