Tuesday 13 December 2016

MPOGOLO, POLEPOLE, LUBINGA SURA MPYA NDANI YA SEKRETARIETI



HALMASHAURI Kuu ya Taifa ya CCM, imeridhia kwa kauli moja kufanya mabadiliko ya muundo na uongozi wa Chama ili kuongeza ufanisi utakaowezesha viongozi kuwatumikia wananchi na wanachama kwa karibu zaidi.

Katika kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli, pia kilipokea tathmini ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana, ambapo baada ya kupokea na kutafakari taarifa hiyo ndipo maamuzi hayo makubwa yalipochukuliwa.

Maamuzi na mapendekezo hayo yatasababisha kufanyika mabadiliko ya Katiba ya Chama na Kanuni za Jumuiya zake.

Aidha, Dk. Magufuli amemteua Rodrick Mpogolo kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), nafasi iliyokuwa ikishikiriwa na Rajabu Luhwavi, ambaye ametuliwa kuwa Balozi huku Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Humphrey Polepole akiteuliwa kuwa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi.

Polepole anashika wadhifa huo baada ya Nape Nnauye, ambaye alikuwa akishikiliwa wadhifa huo, kuteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Aidha, Dk. Magufuli amemteua Kanali Ngemela Lubinga, kuwa Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, nafasi ilikuwa ikishikiliwa na Dk. Asha Rose Migiro, ambaye ameteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza.

Awali, Kanal Lubinga, alikuwa Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Katika uteuzi huo wajumbe wengine wa Sekretarieti watandelea kubaki na nyadhifa zao.

Wajumbe hao ni Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahmni Kinana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Idara ya Oganizesheni, Mohammed Seif Khatibu na Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha, Zakia Meghji.

MAAMUZI

Kupunguza idadi ya wajumbe wa vikao na idadi ya vikao vya Chama katika ngazi mbalimbali ili kuongeza ufanisi wa utendaji wa Chama na kuongeza muda wa viongozi wa Chama kufanya kazi za Chama kwa Umma badala ya kutumia muda mwingi vikaoni.

Ili kuwa na vikao vya Chama vyenye tija imeamuliwa, Halmashauri Kuu ya Taifa kwa sasa ina jumla ya wajumbe 388 idadi ambayo ni kubwa  hivyo imeamuliwa idadi hii ipunguzwe na kuwa wajumbe 158.

Wajumbe hao watakuwa ni Wenyeviti wa Mikoa 26 ya Tanzania Bara, mikoa sita ya mikoa ya Zanzibar, Wajumbe wa NEC wa mikoa 26 ya Tanzania Bara, mikoa ya Zanzibar sita ya Zanzibar ambayo kila mmoja utatoa wajumbe wanne.

Wajumbe 15 wa NEC wa Taifa kutoka Tanzania Bara na 15 kutoka Zanzibar pamoja na nafasi saba za uteuzi atakazobakiwa nazo mwenyekiti wa Chama.

Katika maamuzi hayo pia yamehusisha Wajumbe wa NEC wa Jumuiya za UVCCM, UWT na Wazazi ambazo zitatoa wajumbe watano kwa kila jumuiya, Wajumbe wa watano wa NEC kutoka Bungeni  na nafasi moja ya Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM.

Wengine ni Wajumbe watatu wa  NEC kutoka Baraza la Wawakirishi, nafasi moja ya Katibu wa Kamati ya Wawakilishi huku wengine ni Wajumbe wa NEC wanaotokana na Nyadhifa zao ambao ni Mwenyekiti wa CCM, Makamu Mwenyekiti (Bara), Makamu Mwenyekiti (Zanzibar) na Makamu wa Rais.

Kwenye taarifa hiyo iliyotolewa jana na Nape ambaye aalikuwa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, ilizitaja nafasi zingine kuwa Waziri Mkuu, Makamu wa Pili wa Rais (Zanzibar), Spika wa Bunge, Spika  wa  Baraza la Wawakirishi, Mwenyekiti wa UWT, Mwenyekiti wa WAZAZI, Mwenyekiti wa UVCCM, Katibu Mkuu  WAZAZI, Katibu Mkuu  UWT  na Katibu Mkuu UVCCM ambapo jumla ni wajumbe 158.

