Saturday, 29 August 2015

DK MWAKYEMBE: LOWASSA ANAHUSIKA NA RICHMOND



Asema aliingia jikoni 'akachomoa mboga ya watoto'
Asisitiza akiendelea kujitetea, ataanika uozo zaidi
Dk. Magufuli avunja ngome ya CHADEMA, aahidi neema
Mwakipesile apasuka; waangalizi 120 EU kutua nchini

SELINA WILSON NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA

WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond na mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, hafai kuongoza nchi kwa kuwa uchunguzi ulithibitisha kwamba 'aliingia jikoni na alichomoa mboga ya watoto'.

Lowassa ambaye alijiuzulu Februari 2008 kwa kashfa hiyo baada ya Ripoti ya Kamati Teule ya Bunge ya uchunguzi juu ya Richmond kusomwa bungeni kufuatia uchunguzi uliofanywa tangu mwishoni mwa mwaka 2007.

Waziri wa Afrika Mashariki na mgombea ubunge wa CCM jimbo la Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe aliamua kuweka hadharani namna anavyomfahamu mgombea huyo na kusema hana sifa za kuongoza nchi.

Dk. Mwakyembe ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyofanya uchunguzi wa sakata la Richmond, alisema hayo jana katika viwanja vya John Mwakangale Mjini Kyela katika mkutano wa kampeni za uchaguzi.

“Bahati nzuri wagombea urais wote nawafahamu, huyo mwingine (Lowassa) hafai. Nilichokifanya bungeni ilikuwa ni maelekezo yenu wana Kyela kwamba niwe mtu mkweli katika kusimamia haki. Suala lililomtoa uwaziri mkuu nililisimamia mimi. Tulimchunguza tukamwambia baba tumekukuta kweli jikoni unachomoa mboga ya watoto. Tumekukuta unachomoa mboga ya wazee.

“Tulichokisema bungeni kilikuwa na ukweli na mpaka leo bado kinasimama. Mzee huyu hafai ndugu zangu msimpe kura mtapoteza kura zenu,” alisema.

Alisema suala la Richmond lilimalizika, lakini baadhi ya watu wanalileta na kulizungumza kwa kupotosha wakati kila jambo lipo wazi kwamba kiongozi mwandamizi wa serikali aliipatia kampuni hewa mabilioni ambayo mpaka leo wananchi wanapata tabu.

“Wakiendelea kuzungumzia Richmond nitasema na mengine, nitaweka mezani ili kila mtu ajue uchafu uliokuwemo ndani ya Richmond. Wakizungumza tutaweka mambo hadharani kila walichokifanya,” alisema.

Alisema kuna ushahidi kuwa Lowassa 'alidokoa mboga ya watoto' na ndio maana mpaka sasa watoto wanalia njaa.

“Wanasema kama ilithibitika kwa nini hakufikishwa mahakamani, nataka niwaambie na wanasheria wanukuu kesi za jinai hazina ukweli, anaweza kufikishwa mahakamani wakati wowote,” alisema.

Dk. Mwakyembe alisema mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli aliyepitishwa na Chama kupeperusha bendera ni chaguo sahihi kwa kuwa mchapakazi na ana sifa za uadilifu na uaminifu, hivyo anafaa kuongoza nchi.

“Mimi nakuita Mheshimiwa Rais kabisa. Wana Kyela tuna kila sababu ya kuunga mkono kwa kuwa wewe ni kiongozi bora mwenye kuahidi na kutekeleza. Dk. Magufuli mimi ni mwalimu wangu, amenipiga shamba darasa kwa miaka miwili. Nimetoka pale nimejifunza kitu kimoja kikubwa kwamba kwake ‘zege halilali’. Nilipikwa nikapikika,” alisema.

Alisema katika kipindi kifupi kilichopita alitia saini mradi wenye thamani ya sh. bilioni 56 wa ujenzi wa barabara ya lami ya Kyela - Matema Beach yenye kilometa 38 na mkandarasi yuko eneo la kazi.

Dk. Mwakyembe alisema wakati Dk Magufuli alipoteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi mwaka 2010 aliahidi watu watatoka Mtwara hadi Kagera kwa teksi na kweli alitekeleza, hivyo ni mtu mwenye ahadi za kweli.

Aliwaomba wakazi wa Kyela wamchague ili awe Rais wa Tanzania aendelee kuleta maendeleo ya nchi ambayo yanahitaji tingatinga lenye uwezo wa kuchapa kazi.

“Tulikuwa na shida ya kivuko katika ziwa Nyasa, Dk. Magufuli alisema ni vizuri kujenga cherezo (eneo la kutengenezea vivuko na meli) ambapo alitenga sh. bilioni 28.5 na kuanza kazi hiyo ambayo sasa ujenzi wake umefikia asilimia 95,”alisema.

Alisema baada ya kukamilisha mradi huo, Bandari ya Itungi, itakuwa ni eneo muhimu na litakalokuwa na huduma ya kutengeneza meli na vivuko na kutakuwa hakuna haja ya kwenda Malawi kufuata huduma hiyo.

Kutokana na utendaji huo, Dk. Magufuli anatosha kuwa rais na Lowassa ni sawa na aliyejenga kwenye hifadhi ya barabara, hivyo tingatinga Magufuli atasafisha.

Awali akizungumza katika mkutano huo, Dk. Magufuli alisema akishinda urais ataanzisha mahakama maalumu kwa ajili mafisadi na majizi ili kudhibiti vitendo hivyo.

Dk. Magufuli alisema mafisadi na wala rushwa ndio wanaosababisha wananchi wa chini kukosa huduma muhimu, hivyo atakahikisha anawadhibiti na ataokoa fedha ili ziende kwa wananchi.

“Yaani natamani nipasuke, lakini bahati mbaya kifua kinanisumbua lakini kwa jina la Yesu kitashindwa.
Nitapambana nao, nitahakikisha nalala nao mbele ili kuleta mabadiliko bora kwa Watanzania,”alisema.

Dk. Magufuli pia alikabidhiwa  zawadi ya mkuki na wazee machifu wa Kyela na alikabidhiwa jina rasmi la Simonile ambalo ni jina la chifu Mwakyembe.

Akizungumza kwa nyakati tofauti katika mikutano ya kampeni ya Kyela na Rungwe, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, William Lukuvi, alisema Dk Magufuli ni tingatinga, hivyo wamletee Power Tiller ili wafanye naye kazi .

Lukuvi alisema amekuwa akifanya mikutano 12 kwa siku na jana alikuwa na mikutano minane, hiyo inaonyesha kwamba ni mchapa kazi.

AVUNJA NGOME CHADEMA

Dk.Magufuli alifanikiwa kuvunja ngome ya CHADEMA katika Kata ya Kiwira wilayani Rungwe, baada ya vigogo zaidi ya 16 kujiunga na CCM na kukabidhiwa kadi zao.

Kata ya Kiwira ilikuwa inatambulika kuwa ngome ya chama hicho na hivyo kuondoka kwa wanachama hao ni sawa na imesambaratika.

Tukio hilo lilijiri kwenye mkutano wa kampeni za mgombea huyo, ambapo pia alitumia nafasi hiyo kuwanadi wagombea ubunge wawili wa CCM, Atupele Mwakibete (Busokelo) na Sauli Amon (Rungwe).

Akizungumza kwenye mkutano huo, mmoja wa vigogo hao, Frank Kajigili, alisema wamekaa na kutafakari kwa kina, lakini mwisho wa siku wameamua kurudi CCM kwa kuwa CHADEMA ni chama ambacho hakina nia ya dhati ya kuwatumikia Watanzania kutokana na viongozi wake kujaa ubabaishaji.

“Rais mtarajiwa ama nikuite Rais Kamili mheshimiwa Dk.Magufuli leo (jana) nakukukabidhi kadi yangu, kwamba nimeachana na siasa za CHADEMA na najiunga na CCM,” alisema Kajigiri na kuufanya umati wa wananchi uliohudhuria mkutano huo kulipuka kwa shangwe .

Kajigiri alisema wananchi wa mji wa Tukuyu na wilaya nzima ya Rungwe, wasikubali kudanganyika na maneno ya wanasiasa wachache ambao maisha yao hayana vielelezo.

Dk. Magufuli alifurahishwa na hatua hiyo na ili kuthibitisha hilo aliwaita wote na kupiga nao picha.

