Tuesday, 25 August 2015
NGELEJA AIMALIZA CHADEMA
NA MWANDISHI WETU, SENGEREMA
MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Sengerema mkoani Mwanza, William Ngeleja, ameusambaratisha upinzani baada ya vigogo wa juu wilayani humo kujiunga na CCM.
Hali hiyo imejitokeza baada ya wanachama hao kubaini, kutokuwepo kwa dhamira ya dhati ndani ya CHADEMA ya kuwaletea maendeleo wananchi na kutotekeleza misingi ya demokrasia kwa vitendo.
Wanachama hao wa ngazi za juu wa chama hicho waliojiunga na CCM ni aliyekuwa Katibu Mwenezi wa Chadema kata ya Ibisabageni, Boniface Malembela, Evarist Nkingwa, Gabriel Kapama na Salum Mathias.
Wengine ni George Kaju,Hamadi Ikumbo,Meta Nayo na Mathias Ladislaus, ambao wamesema wamechoshwa na siasa za mizengwe zilizopo Chadema.
Wakizungumzia sababu zingine zilizowafanya kukihama chama hicho, walisema ni kuendekeza upendeleo na kutoheshimu mawazo ya wanachama wao hususan katika mchakato wa kura za maoni wa kumpata mgombe ubunge wa jimbo hilo.
Katika mchakato huo, walisema Kamati Kuu ya chama hicho kwa makusudi ilikata jina la Kimasa Shejamabu, aliyeongoza kura za maoni za ubunge na nafasi ya hiyo kupewa Hamisi Tabasam, aliyeshika nafasi ya pili.
Walidai Tabasamu hana sifa za kuwa mbunge wa Sengerema kwa sababu elimu yake ni ya darasa la pili na mtu asiyeaminika na kuheshimika katika jamii.
Walisema wameamua kurudi CCM, kwa sababu ya kuridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya Chama na uchapakazi wa mbunge Ngeleja.
Walisema watampigia kampeni Ngeleja, mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli na madiwani kwa sababu wanaona juhudi zinazofanywa na serikali ya CCM kutatua kero za wananchi wa Sengerema.
"Tunashuhudia utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji unaoendelea hivi sasa mjini Sengerema, wenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 23, hivyo hatuoni sababu ya kutoendelea kumuunga mkono Ngeleja," walisisitiza.
Kufuatia kuhama huko kwa wanachama hao wa Chadema, wananchi wa jimbo hilo wameupongeza uamuzi huo, waliouita kuwa ni wa busara kwa sababu CCM, imekuwa ikiwatatulia changamoto zao kila siku na sio kulalamika kama wanavyofanya wapinzani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment