MGOMBEA Urais kwa tiketi ya CCM, John Magufuli akitambulishwa kwa wananchi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika mkoani Katavi |
Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, John Magufuli akiwahutubia wananchi mkoani Katavi
SELINA WILSON, MPANDAMGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, ameanza kampeni zake za kwenda Ikulu katika Mkoa wa Katavi huku akiahidi kuwa akichaguliwa atamteua Waziri wa Ujenzi, ambaye ni mchapa kazi zaidi yake.
Dk. Magufuli, ambaye alianza ziara nyake jana katika Kijiji cha Mishamo wilayani Mpanda, alisema atahakikisha anapatikana waziri mzuri atakayeendeleza ujenzi wa barabara za lami nchini.
Pia, amesema ahadi yake ya kuanzisha Mahakama Maalumu kwa ajili ya kesi za ufisadi na uhujumu uchumi, ataitekeleza haraka ili kulinda rasilimali za taifa.
Alisisistiza kuwa anatambua kilio cha wananchi wa Mishamo na vijiji vingine vya jirani ni barabara ya Mpanda/Uvinza yenye urefu wa kilometa 195 na kwamba, akichaguliwa hilo atalifanya kwa vitendo na kulipa kipaumbele cha haraka.
“Kwa kuanzia tutataanza na kilometa 30. Tumeshaanza kufanya upembuzi yakinifu, baadae tutaijenga kwa kiwango cha lami, lakini tutakwenda kwa awamu,
“Mimi ndiye John Pombe Joseph Magufuli, naomba mnichague niwe Rais wenu. Nimekuja kwa barabara ili nione changamoto mnazopata, sikutaka kuja kwa helkopta, kwa mimi ndiye mtu wa barabara, mkinichagua hii ndio itakuwa kazi yangu ya kwanza,” alisema.
Alisema amekuwa waziri wa ujenzi kwa miaka 15, alikuwa anaagizwa anafanya, sasa akiwa rais yeye ndiye atakuwa anaagiza kazi hiyo ifanywe na waziri atakayemteua.
“Nawahakikishia nitateua waziri wa barabara atakayefanya kazi kuliko nilivyofanya mimi,” alisema.
Dk. Magufuli kila alipopanda jukwaani alitoa salamu kwa lugha mbalimbali, ikiwemo Kirundi, Kiha, Kifipa na Kisukuma, jambo ambalo lilikuwa likiibua kelele za shangwe.
Hakuna rais kusumbuliwa
Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli aliwahakikishia wakazi wa Mishamo na Katumba, ambako yalikuwa makazi ya wakimbizi wa Burundi kwamba, wameshakuwa raia hivyo hawatasumbuliwa.
Alisema sera nzuri za CCM ndizo zilizowafanya wawe raia wa Tanzania na hivyo yeye ataendelea kulinda maslahi yao na kuhakikisha changamoto zao zinatatuliwa.
Dk. Magufuli alisema anafahamu changamoto za huduma za afya, maji na umeme, hivyo akichaguliwa atazitatua na kwamba, kwa kawaida yeye ni mtu aliyezoea kusema ukweli na akiahidi anatekeleza.
Alisema CCM kwa muda mrefu imekuwa ikipigania amani katika nchi mbalimbali, hivyo na wananchi wanapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda amani.
“Nyinyi mnajua yaliyotokea Burundi, sasa muwe makini msichague vyama ambavyo salamu zao ni ngumi , na ngumi maana yake na uvunjifu wa amani, hivyo chagueni CCM ili muendelee kuishi kwa amani,” alisema.
Mapema akiwa njiani kuelekea Mishamo, msafara wa Dk. Magufuli , ulisimamishwa mara tatu na umati wa wananchi katika vijiji vya Majalila, Vikonge na Luhafwe, ambako alilazimika kuhutubia na kuomba wananchi waichague CCM.
Akiwa katika vijiji hivyo, Dk. Magufuli alisema anatambua changamoto za zahanati, maji na umeme, hivyo atahakikisha wananchi wa vijiji hivyo wanapata huduma ili waweze kuendelea na maisha yao kama Watanzania wengine.