Awali, akizungumza mjini Tukuyu wilayani humo, alisema ujenzi wa kilometa 80 kwa kiwango cha lami, katika barabara ya Katumba utatekelezwa na kuwatoa hofu wananchi.

Alisema barabara hiyo ambayo ni muhimu kwa uchumi wa wilaya hiyo itatengenezwa kwa kiwango cha lami kama ilivyokuwa imekusudiwa na serikali.

“Nikiwa Waziri wa Ujenzi nilikuwa natumwa na Rais Jakaya Kikwete kutengeneza barabara sasa nawaomba mnichague niwe Rais ili sasa na mimi nimtume waziri wangu nitakayekuja kumteua kufanya kazi hii,” alisema Dk. Magufuli na kushangiliwa.

Vilevile alisema atashughulikia kero ya maji iliyopo wilayani humo na anachohitajika kutoka kwa wananchi ni kumchagua kwa kura nyingi.

Alisema kuanzia mwakani, serikali yake ya awamu ya tano chini ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM imeazimia wanafunzi wote kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne watasoma bure na kuwa wapo baadhi ya wanasiasa watahoji fedha hizo zitatoka wapi.

Aliwatoa hofu kwa kuwaeleza wananchi kuwa amekaa serikalini kwa kipindi cha miaka 20, hivyo anatambua vyema maeneo mengi ambayo fedha za serikali zimekuwa zinavuja na kuwanufaisha watu wachache, hivyo ataziba mianya hiyo ili zilete matunda kwa Watanzania wote.

MWAKIPESILE APASUKA

Kutoka Kyela, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, alisema Watanzania watafanya vizuri kumchagua Dk. Magufuli, kwa kuwa anastahili kushika wadhifa huo kutokana na umakini na uchapa kazi wake.

Alisema kabla ya kustaafu nafasi hiyo, aliwahi kufanya kazi na mgombea huyo kwa miaka sita, hivyo anatambua uchapakazi wake kutokana na kuwa mwadilifu, mwaminifu, mnyeyekevu, mtu makini na mzalendo wa kweli kwa taifa lake.

Mwakipesile aliyasema hayo alipopewa nafasi ya kuwasalimia wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Mwakangale, mjini Kyela.

“Katika maisha yangu, leo ni siku ambayo nimefurahi sana na nawashukuru wananchi wa Kyela kwa mapokezi haya mazuri. Namfahamu Dk. Magufuli kwani nimeingia naye bungeni mwaka 1995,” alisema Mwakipesile.

Alisema Watanzania wanatakiwa kukumbuka kiongozi anayetafutwa ndiye atakuwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, lakini kama hana upendo kwa Watanzania na ni fisadi hawezi kufaa katika nafasi hiyo.

“Wananchi wa Kyela tunakuhakikisha Rais mtarajiwa kuwa Oktoba 25, mwaka huu tutakupigia kura zote za ndiyo kwani wewe ndiye unayestahili kuwa Rais wa serikali ya awamu ya tano,” alisema Mwakipesile.

Naye Mwenyekiti wa CCM, mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi, alisema awali kulikuwa na maneno ya mitaani kuwa CCM ndiyo inasambaratika, lakini mara baada ya makapi yaliyokuwemo ndani ya Chama kuondoka, Chama ndio kimekuwa imara zaidi.

Naye Rachel Kyala kutoka Dar es Salaam anaripoti kuwa, waangalizi 120 kutoka Umoja wa Ulaya (EU), wanatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote kuanzia sasa kufuatilia masuala ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Waangalizi hao wanatarajia kufuatilia mwenendo mzima wa uchaguzi kuanzia kampeni, upigaji kura hadi matokeo na kutoa maoni kupitia taarifa maalumu watakayoiandaa.

Balozi wa EU nchini, Filiberto Sebregondi, alisema hayo jana wakati wa utiaji saini hati ya makubaliano kati ya Tanzania na umoja huo kuhusu usimamizi wa uchaguzi mkuu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Liberata Mulamula, alisema makubaliano hayo ni ya awali kwa ajili ya kuwakaribisha nchini waangalizi hao kwa kuwa wizara hiyo ndiyo yenye jukumu hilo.

No comments:

Post a Comment