Tuesday, 25 August 2015

MAGUFULI: NITAFUTA KODI ZA AJABU AJABU


Mgombea wa Urais kwa tiketi ya CCM Dk. John Pombe Magufuli akiwaonyesha ishara ya ushindi wananchi waliojitokeza kwa wingi kwenye uwanja wa Nelson Mandela.
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli akisalimiana na mbunge wa zamani wa Sumbawanga, Dk. Chrisant Mzindakaya baada ya kuwasili kwenye uwanja wa Nelson Mandela.
Mgombea wa Urais kwa tiketi ya CCM Dk. John Pombe Magufuli akihutubia umati wa wakazi wa Sumbawanga mjini kwenye mkutano wa kampeni ambapo aliwaambia wananchi hao kuwa atawatumikia kwa nguvu zake zote, na hatokuwa na simile na watendaji wazembe.
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha CCM Dkt John Pombe Magufuli akiwasalimia wananchi wa mji wa Namanyere wilayani Nkasi (hawapo pichani),kabla ya kuanza kuwahutubia kwenye mkutano huo wa kampeni,kati ni Mjumbe wa Kamati kuu ya CCM,Mhe. Mizengo Pinda pamoja na anaewania nafasi ya Ubunge katika jimbo la Nkasi Ndugu Ali Kessy

Ni zinazohusu bodaboda, mama ntilie na machinga L Asema vigogo wanaodhulumu wanyonge mwisho umefika

NA  SELINA WILSON, SUMBAWANGA

MGOMBEA Urais wa CCM, Dk. John Magufuli, ameahidi kufuta kodi alizoziita za ajabu ambazo si rafiki katika kumuinua Mtanzania wa kipato cha chini.

Pia, amesema akipewa ridhaa ataunda Baraza la Mawaziri ndogo na ambalo atalichuja kwa utaratibu maalumu ili kupata timu bora itakayofanya kazi usiku na mchana kwa maslahi ya Watanzania wote.

Aidha, amewaonya watendaji na vigogo waliojiingiza katika mtandao wa kudhulumu wanyonge kuacha haraka na kuanza kutubu dhambi hizo ili waungane katika kuwaletea Watanzania maendeleo.

“Nafahamu umati huu uliofurika hapa wengi mtanipigia kura, lakini baadhi ya wakubwa hawatanichagua kwa sababu wananijua vizuri shughuli yangu, hivyo kwa kuwa nyie wadogo ndio wengi sina shaka na ushindi.

“Najua fedha zipo, najua mapato ya serikali yanavujia wapi, nitabana matumizi na kuhakikisha fedha zinakwenda katika shughuli za maendeleo ya wananchi.

“Nawahakikishia kwamba fedha zote zinazoliwa huko juu, zitakwenda kwenye maendeleo ya wananchi… nikiahidi lazima nitekeleze na sina kawaida ya kusema uongo kwa kuwa namuamini Mungu na natekeleza amri zake,” alisema Dk. Magufuli.

Akizungumza katika Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga, Dk. Magufuli alisema vigogo ambao hawatampigia kura wanatambua akiiingia madarakani hawatapona.

Alisema kila mwaka serikali imekuwa ikitenga fedha kwenye mfuko wa barabara, lakini Mji wa Sumbawanga, hakuna barabara za lami kwenye mitaa.

Dk. Magufuli alisema kwa mwaka huu mfuko wa barabara umetenga zaidi ya sh. bilioni 800,  hivyo haoni sababu ya mitaa ya mji huo kukosa lami wakati Mpanda zipo barabara za lami.

Alisema kwa kuwa yeye ndiye anayesimamia mfuko huo akiingia madarakani atahakikisha barabara hizo zinajengwa kwa lami.

Kuhusu kodi za ajabu ajabu, Dk. Magufuli, alisema ataondoa kodi hizo zikiwemo zinazotozwa kwa mama ntilie, boda boda na machinga ambazo zimekuwa kero.

Alisema anataka kujenga nchi ambayo watu watafanya kazi bila kusumbuliwa kwa kuwa hakuna sababu ya wananchi kurundikiwa mzigo mkubwa wa kodi.

Alisema Watanzania ni wasikivu na kwamba, wakijengewa mazingira mazuri ya kufanya biashara watalipa kodi halali kwa serikali bila kushurutishwa.

“Hili nimeliona na nitaanza nalo…kodi za ajabu ajabu ambazo zingine zinaingia mifukoni mwa watendaji wa halmashauri nitazifuta…ndugu zangu mama ntilie, machinga na bodaboda nataka wafanye kazi zao kwa amani bila bughudha,” alisema huku akishangiliwa na umati wa watu.


ELIMU YA SEKONDARU BURE


Watanzania wataanza kunufaika na huduma ya elimu ya sekondari bila kulipa karo katika awamu ya tano ya uongozi wa serikali.

Mgombea urais wa CCM, Dk. Magufuli alitoa ahadi hiyo katika maeneo mbalimbali aliyofanya mikutano ya hadhara ya kampeni ambapo alisititiza kwamba mwanafunzi ataanza kidato cha kwanza hadi kidato cha nne bila kulipa karo.

Dk. Magufuli alisema Tanzania ina utajiri mkubwa wa rasilimali za madini, samaki na zingine ambazo zinaweza kutumika kulipa karo wanafunzi hao.

Alisema fedha zipo, lakini zinatumiwa na wajanja wachache wala rushwa, hivyo akichaguliwa kuwa Rais atadhibiti mianya ya wala rushwa na kuzitumia fedha hizo katika kutoa huduma kwa wananchi.

“Fedha nyingi zinapotelea kwa wala rushwa, nikiingia madarakani hao ndio nitashughulika nao kwanza ili fedha hizo ziende kwenye maendeleo,”alisema.

Katika hatua nyingine Dk. Magufuli akiwa katika mji wa Namanyele, alisema atahakikisha anadhibiti wezi wa dawa wanaoiba na kupeleka katika maduka ya dawa.

“Wezi wa dawa, madaktari wanaopeleka dawa kwenye maeneo mengine moto wao unakuja. Unakwenda hospitali unaandikiwa dawa kwenye karatasi unaambiwa kanunue pale dukani. Zimefikaje kwenye hilo duka, sitakubali,” alisema.

Alisema kama ni suala la kuboresha maslahi ya madaktari na wauguzi litapewa umuhimu, lakini wezi hawataruhusiwa.

“Nitaboresha maslahi ya wafanyakazi wote, wauguzi, walimu, madaktari na wengine ili kuhakikisha wanafanya kazi zao vizuri,”alisema.


BARAZA LA MAWAZIRI

Dk. Magufuli alisema ataunda baraza la mawaziri wa kujibu hoja za wanyonge na sio kuleta habari za kuwazungusha kwa kusema mambo ya mchakato, mara kesho kutwa litashughulikiwa.

Alisema anahitaji mawaziri wachapa kazi na aliwatahadharisha watu atakaowateua kama mtu ataona anashindwa kazi ni kheri akatae siku hiyo hiyo.

“Habari za mchakato, mara unaitwa kwa wananchi unatoa ahadi ya kesho kutwa, kabla ya kufika hiyo keshokutwa atakuwa ameshavuliwa cheo chenyewe,”alisema.

Dk. Magufuli alisema inawezekana wengine wakakimbia uwaziri, lakini yeye anachohitaji ni kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo ya Watanzania.

Alisema atawatumikia Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama na kwamba amegombea nafasi hiyo kwa kuwa ana uwezo wa kuongoza nchi na ataweka safu bora ya uongozi.

“Tusibaguane kwa sura zetu, tujenge umoja  na amani. Nitazunguka nchi nzima kwa barabara ili nijue changamoto za Wanzania wote. Huu ni wakati wa kupata Tanzania mpya umefika na Tanzania mpya italetwa na mimi Magufuli,” alisema.

Dk. Magufuli, pia alisema ataimarisha ulinzi na usalama ili kuhakikisha wananchi wanafanya shughuli katika mazingira salama na kupata huduma bora muhimu.

Akiwa Nkasi Kaskazini, Dk. Magufuli alimnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo, Ally Keissy, na kuwaomba wananchi wamchague kwa kuwa ni mtu anayependa kusema ukweli.


WAZIRI MKUU PINDA

Akizungumza na maelfu ya wananchi wa Sumbawanga, Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliwaponda wanasiasa wanaofanya siasa za maigizo.

Pinda aliwashangaa wengine ambao wameanza kupanda daladala ili kutafuta kura kwa wananchi.

Aliwataka wananchi wahoji siku zote walikuwa wapi na sasa ndio wapande daladala.

Katika hatua nyingine, Pinda alivunja ukimya juu ya mchakato wa kumpata Dk. Magufuli na kusema ulikwenda vizuri na anamuunga mkono kwa asilimia 100 kwa kuwa ni kiongozi bora.

“Tulikuwa 42 baadaye 38 na mchujo ulipopita ilikuwa ni lazima apatikane mmoja atakayekuwa mgombea wa CCM na ndio tumempata Dk. Magufuli ndiye mgombea wetu,”alisema.

Alisema kuna watu walianza kumpigia simu na kumuuliza mbona hajaonekana uwanjani Jangwani Dar es Salaam, kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi.

“Mimi ni muumini wa chama changu CCM , namuunga mkono Dk. Magufuli na mchakato wa kumpata ulikwenda kihalali kwa asilimia 100, na hakuwepo jangwani kwa kuwa aliwahi kufanya maandalizi ya mikutano ya kampeni baada ya mkoa wake wa Katavi kupewa heshima ya kuanza kampeni,”alisema.

Aliwataka wananchi wamchague Dk. Magufuli na wabunge wa CCM ili iendelee kuwatumikia kwa sababu ya kiongozi mtendaji ambaye anaweza kuwakomboa Watanzania.

No comments:

Post a Comment