Katika kijiji cha Luhafwe, alisema mbali na ujenzi wa barabara ya lami, pia atashughulikia tatizo la migogoro ya ardhi na kuhakikisha wananchi wanapata haki.
Alisema anajua kuna watu wanahamishwa katika maeneo yao, lakini hawajui wanapelekwa wapi hivyo wakimchagua hatuwaangusha, atalitatua suala hilo.
Mgombea huyo wa CCM alisema ataleta maendeleo ya kweli kwa kuwa hana tabia ya kusema uongo na kwamba maendeleo hayana ukabila, chama wala dini.
Pinda: Dk. Magufuli ni mwanaume
Akimnadi Dk. Magufuli katika mikutano ya kampeni, Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema mgombea huyo ni mwanaume wa shoka na amefanya kazi kubwa ya kwa miaka 20 aliyomfahamu.
“Nimemfahamu Dk. Magufuli kwa miaka 20, katika utendaji wake amekuwa jembe na tingatinga na sasa tumemleta kwenu ili kuomba ridhaa tumchague awe rais wetu,” alisema.
Alisema CCM ndicho chama chenye sera zilizowafanya raia wa Burundi kuwa Watanzania kwa wale walioamua kubaki nchini baada kumalizika kwa machafuko yaliyotokea nchini kwao miaka ya 70.
Aliwataka wananchi wamchague Dk. Magufuli aliongoze nchi kwa awamu nyingine ya uongozi ili aendelee kulinda na kutatua changamoto zao na kuhakikishia kwamba watabaki kuwa raia wa Tanzania na hakuna atakayewasumbua.
Pinda, alisema CCM haikufanya makosa kumteua Dk. Magufuli kupeperusha bendera katika nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, kwa kuwa ni mtu mwenye kujituma katika utendaji wa kazi.
Aapa kula sahani moja na mafisadi
Akiwahutubia maelfu ya wakazi wa Mji wa Mpanda, Dk. Magufuli aliwatangazia kiama mafisadi na wala rushwa wanaoitafuna nchi na kuwaacha wananchi wakiwa masikini.
Alisema akiigia madarakani, mafisadi watamkoma maana hawatakuwa na nafasi na kuacha wala rushwa waendelee kufanya uharibifu, badala yake atawashughulikia.
Dk. Magufuli pia alisema akiwa Rais, atapunguza maadhimisho ya wiki mbalimbali za huduma kwa kuwa hakuna mantiki kuadhimisha wiki ya maji katika maeneo ambayo maji hakuna.
“Nitahakikisha tunatumia fedha kuleta maendeleo ili kuleta mageuzi ya kiuchumi na kwamba wananchi wote watanufaika kwa namna watakavyojituma katika kufanya kazi,”alisema.
Alisema atahakikisha serikali yake inajenqa viwanda kila mkoa ili kufungua fursa za ajira na kukuza uchumi wa nchi.
“Nimejitolea kuleta maendeleo ya Watanzania, naomba wananchi mnichague niwe Rais wenu, pia mnichagulie wabunge na madiwani wa CCM ili tufanye kazi ya kuleta mabadiliko ya kiuchumi,” alisema.
Akizungumzia mazao ya wakulima, alisema mtindo wa serikali kuwakopa wananchi, itakuwa historia na badala yake wananchi watapeleka mazao yao na kupatiwa fedha zao papo hapo.
Dk. Magufuli alisema anajua kwamba kuna changamoto ya umeme katika Mji wa Mpanda, atahakikisha anateua waziri bora wa nishati na madini na kumkabidhi jukumu la kuweka umeme Mpanda.
Alisema akishampa kazi hiyo, atamfuatilia kikamilifu na akishindwa kazi yake itabidi aondoke.
Barabara ya Tabora/Mpanda
Alisema anatambua kwamba barabara ya Tabora/Mpanda yenye kilometa 356 itajengwa kwa kiwango cha lami ili kufungua mawasiliano ili watu weweze kusafiri kwa haraka na kufanya shughuli za kiuchumi.
No comments:
Post a Comment