Tuesday, 25 August 2015

MGOMBEA URAIS AMLIPUA SUMAYE





Asema anasumbuliwa na njaa
Polepole amvaa tena Lowassa
Ataka Watanzania wamuogope
Kamishna Kova ampiga marufuku

Na waandishi wetu

MGOMBEA urais wa UPDP, Fahmi Dovutwa, amewataka watanzania kumuepuka Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, kwa kuwa ni mnafiki hivyo waendelee kumpuuza.

Amesema kitendo cha Sumaye kuungana na Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, aliyekuwa akimpinga kwa kutokuwa msafi ni cha ajabu na kinaashiria muungano huo hauna dhamira njema kwa Watanzania.

Aidha, aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole, amewaasa Watanzania kukataa hadaa na ushawishi unaofanywa na Lowassa kwa kuwa mtu asiye muadilifu akipewa urais nchi itayumba.

Aliwataka kuwa makini na hadaa ndogo ndogo zinazofanywa na Lowassa ikiwemo kupanda daladala na badala yake waangalie rekodi na uadilifu wa mtu.

Dovutwa katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, alisema ni ajabu Sumaye kusimama hadharani na kumsifu Lowassa, ambaye alikuwa akizunguka kila kukicha kumtangaza kuwa si msafi na ana tuhuma.

"Sumaye aliwahi kusema anayenunua watu kwa fedha akipewa nafasi ya kugombea urais atatoka kwenye chama chake (CCM), huku akimnyooshea kidole Lowassa, alimchambua vya kutosha na kauli hiyo aliirudia kila mara.

"Huyu Sumaye ana tatizo la njaa, si kwamba shida ya chakula bali njaa ya kutokinai, maana yake hatosheki, asiyetosheka hana shukrani na asiye na shukrani hana aibu ni sababu kubwa ya kumuasi Mwenyezi Mungu," alisema.

Hata hivyo, alisema muungano huo kamwe hauwezi kuleta tija na kuwabadili watu mawazo na rekodi walizonazo na kwamba, Lowassa atausikia urais kwenye redio na luninga tu.

"Kwa sababu hoja zilizofanya ampinge ndani ya CCM bado hajaeleza kama kaziacha… hata niliposikiliza hotuba yake wakati anahamia UKAWA sikuelewa hata chenye maana," alisema Dovutwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa UPDP.

Aliongeza kuwa katika kudhihirisha Sumaye ana unafiki hakuweza hata kutaja chama ambacho anahamia na badala yake alibaki akijiumauma ulimi.

"Mwisho Watanzania wajiulize watu aina ya Sumaye ndio viongozi tuwatakao na kweli tutafika huko tuendako?," alihoji.


Polepole amvaa Lowassa

Akizungumza na Uhuru mjini Dar es Salaam, jana, Polepole alisema Watanzania wanapaswa kuwa makini na wakae mbali na ushawishi wa Lowassa.

Alitoa ushauri huo kutokana na Lowassa kuanza kuwahadaa wananchi kwa kujifanya kupanda daladala na kutembelea mama ntilie mitaani, jambo ambalo hakuwahi kulifanya.

Hata hivyo, mkakati huo wa Lowassa kutafuta kuungwa mkono, ulionekana kugonga mwamba kutokana na wananchi kuhoji alikuwa wapi miaka yote na badala yake amesubiri sasa wakati anapoisaka Ikulu.

“Nawaomba Watanzania kuwa makini katika kipindi hiki na wasikubali ushawishi wa kawaida na mwepesi unaofanywa na Lowassa na mgombea mwenza wake, Juma Duni Haji.

“Watu wakae na kutafakari na kujadili kwa kina huku wakiweka maslahi ya taifa mbele kabla ya kufanya uamuzi. Mambo ya kuigiza hayana nafasi kwa sasa…ni kwa nini hakufanya wakati akiwa madarakani?,” alihoji Polepole.

Alisema serikali ya awamu ya nne imefanya mambo mengi ya kijivunia na kwamba, wananchi waendelee kuiamini CCM kwa kufikia mafanikio hayo.

Polepole alisema nafasi ya urais anapewa mtu,  hivyo ni lazima angaliwe mtu muadilifu anayeweza kulitumikia taifa kwa moyo mmoja.

Kamishna Kova amempiga marufuku

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imepiga marufuku ziara za Lowassa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

Onyo hilo la Polisi limekuja ikiwa ni siku chache baada ya Lowassa kuanza kuzunguka kwa lengo la kujaribu kutafuta kuungwa mkono, akitembelea maeneo tofauti na kupanda daladala.

Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema mtindo ulioanzishwa na Lowassa ni kinyume cha utaratibu na umekuwa kero kwa wananchi.

Alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeandaa ratiba maalumu ya kampeni za wagombea wa vyama vyote, ambapo polisi imepewa jukumu la kutoa ulinzi kwenye mikutano hiyo.

“Huyu mgombea amepanga ratiba bila kutupa taarifa hii ni hatari kwa usalama wake… tunataka uchaguzi huu upite kwa amani. Tueleweke kwamba hatuna nia ya kuzuia mafanikio ya mtu kisiasa kwa njia yoyote, lakini sheria zifuatwe,” alisema Kova.

Alisema ziara za Lowassa si rasmi na kutokana na hilo wamepiga marufuku ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza huku polisi wakiwa hawana taarifa na uwepo wake.

Kamishna Kova alisema mikusanyiko hiyo ya madereva wa bodaboda, wafanyabiashara wadogo na makundi mengine ya watu, imesababisha taharuki na usumbufu mkubwa huku wananchi wakilalamikia msongamano wa watu na magari, hivyo shughuli za uzalishaji mali kusimama kwa muda.

Jana, saa sita mchana katika makutano ya mtaa wa Swahili na Uhuru, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lucas Mkondya, alilazimika kukutana na Lowassa, ambaye alikuwa akitaka kwenda Soko Kuu la Kariakoo na kumuonya kuacha kwa kuwa hana uhakika na usalama wake.

Kamishna Kova alisema Lowassa katika msafara wake huo alikuwa na bodaboda zaidi ya 40, magari lukuki hali iliyozua kero kubwa kutokana na kusababisha msongamano kwenye mitaa hiyo.

“Tumempa tahadhari kwa sababu mtindo alioanza kuufanya unaweza kuleta madhara na kero kubwa… huwezi kujua sio kila mtu anakupenda ukienda mahali, hivyo kwa masuala ya kiusalama tuna haki ya kuepusha hilo,” aliongeza.

No comments:

Post a Comment