Tuesday 13 December 2016

CCM YASUKWA UPYA


RAIS na Mwenyekiti wa CCM, Dk. John Magufuli, ameweka hadharani taswira ya CCM anayoitaka katika kipindi chake cha uongozi wa Chama.

Taswira hiyo imejengwa na mambo manane (8), ambayo aliyaeleza kupitia hotuba yake aliyoitoa kwa dakika takriban 35, mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), katika ukumbi wa Ikulu, jijini Dar es Salaam, jana.

Alisema kipaumbele chake cha kwanza ni kuimarisha Chama katika ngazi zote na jumuia zake ili kiwe na nguvu zaidi na kwamba, hataki kuona Chama kinakuwa legelege.

Pia, alisema dhamira ya pili ni kuongeza idadi ya wanachama ndani ya CCM, ambapo alishauri nguvu kubwa ielekezwe kwenye kuongeza idadi ya vijana, ambao ndio nguvu kazi ya taifa.

Alisema katika kazi ya kuongeza idadi ya wanachama, ni vyema suala la wanachama hewa likaepukwa kwa sababu mtindo huo umekuwa utamaduni wa muda mrefu, hasa wakati wa chaguzi mbalimbali.

Pamoja na hilo, Rais Dk. Magufuli alisema jukumu kubwa, ambalo linapaswa kuwekewa mkazo ni suala la kukomesha rushwa ndani ya CCM.

Alisema CCM ni miongoni mwa taasisi zinazotajwa kujihusisha na rushwa kwenye utendaji, hususan katika vipindi vya uchaguzi, jambo ambalo siyo zuri.

"Chama chetu kinatuhumiwa kuendekeza rushwa na inajidhihirisha wakati wa chaguzi zetu ndani ya Chama. Huu ni ugonjwa sugu, unahitaji kutafutiwa ufumbuzi.

"Tukielekea kwenye uchaguzi mkuu wa Chama mwakani, hatutakuwa na msamaha kwa mtu atakayejihusisha na kutoa au kupokea rushwa kwa sababu tunataka viongozi waadilifu," alisisitiza.

Aidha, alisema kwa kuwa CCM inavyo vitega uchumi na rasilimali nyingi, hivyo ni wazi kuwa inapaswa kuvitumia kwa manufaa ili kuepuka utegemezi wa ruzuku kutoka serikalini.

Mwenyekiti huyo alisema rasilimali za CCM hazikisaidii Chama kutokana na ubadhirifu wa baadhi ya viongozi na kuingia mikataba mibovu, isiyo na tija ya uwekezaji.

Dk. Magufuli pia alitaja udhibiti wa wasaliti wa Chama katika uchaguzi uliopita kama moja ya dhamira zake huku akitumia fursa hiyo kuzipongeza kamati za siasa za wilaya na mikoa za CCM nchi nzima kwa kuwashughulikia wasaliti.

Alisema CCM yake anataka iwe imara kwa wanachama wa chini na si kwa wanachama wachache wa ngazi za juu, ambapo alibainisha kuwa atafurahi kuwa na wajumbe wachache wa vikao vya juu tofauti na ilivyo sasa.

"Jambo jingine, ninataka Chama kizingatie kanuni zilizoko kikatiba, ikiwemo ile ya mwaka 2012 kifungu cha 22 na 23 kinachokataza mwanachama kuwa na nafasi zaidi za moja.

"Hakuna umuhimu wa mtu mmoja kushika nafasi mbili, katiba yetu inakataza, hivyo tufuate kanuni katika kuenenda kwetu,"alisisitiza.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwataka wanachama na viongozi ndani ya CCM, kusimamia katiba iliyopo kwamba, hakuna umuhimu wa kuwa na vyeo ambavyo kikatiba havipo.

Rais alizitaja baadhi ya nafasi hizo kuwa ni Ukamanda wa jumuia mbalimbali, ulezi na ushauri, ambavyo kiuhalisia havina mantiki kiutendaji.

Pia, alisema Chama kinapaswa kufuatwa na wanachama na si mwanachama kufuatwa na Chama kama ilivyowahi kuonekana hapo awali.

"Chama ni mali ya wanachama, siyo mali ya mtu, hivyo chama kisimfuate mtu bali mtu akifuate Chama," alisema.

Alisema malengo hayo licha ya kuwa na nia ya kuyatekeleza, peke yake hataweza, hivyo aliwaomba wajumbe wa NEC na wanachama kwa ujumla kumuunga mkono katika utekelezaji huo.

Sambamba na hilo, aligusia uchaguzi wa Chama, ambao mchakato wake utaanza Februari hadi Novemba, mwakani, ambapo alitoa wito kwa wanachama kujiandaa.

Alisema uchaguzi huo unapaswa kupewa uzito wa aina yake, kwa sababu safu ya uongozi itakayowekwa madarakani ndiyo itakuwa na majukumu ya kukipa ushindi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu mwaka 2020.

Aliitaka sektretarieti na mamlaka zingine, kuwaandaa wanachama ili wachague viongozi waadilifu, wachapakazi, wenye kukubalika kwenye jamii na wanaokataa rushwa.

"Mchague watu ambao ni waadilifu ndani ya Chama, wala rushwa hatuwataki, wametutesa sana, umefika muda wa kusema sasa basi," alisema.

Alionya juu ya uwepo wa mapandikizi kwenye uchaguzi huo, utaratibu ambao umetekelezwa na baadhi ya watu, ambapo alisema endapo Chama kitabaini mapandikizi katika uchaguzi huo, hakitasita kufuta uchaguzi wote.

Rais alisema CCM imeanza kujiandaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, kwa kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015-2020, kwenye sekta mbalimbali.

Alisema baadhi ya mafanikio yaliyofanywa na serikali katika utekelezaji wa Ilani ya CCM katika kipindi cha mwaka mmoja tangu aingie madarakani, asilimia 40 ya trilioni 29.5 za bajeti, ilitengwa kwenye miradi ya maendeleo ili kujenga misingi ya uchumi makini wa viwanda.

Rais Magufuli alisema miradi hiyo ni kwenye sekta zote, ikiwemo miundombinu ya umeme kama Kinyerezi 1 mpaka 3, miundombinu ya reli ya kisasa, ambayo mradi utaanza na ujenzi wa kilomita 200.

Kwenye usafiri wa anga, alisema tayari serikali imenunua ndege sita zikiwemo tatu aina ya Bombadier Q-400, zinazobeba abiria 76 na mbili modeli ya CS-300, zitakazoanza kutumika kwa mara ya kwanza Afrika zinazobeba abiria 137 mpaka 150.

Pia, alisema ndege hizo mbili zilikuwa zikitumiwa kwenye kampuni ya Swiss Air na kwamba, zitaingia nchini Mei na Juni, 2018, huku ile ya mwisho kubwa Boeing 787 8th-Generation yenye uwezo wa kubeba abiria 262, nayo ikitarajiwa kuingia Juni 2018.

Alisema lengo ni kujenga uchumi kwa utalii wa nchi, ambayo ina utajiri mkubwa wa maliasili kwenye maeneo mbalimbali.

"Tanzania ina watu zaidi ya milioni 50, Morocco ina watu milioni tano, lakini takwimu za watalii kwa mwaka Tanzania inapokea watalii milioni mbili huku Morocco ikipokea watalii milioni 20.

"Kwanini itakuwa hivi? Siri kubwa ni umiliki wa shirika lao la ndege, ndege zina mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya utalii na sisi tumeamua kufufua la kwetu," alisema.      

Kwenye sekta ya afya, alisema bajeti ya afya imeongezeka kutoka sh. bilioni 31 mpaka sh. bilioni 250, huku sekta ya elimu ikitoa elimu bila malipo kwa kutenga bilioni 18.777, kila mwezi ili kugharamia elimu kuanzia msingi mpaka sekondari.

