Monday 24 July 2017

RAIS MAGUFULI AMFAGILIA KAFULILA

ALIYEKUWA Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, amepongezwa na Rais Dk. John Magufuli kwa kujitoa mhanga kutetea Watanzania, baada ya kuibua kashfa ya fedha za Tegeta Escrow.

Rais Magufuli amesema kitendo kilichofanywa na Kafulila kuibua kashfa hiyo ni cha kizalendo na kamwe hawezi kusahaulika katika historia ya Tanzania.

Akizungumza na wananchi wa Nguruka, juzi, wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji, Rais Magufuli alisema atakuwa mnafiki iwapo atashindwa kumpongeza Kafulila kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuibua mambo mabovu yaliyofanywa na Kampuni ya IPTL.

Alisema Kafulila alitukanwa wakati alipoibua sakata la Escrow na anafahamu kwamba, mtu anapoibua kitu cha kizalendo, lazima asemwe vibaya na kusakamwa.

Rais Magufuli alisema anampongeza  Kafulila kwa kuwa mzalendo na kusisitiza kwamba, maendeleo hayana chama, ndio maana mbunge huyo wa zamani alijitoa kutetea fedha za wananchi.

"Ninajua Kafulila ulitukanwa sana wakati wa kuibua sakata la Escrow. Wapo watu walikuita tumbili, wewe sio tumbili. Najua wewe ni wa chama kingine, kwa hiyo nitakuwa mnafiki nisipokupongeza, kitu ulichokifanya ni kikubwa, naomba nikupongeze kwa hilo,"alisema Rais Magufuli.

Alisema kiongozi mzuri ni yule anayetetea wananchi bila kujali itikadi za kisiasa, hivyo atahakikisha wananchi hawateseki na wale, ambao wameiba fedha za serikali na za wananchi, atahakikisha wanazirudisha bila kujali nyadhifa walizonazo.

Rais Magufuli aliwaahidi wananchi wa Nguruka kuwa, atahakikisha anatatua kero ya maji na umeme na kwamba, atamtuma Waziri wa Nishati na Madini ili aweze kutatua tatizo hilo.

Alimaliza ziara yake mkoani Kigoma, juzi, kwa kuzindua mradi wa maji katika Kata ya Nguruka na kwenda Tabora, kuendelea na ziara yake.

No comments:

Post a Comment