Tuesday, 25 August 2015

SAMIA KUTIKISA ARUSHA LEO

Mama Samia, akimpongeza Devis Mosha kwa hotuba nzuri

Mgombea mwenza kwa tiketi ya CCM, Mama Samia akiwanadi wagombea wa Ubunge, Davis Mosha (Moshi Mjini), Innocent Meleck (Vunjo) na Dk. Siril Chami (Moshi Vijijini) wakati wa mkutano huo.

MGOMBEA  mwenza wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan leo atanguruma katika mkoa wa Arusha, ambapo atafanya  mikutano saba ya kampeni katika wilaya sita za mkoa wa Arusha ya kuinadi Ilani ya CCM.

Akizungumza na Uhuru jana, katibu wa CCM mkoa wa Arusha, Alphonce Kinamhala, alisema taratibu zote za mikutano ya kampeni zimeshakamilika na kwamba watampokea leo saa saba mchana katika eneo la KIA, akitokea mkoa wa Kilimanjaro, ambako pia alikuwa na mikutano kadhaa ya kampeni.

Alisema mara baada ya kupokelewa, atakwenda moja kwa moja katika viwanja vya Ngaresero vilivyoko eneo la Usa River wilayani Arumeru, kwa ajili ya mkutano wa kampeni.

Alisema baada ya mkutano huo, atakwenda kwenye mkutano mwingine wa kampeni wilaya ya Arusha Mjini, utakaofanyika katika viwanja vya Samunge, ambapo  atahutubia wakazi wa Jiji la Arusha na viunga vyake.

Kinamhala alitumia fursa hiyo kuwataka wana CCM kujitokeza kwa wingi na kwa wakati ili kusikiliza sera za mgombea mwenza huyo, ambazo zimewakuna  wana CCM na wananchi wengi hapa nchini.

Alisema baada ya mikutano hiyo miwili, ataendelea na kampeni siku itakayofuata  katika wilaya za Longido, Mamlaka  ya Mji Mdogo Namanga, Monduli na Kataru kisha kwenda mkoa wa Manyara.

Wakizungumza na Uhuru, wakazi wa jiji la Arusha walisema wanaipongeza Ilani ya CCM iliyotolewa na Dk. John Magufuli kwani imegusa changamoto zote zinazowakabili Watanzania.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mkazi wa Jijini hapa, Zam Zam Ramadhan aliipongeza CCM kwa kumchagua Dk. Magufuli  kwa kuwa ni 'katapila' na anafanyakazi usiku na mchana kwa moyo na dhamira ya dhati ya kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo.

Kuhusu Samia, ambaye ni mgombea  mwenza, alisema haijawahi kutokea tangu Tanzania kupata uhuru kuwepo makamu wa rais mwanamke na  ana imani kina mama watapata maendeleo  makubwa ya kiuchumi kupitia mwanamke huyo mwenzao.

“Tumefarijika sana kwa uteuzi wa mwanamke mwenzetu kuwa mgombea mwenza, tunaamini wanawake wa Tanzania sasa tumepata mtetezi na mkombozi wetu,” alisema.

Alisema moja ya sera zake zilizowakuna wanawake wa mkoa wa Arusha ni ile ya kutoa milioni 50 kwa kila kijiji kwani wana uhakika wa kupata mitaji kupitia fedha hizo kwa ajili ya biashara ndogondogo.

No comments:

Post a Comment