Aidha, kwenye elimu ya juu, alisema serikali imeongeza fedha kwa kutenga sh. bilioni 483, zilizoongeza udahili wa wanafunzi kutoka 98,000, waliokuwa wakihudumiwa na bajeti ya sh. bilioni 340, kwa mwaka jana, mpaka wanafunzi 125,000.

"Ongezeko hili la bajeti kwenye sekta ya elimu limesababisha kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya msingi kwa asilimia 84, huku sekondari wakiongezeka kwa asilimia 26. Makusanyo kwa wastani yamepanda pia kutoka sh. bilioni 850 mpaka sh. trilioni 1.2," alisema.  

Rais pia alisema licha ya jitihada hizo za serikali za kuileta Tanzania mpya, bado kumekuwa na changamoto nyingi zikiwemo za watumishi hewa, wanafunzi hewa na wanufaika hewa wa fedha za TASAF

"Nimewaambia kuhusu mafanikio, nisipowaeleza kuhusu changamoto mtanishangaa najua, kwa hiyo tuna changamoto kadhaa, ambazo serikali kwa umoja wake tunazishughulikia ipasavyo.

"Wakati tunapunguza PAYE kwa watumishi kutoka asilimia 11 mpaka 9, matatizo ya watumishi hewa yakajitokeza, baada ya kuhakiki tumebaini watumishi hewa 19,000," alisema.

Aidha, alisema serikali ilipoamua kutekeleza azimio lake la elimu bila malipo, walibainika wanafunzi hewa 65,000, kote nchini huku kaya hewa za TASAF 55,000, zikibainika baada ya serikali kuongeza fungu kwenye mfuko huo.

Dk. Magufuli alisema hali ni shwari na kwamba, wanakwenda vizuri kwenye utekelezaji wa Ilani kutokana na jinsi mambo yalivyo nchini.

"Mipaka yetu iko salama, muungano uko imara na tunamuona Rais Shein yuko hapa salama salimini, tumedumisha mahusiano ya kimataifa kwa kupokea wageni lukuki na mimi nikaenda Kenya, Uganda na Rwanda," alisema.

Alibainisha kuwa suala la kutokwenda nje ya nchi ni uamuzi alioufanya kwa sababu amepata mialiko zaidi ya 50, lakini akaona vema asafishe nyumbani kwake kabla ya kwenda kwa wenzake.

Sambamba na hilo alisema kuna mambo mengi ambayo serikali inayafanya kwa haraka na kwa wakati mmoja, hivyo ushirikiano wa wajumbe wa NEC na wanachama kwa ujumla ni muhimu ili kutimiza ahadi kabla ya mwaka 2020.

AWASHANGAA WANAOHOJI NEC KUKUTANA IKULU

Awali, akianza hotuba yake, aliwakaribisha wajumbe wa NEC kuwa Ikulu ni kwao hivyo wasione unyonge kukutana kwenye kikao chao cha Halmashauri Kuu ya CCM.

"Ikulu ni kwenu, bila ninyi mimi nisingekuwa hapa, hivyo sioni aibu kuwaalika wana CCM wenzangu hapa kwa sababu ni kwa mwana CCM mwenzao," alisema.

Alisema Ikulu ni ya Watanzania wote, wakiwemo wageni ndio sababu viongozi wa mataifa mbalimbali hupokelewa, wasanii wa hapa nchini na baadhi ya dhifa ikiwemo ya Iddi hufanyika pale.

"Ninawashangaa wanaohoji kwanini niwaalike CCM hapa, hata vyama vingine kama vinataka kuja kufanya mikutano yao hapa, ninawakaribisha ila hapa kuna taratibu zake, ikiwemo lazima tujue ajenda zao na tusikilize kikao chao wanasema nini," alisema huku akicheka.

Dk. Magufuli alisema NEC kukutana Ikulu haitakuwa mara ya mwisho na kwamba, muda wowote atakaohitaji kukutana nao atawaita.

"Hii haitakuwa mara ya mwisho, nitakapoamua nitawaita na hakuna atakaye niagiza nifanyie wapi mkutano," alisema.

ATOA SHUKRANI KWA JK, KINANA, NEC

Katika hatua nyingine, alitumia fursa ya hotuba hiyo kumshukuru Katibu Mkuu, Komredi Abdulrahman Kinana, kwa utendaji wake kwa Chama na kumwita nguzo na hazima ya CCM.

Alimtaja Mwenyekiti mstaafu, Jakaya Kikwete kuwa ni mwalimu wake kwenye mambo mbalimbali na kwamba, Mama Salma Kikwete amfikishie salamu na shukrani zake arudipo nyumbani.

Pia, aliwashukuru wajumbe wa NEC kwa kumpigia kampeni mjini Dodoma, Julai, mwaka huu na kumwezesha kushinda kura zote za wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama, jambo lililomfanya kupitishwa kuwa Mwenyekiti wa CCM.

KINANA ALONGA

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, akifungua kikao hicho, alisema ni kikao muhimu cha kutathmini historia ya CCM katika sura nne, ikiwemo miaka 40 tangu kuzaliwa kwake, miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar, miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara na miaka 25 ya vyama vingi, ambayo muda wote CCM imeshinda dola.

Alisema kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe 355, sawa na asilimia 96.7 ya wajumbe wote, ambao jumla ni 374, huku maazimio yaliyofikiwa yakiwa ni kwa maslahi ya Chama ili kuongeza uimara, ukaribu kwa wananchi, usikivu na kuwasemea wananchi.

"Tunataka CCM iendelee kushika dola kwa miongo mingi zaidi ijayo kutokana na maamuzi tutakayoyafanya leo (jana)," alisema.

Pamoja na hayo, alisema Rais Dk. John Magufuli amewatendea haki wana CCM kwa kuwateuwa kwa wingi kwenye nafasi mbalimbali za uongozi serikalini.

Alisema wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali ni makada wa CCM, jambo linalotoa fursa ya maendeleo kwa kuwa wote wanaijua vizuri Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

"Walioteuliwa wajue kuwa sasa wao ni watumishi wa serikali, wanapaswa kutii sheria, kanuni na taratibu za utumishi bila kusahau kufuata katiba ya nchi, lakini wasimamie kidete Ilani ya Uchaguzi ya CCM," alisema.

Aliongeza: "Mwenyekiti, kuna mtu asubuhi aliniambia wako watu wawili tu wanaoitwa 'His Excellency' yaani Rais na Balozi, sasa umewateuwa miongoni mwetu mabalozi, lakini kuna mtu kaniuliza kwanini mi si miongoni mwa wateule? Nikamjibu mkuu kaniweka kiporo, si ajabu kaniwekea sehemu nzuri zaidi ya hizo."

Kauli hiyo ya Katibu Mkuu iliwafanya wajumbe wote kucheka kwa furaha na baada ya muda alitoa nafasi kwa wajumbe watano wa NEC walioteuliwa na Rais kwenye nafasi mbalimbali hivi karibuni wazungumze kwa ufupi.

RAJABU LUHWAVI (Balozi Mteule)

"Ninamshukuru Rais Magufuli, amekipa heshima Chama hivyo nitaitumikia nafasi hii kwa nguvu na akili zangu zote ili kutokukiangusha." 

PINDI CHANA (Balozi Mteule)

"CCM ndio kila kitu kwangu tangu namaliza masomo yangu, kimenilea na kunikuza, kwa ufupi naahidi kufanya kazi kwa bidii, kidumu Chama Cha Mapinduzi."  

EMMANUEL NCHIMBI (Balozi Mteule)

"Ninashukuru kwa nafasi hii, nimekuwa Mjumbe wa NEC kwa miaka 19, Kamati Kuu kwa miaka 14. Nina matumaini makubwa na uongozi wa Rais Magufuli, amefanya makubwa akiwa waziri katika wizara mbalimbali."

"Ametusaidia umoja wa vijana kuokoa hati ya kiwanja chetu, ambayo tulitapeliwa, akiwa pale ardhi nikamfuata akatusaidia tukaipata. Wakati tunajenga lile jengo la Umoja wa Vijana, tukaambiwa mwisho ghorofa nane, lakini nikamfuata pia akabatilisha agizo hilo ndani ya saa 24, bila yeye kusingekuwa na jengo la UVCCM pale, hivyo nikasema hapa ni waziri akiwa Rais si atafanya mambo makubwa? Nashukuru sana, ninakwenda kufanya kazi."

YUSUPH MZEE (Balozi Mteule)

"Nawashukuru sana Rais Magufuli na Rais Shein kwa kutambua uwezo wangu, nimeshika nafasi mbalimbali ndani ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikiwemo Uwaziri wa Fedha na Jamhuri ya Muungano nilikoshika Unaibu Waziri wa Fedha.

"Kote huku nimefika kutokana na kuonekana na viongozi hawa, kuteuliwa huku ni heshima kwangu, kwa familia na kwa nchi yangu hivyo naahidi licha ya kwamba sijajua utanipeleka nchi gani, kokote nikakakokwenda nitakwenda na Ilani ya CCM kuitangaza Tanzania na Chama."

OLE SENDEKA (Mkuu wa Mkoa Njombe)

"Mwaka huu ni mwaka wa bahati kwangu, nikiwa Simanjiro nilipigiwa simu nije Dar, Ikulu kwani viongozi wangu wa Chama wamekaa na kuamua nikisemee Chama changu baada ya mdogo wangu Nape Nnauye kuteuliwa kuwa waziri.

"Nilifanya kazi yangu hadi juzi, nilipoonekana tena na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, naahidi ninakwenda Njombe kuonyesha kuwa uelewa wangu wa chama na Ilani zake ndivyo ulivyo kwenye utendaji.

"Kwa sababu nimelelewa na Chama tangu chipukizi nilipokelewa na Lukuvi na Kaka Mohammed Khatibu, wakaniajiri pale UVCCM mpaka sasa nimekuwa ndani ya CCM, nimeshika wadhifa serikalini miaka mitatu tu.

"Ninashukuru, ninawaahidi wana CCM ninakwenda kuwakilisha vizuri Chama na nashukuru kwa sababu kwa nafasi hii nitapata fursa ya kuvaa shati langu la kijani kwenye kamati za siasa za mkoa tofauti na hawa wenzangu waliochaguliwa kuwa mabalozi, ambao wao watakuwa wakivaa suti tu muda wote. Ahsante sana Rais wangu, sitakuangusha."

HALI ILIVYOKUWA

Kikao kilianza saa 04.10 asubuhi, ambapo wajumbe wote 355, waliingia ukumbini kumsubiri Mwenyekiti Dk. John Magufuli, ambaye alitanguliwa na Makamu Mwenyekiti Bara, Philip Mangula na Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Rais Dk. Ali Mohammed Shein.

Kulikuwa na hali ya utulivu kana kwamba kila mmoja ana maswali mengi kichwani kutokana na kuulizwa fumbo lisilokuwa na jibu.

Kikao kilianza mara tu baada ya kuingia Rais Magufuli, ambaye alipokelewa kwa nyimbo mbalimbali za hamasa za Chama kutoka kwa wajumbe hao.

Bila kupoteza muda agenda zilitajwa ikiwemo hotuba ya Mwenyekiti, ambapo muda wote aliyokuwa akizungumza wajumbe walikuwa wakimpigia makofi na kumshangilia.

Mara baada ya hotuba yake, taratibu nyingine zilifuata kwa mujibu wa ratiba iliyokuwepo kwa siku hiyo (jana).

No comments:

Post a Comment