Tuesday 24 October 2017

ADVANSI MAKINIKIA KUNUNUA BOMBARDIER 10



MAFANIKIO ya awali katika majadiliano kati ya wataalamu wa serikali na wawakilishi wa Kampuni ya Barrick, inayomiliki Kampuni ya Acacia, yamebainisha kuwa, iwapo yatatazamwa kwa jicho la kimaendeleo zaidi, yanaweza kusaidia mapinduzi katika utoaji wa huduma nchini.

Katika makubaliano hayo, Barrick Gold, kampuni kubwa zaidi ya dhahabu duniani, wamekubali kutoa Dola za Marekani milioni 300, sawa na sh.bilioni 700, kama utangulizi wa kuonyesha kuguswa na sakata lililojitokeza huku majadiliano zaidi yakiendelea kuhusu matrilioni, ambayo kampuni hiyo inadaiwa na serikali.

Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa wa upinzani wameibuka wakipinga kiasi hicho cha fedha kuwa ni kidogo, wakisisitiza serikali ingeweza kufaidika zaidi katika majadiliano hayo. Lakini wachambuzi wa mambo ya chumi, wamepinga mtazamo huo kwa kusema kilichopatikana siyo cha kubeza.
                                          
Mmoja wa wanaoamini hivyo ni Wakili wa Mahakama Kuu na Mwanaharakati wa Masuala ya Madini nchini, Dk. Rugemeza Nshala, ambaye amekaririwa akisema, kiwango ambacho Tanzania imekipata, siyo cha kubezwa na kutaka hatua zaidi zichukuliwe siku zijazo.

“Ukweli ni kwamba, hatua hii siyo ya kubezwa. Kwamba tumeweza kujadiliana na wakubwa hawa na kupata tulichokipata, ni jambo jema. Nimefurahishwa zaidi na uamuzi wa migogoro kama hii kusikilizwa katika mahakama zetu,” alisema Dk. Nshala.

Mwanasheria Mwandamizi nchini, Profesa Palamagamba Kabudi, aliyeongoza majadiliano hayo, amenukuliwa akifafanua zaidi kuwa, makubaliano ya Tanzania kupata asilimia hamsini ya faida itakayopatikana katika migodo ya Barrick hapa nchini ni makubwa na ya kihistoria.

“Mfumo kama huu upo sehemu chache duniani, lakini kote wanahesabu mgawanyo huo kabla ya kodi. Sisi tutapata nusu kwa nusu baada ya kodi za serikali kuwa zimeshalipwa,”alisema.
                                           
Uchunguzi wa kina wa Uhuru, umebaini kuwa, kwa Dola za Marekani milioni 300, pekee ambazo serikali italipwa, kama Rais John Magufuli ataamua kumaliza kabisa matatizo katika Shirika la Ndege nchini, anaweza kununua ndege za Bombardier aina ya Q400 zipatazo 10.

Kwa mujibu wa tovuti ya Kampuni ya Bombardier iliyoko Canada, bei ya soko iliyoidhinishwa Januari, 2017, ndege moja mpya ya Bombardier Q400, inauzwa kwa Dola za Marekani milioni 32.2.

Bei hiyo ni kabla ya majadiliano kati ya mnunuzi na kampuni hiyo, hivyo Serikali ya Rais Magufuli, inaweza kuamua kufanya majadiliano na kununua Bombardier nyingine zaidi ya 10 kwa fedha hizo.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, iwapo Rais Magufuli ataamua kutumia fedha hizo kununua ndege kubwa zaidi ya CS 300, ambayo nayo inatengenezwa na Kampuni ya Bombardier, serikali inaweza kupata mpaka ndege nne za aina hiyo.

Bombardier CS 300, ina uwezo wa kuchukua abiria mpaka 150, ikiwa na uwezo wa kupunguza matumizi ya mafuta kwa asilimia mpaka 20, ikilinganishwa na ndege za ukubwa huo za mashiriki mengine na ndiyo inayotumia teknolojia za kisasa zaidi, ikiwemo kupunguza mngurumo.

No comments:

Post a Comment