KATIBU wa NEC, Itikadi wa Uenezi wa CCM, Humphery
Polepole, amesema kwamba, utamaduni wa vyama vya upinzani kudai viongozi
wanaotoka upinzani kwenda CCM wamenunuliwa ni siasa chafu.
Amesema, desturi hiyo haifai, hasa ikizingatiwa mtu
anayetoka CCM kwenda upinzani, wanasiasa wa upinzani huona ni sawa kwa watu hao
kuchukua uamuzi huo.
Polepole alisema, kitendo cha wanasiasa wa upinzani
kuhamia Chama tawala kwa zama hizi ni dalili za kuridhishwa na mwenendo wa CCM
mpya, inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli.
"Niseme jambo moja, hawa wamekuja kwa hiari
yao wenyewe. Kuhama kwao kuna maana kuwa walikotoka hakuna hoja, hakuna sera,
itikadi na falsafa inayoongoza vyama hivyo kwa hiyo kutoa maneno kuwa
wamenunuliwa ni kama mfa maji, haishi kutapatapa," alisema.
Katibu huyo wa NEC ya CCM, alitoa kauli hiyo hivi
karibuni, alipozungumza kwenye kituo cha runinga cha TBC1, siku moja kabla
baadhi ya wabunge wa upinzani kusema wana uthibitisho wa video kuhusu madai ya
madiwani wa CHADEMA, kununuliwa ili kujiunga na CCM.
Madai hayo yaliyoanza mara baada ya Rais na
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk. John Magufulin kuzuru mkoani Arusha na kuwapokea
madiwani 10, waliojiuzulu CHADEMA na kujiunga na CCM, yaliibuliwa na Mbunge
Joshua Nassari na Godbless Lema.
Katika ombi lake kwa Rais Magufuli wiki kadhaa
zilizopita, Nassari, ambaye ni Mbunge wa Arumeru Mashariki, alisema endapo Rais
Magufuli atampa ruhusa, atampelekea 'flash' yenye uthibitisho wa video za
'kununuliwa' kwa madiwai hao.
Siku chache baadaye, mbunge huyo aliibuka akidai
atakutana na wanahabari, akiwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Lema ili kuwasilisha
video hizo kwa umma, jambo walilolifanya mwishoni mwa wiki iliyopita.
Hata hivyo, video hiyo imeibua sintofahau lukuki
miongoni mwa wataalamu wa uchambuzi wa video na wananchi kwa kuwa haina
uhalisia wa walichokuwa wakikizungumza kwa kujiamini dhidi ya madai yao.
Katika uwasilishaji huo, Lema na Nassari
walionyesha video fupi, ikiwaonyesha Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander
Mnyeti na Mkurugenzi wa wilaya hiyo, bila kuwaonyesha madiwani waliodaiwa
kupokea rushwa kama ushawishi wa kuhamia CCM.
Matukio hayo yote yanaonekana kuwekewa shaka,
yakitanguliwa na kauli ya Polepole kuhusu aina hiyo ya siasa, huku pia wadau
mbalimbali wakihoji kilichowazuia wanasiasa hao wa upinzani kutokuwasilisha
hoja zao Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kabla ya
kuzungumza na wanahabari.
"Naona wanatuchanganya. Kwa nini wasiamue
kupeleka kwanza TAKUKURU na kuamua kuanza na vyombo vya habari. Na kama kweli
madiwani hao wamenunuliwa, bado ni shida kwa upande wao kwamba, kwanini
wakubali kununulika?" Alihoji Seleman Daffa, Kada wa CCM mkoa wa Tanga.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti,
aliyetajwa na Nassari kwamba, amehusika zaidi kwenye madai hayo, jana asubuhi
ilidaiwa angezungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha, lakini alikanusha
taarifa hiyo alasiri.
Hadi kufikia sasa, kanda ya kaskazini inaongoza kwa
viongozi wa vyama vya upinzani, hususan CHADEMA, kujivua uanachama na kujiuzulu
nafasi zao za kisiasa ili kujiunga na CCM, ambako wanasema kunafaa kwa maslahi
ya taifa, ikifuatiwa na nyanda za juu kusini na kanda ya ziwa.
No comments:
Post a Comment