VIKAO

Imeamriwa kuwa vikao vya kawaida vya Halmashauri Kuu ya Taifa vifanyike kila baada ya miezi sita badala ya miezi minne kama ilivyo sasa isipokuwa vinaweza kufanyika vikao maalum inapohitajika.

Pia, imeamuliwa wajumbe wa Kamati Kuu wawe 24 badala ya 34 kwa kuhusisha Mwenyekiti wa CCM, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Makamu Mwenyekiti wa CCM  (Zanzibar), Makamu wa  Rais, Katibu Mkuu wa CCM,  Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara) na Naibu Katibu Mkuu wa CCM  (Zanzibar).

Wengine ni Waziri Mkuu, Makamu wa Pili wa Rais (Zanzibar), Spika wa Bunge, Spika  wa Baraza la Wawakirishi, Mwenyekiti  wa WAZAZI, Mwenyekiti  wa UWT, Mwenyekiti  wa UVCCM, Katibu wa   wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa  Organaizesheni na Katibu wa  Halmashauri Kuu ya Taifa wa  Itikadi na Uenezi.

Nafasi nyingine ni Katibu wa   wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa  Uchumi na Fedha, Katibu wa   wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa  Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Wajumbe  watatu wa kuchaguliwa  na Halmashauri Kuu kutoka Bara na Wajumbe watatu wa kuchaguliwa  na Halmashauri Kuu kutoka Zanzibar.

Aidha, vikao vya kawaida vya Kamati Kuu vipunguzwe ili vifanyike kila baada  ya miezi minne badala ya miezi miwili isipokuwa vinaweza kufanyika vikao maalum inapohitajika.

Kwa ngazi ya mkoa, Wajumbe wa Kamati za Siasa za Mikoa wamepunguzwa kwa kuondoa wajumbe  watatu ambao Katibu wa Uchumi na Fedha wa Mkoa, Wajumbe wa kuchaguliwa na Halmashauri au Mkoa.

Pia imeamriwa Vikao  vya kawaida vya Kamati ya Siasa ya Mkoa vifanyike kila baada ya miezi mitatu badala ya kila  mwezi kama ilivyo sasa isipokuwa vinaweza kufanyika vikao maalum inapohitajika.

Kwenye wilaya Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya wamepunguzwa kwa kuwoandoa, Katibu wa Uchumi na Fedha wa Wilaya, Katibu wa Kamati ya Madiwani, Wajumbe wa kuchaguliwa na Halmashauri Kuu ya Wilaya ambao jumla ni wanne.

Vikao vya kawaida  vya Kamati ya Siasa ya Wilaya  vitafanyika kila baada ya miezi mitatu badala ya kila  mwezi isipokuwa vinaweza kufanyika vikao maalum inapohitajika.

Maamuzi hayo pia yaligusa muundo wa Wilaya za Chama kutakiwa kuendana na muundo wa sasa wa Serikali.

Vile vile kwenye Kata,Tawi na Shina, imeamriwa kuwa dadi ya kuanzisha Shina iwe wanachama 50  hadi 300.

Idadi ya kuanzisha Tawi iwe wanachama kuanzia 301 hadi 1,000, hata hivyo idadi hiyo izingatie eneo la kijiografia na wingi wa wanachama katika eneo hilo.

Vikao vya kawaida vya  Kamati za Siasa  za  ngazi hizo viwe vinafanyika mara moja kila baada ya miezi mitatu, isipokuwa vinaweza kufanyika vikao maalum inapohitajika.

NAFASI ZA UONGOZI

Kikao hicho kimeamua, mwanachama kutakiwa kuwa na nafasi moja pekee ya uongozi wa kazi za muda wote kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni za uchaguzi wa Chama Toleo la 2012 kifungu cha 22 na 23 ambazo zimetajwa kuwa ni Mwenyekiti wa Tawi,Kijiji au Mitaa.

