Tuesday, 25 August 2015
DK. MAGUFULI AMEDHIHIRISHA WAZI KUWA NI KIONGOZI SAHIHI KWA WATANZANIA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) juzi kilizindua rasmi kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani huku kikitangaza ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2015/ 2020.
Katika mkutano huo wa ufunguzi uliofanyika kwenye viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi na wanachama wa CCM, mgombea urais wa Dk. John Magufuli alitangaza vipaumbele vyake 32 iwapo atachaguliwa kuwa rais.
Huku akishangiliwa kwa nderemo na vifijo na wananchi, Dk. Magufuli alisema serikali yake ya awamu ya tano itakuwa ya viwanda na kwamba ataanzisha mahakama maalumu kwa ajili ya kuwashughulikia wezi na mafisadi wanaokula mali za wananchi.
Aidha, Dk. Magufuli alisema serikali yake itaimarisha viwanda ikiwa ni pamoja na kujenga vingine vipya ili kuongeza ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa nchi na kwamba viwanda vilivyobinafsishwa na ambavyo havijaendelezwa, vitarejeshwa.
Ahadi zingine zilizotolewa na Dk. Magufuli ni pamoja na kuwataka wananchi wajiandae kwa mabadiliko makubwa ya kiutendaji wakati wa utawala wake ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta za kilimo, mifugo, afya na uvuvi ili ziweze kukuza uchumi wa nchi.
Mbali na Dk. Magufuli, mkutano huo wa ufunguzi wa kampeni pia ulihutubiwa na Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete, Marais wastaafu wa awamu ya pili na ya tatu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa na Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba.
Tunampongeza Dk. Magufuli kwa hotuba yake maridhawa, ambayo licha ya kuelezea Ilani ya Uchaguzi ya CCM, pia imeelezea kwa kina, yale ambayo serikali yake imepanga kuyafanya na kuyapa kipaumbele katika kipindi cha miaka mitano ijayo ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Kutokana na hotuba yake hiyo, ni wazi kuwa Dk. Magufuli anazifahamu vyema kero zinazowasumbua Watanzania hivyo ndiye mgombea pekee miongoni mwa wagombea wanane waliopitishwa kuwania urais mwaka huu, mwenye uwezo wa kuzitatua kutokana na uwezo, uzoefu na rekodi yake ya utendaji kazi.
Hotuba hiyo ya Dk. Magufuli, Rais Kikwete na marais wastaafu pia zimeonyesha dhahiri kuwa hakuna chama kinachoweza kutoa rais bora zaidi ya CCM na kwamba wananchi watarajie mabadiliko makubwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Aidha, tunawapongeza Mzee Mwinyi na Mzee Mkapa kwa kuwaeleza wazi wananchi kwamba hakuna chama kinachoweza kuwakomboa Watanzania zaidi ya CCM na kwamba Dk. Magufuli amekidhi sifa zote zilizokuwa zikihitajika kwa mgombea wa Chama.
Kwa kuzingatia ukweli huo, tunatoa mwito kwa Watanzania kutofanya makosa ya kuvipigia kura vyama vya upinzani katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, kwa lengo la kufanya majaribio ya uongozi wa nchi kwa watu wasiokuwa na uwezo na sifa za uongozi. Kufanya hivyo ni kosa kubwa.
Ieleweke kuwa sera thabiti na ilani yenye kutekelezeka inayotumiwa na CCM ni ngao imara ambayo wana-CCM wanajivunia kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania kwa miaka mingine ijayo, hivyo hakuna sababu kwa wananchi kuvipigia kura vyama vya upinzani, ambavyo havina sera wala ilani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment