Monday, 3 July 2017
RAIS MAGUFULI AWAONYA WANASIASA WAROPOKAJI, AKIWEMO LOWASSA
RAIS Dk. John Magufuli amemtolea uvivu Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richomond, Edward Lowassa, kuhusu kauli yake kuhusiana na kuitaka serikali kuwatoa gerezani viongozi wa Jumuia na Taasisi ya Mihadhara ya Kiislamu(UAMSHO) na kumtaka aache kuropokaropoka.
Pia, amesikitishwa na vitendo vya wanasiasa kushindwa kutoa matamko juu ya mauaji yanayoendelea wilayani Kibiti, mkoani wa Pwani, badala yake wamekuwa mstari wa mbele kuchochea mifarakano, ambapo amedai atawashughulikia na kuitaka polisi isimuogope mtu yeyote katika kuchukua hatua.
Rais aliyasema hayo jana, kwenye hafla ya uzinduzi na uwekaji wa jiwe la msingi la kuboresha ufanisi na kuboresha uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam, ambapo alisema ni lazima watu hao wahojiwe na vyombo vya dola kwa ajili ya kutoa ushirikiano.
Alisema kuna wakati yanafanyika mambo hata mtu kushindwa kujua hao wanaoyazungumza wana mantiki gani, ikiwa vitendo vinavyofanywa sio sahihi na mustakabari wa ustawi wa taifa katika kulinda amani na utulivu ili kuisaidia nchi kupata maendeleo.
"Mimi ni rais wa miaka mitano, moja ya jukumu nililopewa na Watanzania ni kuilinda amani, kwa kuwa bila amani, maendeleo hayawezi kuja na hata wahisani wanaotupa fedha nyingi, hawawezi kutoa kwa kuwa muda mwingi tutakuwa tunashughulika na usalama,''alisema.
Aliongeza:" Kuna mwanasiasa mmoja anataka viongozi wa dini walioko gerezani watolewe. Ni jambo la ajabu sana. Mimi napenda kumpa salamu, anataka kuunganishwa nao ili aweze kutoa ushahidi? Naviomba vyombo vya dola visiogope kuhoji watu wa namna hiyo."
Alisema ni lazima Watazania wawe pamoja kwenye ulinzi wa amani, ambapo alihoji mbona nchini Marekani, wanapowashikilia watu kwa zaidi ya miaka 20, kwenye magereza yao, ikiwemo Guantanamo, hakuna wanasiasa wanaohoji,
iweje Tanzania ndiko wanasiasa wanakuwa mstari wa mbele.
"Napenda kuwaonya na kuwatahadharisha katika hilo. Juzi tumekamata gwanda za kijeshi zaidi ya elfu tano, hizi ni sawa na batalioni sita, huku pia watu wanakufa na askari, lakini ukitazama haya mambo kwa nini iwe kwa Chama kimoja pekee?' Alihoji huku akiwataka Watanzania kuwa wamoja na kuachana na wanasiasa wa aina hiyo.
Alisema polisi wawe makini na wasiogope mtu, iwe cheo chake au anatembeaje, kwa kuwa ameamua kuipeleka nchi mbele na hakuna wa kumkatisha tamaa kwa kuwa moja ya malengo yake ni kuhakikisha nchi inakuwa na usalama wa kutosha ili kila mtu aishi kwa amani na kufanya shughuli zake.
Hivi karibuni, Lowassa akiwa kwenye futari iliyoandaliwa na Mbunge wa Ukonga-CHADEMA, Mwita Waitara, aliitaka serikali kuwaachia masheikh hao, wanaoshikiliwa kwa mwaka wa nne kwa makosa ya ugaidi.
Kitendo hicho kilimfanya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai(DCI), Robert Boaz kumuita Waziri Mkuu huyo kwa ajili ya kumhoji kutokana na kauli hiyo ya kichochezi, ambapo mahojiano ya awali yameshafanyika na kumtaka arudi tena Makao Makuu ya Polisi, Julai 13, mwaka huu, kwa ajili ya kujua hatma yake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment