Monday 24 July 2017

RAIS MAGUFULI AWATAKA WAPINZANI KUJIFUNZA KWA ZITTO KABWE


WABUNGE wa vyama vya upinzani nchini, wameshauriwa kujifunza kupitia kwa Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe kwa kushirikiana na serekali katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Rais Magufuli alitoa ushauri huo jana, wakati akiweka jiwe la msingi katika mradi mkubwa wa maji, uliojengwa katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, ambao umegharimu sh. bilioni 42.

Alisema Zitto ni tofauti na wanasiasa  wengine wa upinzani, ambao kazi yao ni kuipinga serikali, hata kama imefanya kitu kizuri na kwamba, amekuwa akiisaidia serekali kuwaletea wananchi maendeleo.

Pia, alisema Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo ni kiongozi mwenye akili nyingi, ndiyo maana alimteua kushika wadhifa huo ili kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

"Wakati namchagua Mkumbo na Mama Anna Mghwila, watu wengi walishangaa kwa nini nachagua mtu wa upinzani. Mkumbo ana akili nyingi na wanafanyakazi zao vizuri,"alisema Rais Magufuli.

Alisema maendeleo ya nchi hayana chama kwani yanamgusa kila mwananchi aliye na chama na asiye na chama, hivyo aliwataka watu wote kufanyakazi kwa kushirikiana.

Kwa upande wake, Zitto alisema yeye ni kiongozi anayewatumikia wananchi na yuko tayari kuendelea kuiunga mkono serikali kwa kila jambo zuri inalofanya kwa kuwa maendeleo hayana chama.

Alisema akiwa mbunge, ataendelea kuwashawishi wawekezaji kuja kuwekeza katika mkoa wa Kigoma, kwa kuwa serikali ya awamu ya tano imejipanga kuwekeza katika viwanda, hivyo ni lazima waiunge mkono.

"Kiongozi yeyote  mzalendo na mpenda maendeleo, hawezi kuacha kuiunga mkono serikali inayoongozwa na Rais wetu. Nawashangaa viongozi wanaomtukana Rais, hawana uzalendo. Sisi kama viongozi, lazima tuyaunge mkono maendeleo yanapotokea," alisema Zitto.

No comments:

Post a Comment