Wengine ni Mwenyekiti wa Kata/Wadi, Mwenyekiti wa Jimbo, Wilaya na Mkoa, Makatibu wa Halmashauri Kuu wa ngazi zote zinazohusika, Mbunge, Mwakilishi na Diwani.

Viongozi wa kuchaguliwa wametakiwa kuepuka kuwa watendaji badala yake waongoze na kusimamia shughuli za Chama kwa kuzingatia Katiba na Kanuni.

KUHUSU VYEO

Imeamriwa kuwa vyeo ambavyo havijatamkwa kwenye Katiba ya CCM haviruhusiwi katika Chama au Jumuiya zake ambavyo ni Umoja wa makundi mbalimbali kama Wenyeviti wa ngazi mbalimbali (Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM), Makamanda (UVCCM), Washauri (UWT) na Walezi (WAZAZI) katika ngazi zote.

UHAKIKI WA WANACHAMA

Halmashauri Kuu pia imeona ipo haja ya kufanya uhakiki wa wanachama wa CCM  na Jumuiya zake ili kujua idadi sahihi ya wanachama kwa wakati huu.  

Uhakiki huo utaendana na kutoa kadi mpya za uanachama za kielektroniki ili kuwa na udhibiti wa usahihi wa wanachama na kuondoa wanachama hewa. Aidha, Kadi za UWT, WAZAZI na UVCCM zitafutwa ili kubaki na kadi za CCM pekee.

JUMUIYA ZA CHAMA

Jumuiya za CCM zimetakiwa kufanya kazi zake kwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya CCM na Kanuni za Jumuiya husika, kanuni za Jumuiya ziendane na  matakwa ya Katiba ya CCM.

Uaendeshaji  wa shughuli zote za Jumuiya za Chama na mali zake umetakiwa kuwa chini ya usimamizi wa Chama (Baraza la Wadhamini la Chama Cha Mapinduzi).

Makatibu Wakuu wa Jumuiya watakuwa wanateuliwa na Kamati Kuu na Manaibu Katibu Wakuu watateuliwa na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa.

Pia wakati Chama kikiendelea kubaki  na bendera yenye rangi ya kijani na njano  na  alama ya jembe na nyundo, Halmashauri Kuu imeona ipo haja ya kuzifanya rangi hizo kuwa na muenekano wa kuvutia zaidi.

Utumishi katika Chama na Jumuiya zake. Katibu Mkuu wa CCM na Sekretarieti wametakiwa kupewa majukumu ya kusimamia ajira za Watumishi wa Chama na Jumuiya zake.

Nafasi za Makatibu Wasaidizi wa Mikoa na Wilaya zitaondolewa na badala yake kazi zao zitatekelezwa na Makatibu wa Jumuiya  za Chama wa Mikoa na Wilaya kwa utaratibu utakaopangwa. 

Utaratibu huu utakipunguzia Chama Cha Mapinduzi gharama na kujenga umoja wa utendaji kazi wa Chama na Jumuiya zake katika Mikoa na Wilaya.

HALI YA KISIASA ZANZIBAR.

Halmashauri Kuu ya Taifa imeagiza kuundwa kwa Kamati Maalumu ya kufanya tathimini ya kina kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar kwa masuala yanayohusu uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka jana.

Pia, Mwenyekiti wa Kamati ya udhibiti na nidhamu ametakiwa akamilishe kazi ya taarifa ya udhibiti kwa wanachama waliokiuka mienendo ya kiuanachama kabla ya kuanza uchaguzi Mkuu wa Chama Februari mwakani.

Mikoa na Wilaya ambazo hazijaleta taarifa za kiudhibiti zimeagizwa ziwe zimefikisha taarifa zao kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Udhibiti na Nidhamu kabla ya Februali mwakani.

Kikao hicho kimeamua uhakiki wa mali za Chama uendelee kufanyika kwa kina na uchambuzi zaidi ukikamilika, taarifa yake iwasilishwe kwa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa mapema iwezekanavyo.

Hivyo mambo ambayo yatahitaji mabadiliko ya Katiba, Mkutano Mkuu utaandaliwa mwakani na kutafakari kisha kupitisha mabadiliko hayo ya Katiba.

No comments:

Post a Comment