Tuesday, 25 August 2015

MBEYA IKO TAYARI KWA MAGUFULI



Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda akimtambulisha mgombea wa CCM Dk. John Pombe Magufuli kwa wakazi wa Sumbawanga mjini kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Nelson Mandela mjini hapo.


NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, anatarajiwa kuwasili leo, mkoani Mbeya akitokea Sumbawanga. 

Dk. Magufuli, akiwa amefuatana na kamati ya kampeni Kitaifa, atapokelewa saa 4:30 asubuhi katika kijiji cha Nzoka, kilichoko wilayani Momba. 

Akizungumza na Uhuru jana, ofisini kwake, Katibu wa CCM mkoa, Mwangi Kundya, alisema mara baada ya Dk. Magufuli kupokelewa, msafara wake utaondoka na kwenda mjini Tunduma wilayani Momba, ambapo saa 6:00 mchana atafanya mkutano mkubwa wa hadhara. 

Kundya alisema baada ya kumaliza mkutano huo, Dk. Magufuli atakwenda moja kwa moja kata ya Itumba wilayani Ileje, ambako nako atafanya mkutano mkubwa wa hadhara kuanzia saa 7:00 hadi 9:00 mchana. 

Aliongeza kuwa baadaye msafara huo utaondoka wilayani Ileje na kwenda wilaya ya Momba, ambako saa 10 hadi 12 jioni, atakuwa na mkutano wa hadhara katika mji wa Vwawa, ambapo ratiba kwa siku hiyo ndio itakuwa imemalizika. 

Kwa mujibu wa Kundya, Agosti 27, mwaka huu, kuanzia saa 2:30 asubuhi hadi 3:30 asubuhi, Dk. Magufuli atahutubia mkutano wa hadhara eneo la Mlowo wilayani Mbozi, kisha atakwenda wilaya ya Mbeya, ambako, saa 4:00 asubuhi atakuwa na mkutano wa kampeni mji mdogo wa Mbalizi. 

Saa 6:00 mchana, msafara wa mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Magufuli, utakuwepo Mkwajuni-Chunya, ambako atafanya mkutano mkubwa wa hadhara na baadaye saa 8:00 mchana hadi 9:30 alasiri, atakuwa na mkutano wa hadhara eneo la Makongorosi. 

Kundya aliongeza Dk. Magufuli atakuwa na mkutano mwingine mkubwa wa hadhara kuanzia saa 10:30 jioni hadi saa 12 jioni, ambapo safari hii ataunguruma Chunya mjini. Agosti 28, mwaka huu, Dk. 

Magufuli ataondoka wilayani Chunya kwenda Kyela, ambako saa 4:00 hadi saa 5:00 asubuhi, atakuwa na mkutano wa aina yake Kyela mjini, jimbo linaloongozwa na mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Kampeni ya Taifa, Dk. Harrison Mwakyembe. 

Baada ya kumalizika mwa mkutano huo wilayani Kyela, msafara wa Dk. Magufuli utakwenda wilayani Rungwe, ambako saa 6:00 hadi saa 8:00 mchana, ataunguruma wilayani humo na baadaye saa 9:00 alasiri hadi saa 12:00 jioni, atakuwa na mkutano wa kampeni jimbo la Mbeya mjini. 

"Agosti 29, mwaka huu, mgombea wetu ataondoka mkoani Mbeya kwenda mkoa jirani wa Njombe, kuendelea na mikutano ya kampeni," alisema Kundya. 

Kundya aliwaomba wana-CCM, wapenzi, mashabiki na wananchi kwa jumla, kujitokeza kwa wingi katika wilaya zote ambazo Dk. Magufuli atafanya mikutano ya hadhara ya kampeni ili waweze kusikia sera sahihi zenye lengo la kuwaletea maendeleo watanzania.

No comments:

Post a Comment