MGOMBEA Mwenza wa urais kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan, akiwasili kwenye uwanja wa shule ya msingi ya Hedaru |
WANACHAMA wa CCM wakigombea kumsalimia mgombea mwenza wa urais kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan |
Ashangaa kununuliwa na kambi ya ufisadi
Asema hafai kuwa kiongozi, aasa aogopewe
NA EPSON LUHWAGO, HEDARU
WAZIRI MKUU wa mstaafu, Frederick Sumaye, amezidi kushambuliwa kutokana na kitendo chake cha kuhamia upinzani na sasa ameeelezwa kuwa ni mwanamume kigeugeu na hapaswi kuaminiwa.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Shule ya Msingi Hedaru, Same mkoani Kilimanjaro, kwa ajili ya majimbo ya Same Mashariki na Same Magharibi.
Alisema kitendo cha Sumaye kuhamia upinzani na kukiuka kauli zake za awali kuhusu ufisadi, kimeonyesha ni mwanasiasa mnafiki na kigeugeu na haaminiki tena na jamii.
“Mtakumbuka kuwa Sumaye alisema iwapo CCM ingempitisha (Edward) Lowassa kuwa mgombea urais, atajiondoa kwa sababu mtu huyo ni fisadi. Lakini ni cha kushangaza amekula matapishi yake na kwenda upinzani na kuungana na mtu aliyekuwa akimpinga.
“Sasa kwa hili huyu si mtu wa kuaminiwa hata akapewa nafasi ya kuwa kiongozi wa ngazi yoyote. Kamwe wananchi tusihadaike na wapinzani ambao hawana uwezo wa kuongoza,” alisema.
Samia pia alisema Watanzania wasithubutu kufanya mabadiliko ya uongozi kwa kuchagua wapinzani kwa sababu hakuna nchi yoyote duniani iliyowahi kufanya mabadiliko ya uongozi kwa majaribio.
“Kwanza tufahamu kuwa CCM inaomba kura kwa ajili ya kuendeleza mambo ya maendeleo ambayo ilishayaanzisha na haitafuti kura kwa ajili ya kufanya majaribio.
“Pia tukumbuke kwamba CCM iko katika safari ya maendeleo kwani nia yake ni kuendeleza Watanzania kiuchumi na kijamii na tuna afya njema,” alisisitiza.
AAHIDI NEEMA
Akinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika mkutano huo, Samia alisema kero zinazowakabili wananchi wa wilaya ya Same zitapatiwa ufumbuzi na kwamba zimeainishwa katika ilani hiyo.
Akizungumzia barabara ya Mkomazi ambayo imekuwa kero kwa muda mrefu kwa wananchi wa Same Mashariki, alisema itajengwa kwa kiwango cha lami na kumaliza kabisa tatizo hilo.
“Rais ajaye wa CCM ni bwana barabara na bwana madaraja na ndiye tingatinga kama mjuavyo kwa hiyo kazi ya ujenzi wa barabara ndiyo yake. Pia hii ni ahadi ya Rais hivyo itakamilika,” alisisitiza.
Kuhusu maji, alisema utekelezaji wake unaendelea kwa kutoa maji kutoka bwawa la Nyumba ya Mungu na kwamba tatizo hilo litakuwa limemalizika mwishoni mwa mwakani au mwanzoni mwa mwaka 2017, hivyo kufanya kero hiyo kuwa historia.
Kwa upande wa migogoro ya wakulima na wafugaji, alisema wilaya hiyo ni moja ya maeneo yenye tatizo hilo na kwamba mipango ya kudumu ya kulimaliza imeandaliwa.
Katika kufanya hiivyo, alisema kazi kubwa itakayofanywa ni kupima ardhi na kuitenga kwa ajili ya makundi hayo mawili na kwamba baada ya kufanya hivyo, kundi litakaloingia katika eneo la mwingine, litachukuliwa hatua.
“Tumedhamiria kwa dhati kuhakikisha tatizo la ardhi na mapigano ya wakulima na wafugaji linafikia tamati. Yule atakayekiuka baada ya hapo hatutakuwa na msalie mtume naye,” alisema.
Sambamba na hilo, alisema serikali ijayo ya CCM itayapatia ufumbuzi malalamiko ya wafugaji kwa kukosa dawa na majosho, ambayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara.
Awali, Samia alianza rasmi kampeni kwa staili ya aina yake baada ya kutembelea wodi ya wazazi katika kituo cha Afya cha Hedaru, Same mkoani Kilimanjaro.
Samia alifanya hivyo baada ya kuwasili katika mji mdogo wa Hedaru kwa ajili ya kampeni. Baada ya kuwasili kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Hedaru, alikwenda moja kwa moja katika kituo hicho cha afya kilicho karibu na eneo la mkutano.
Hatua hiyo ilizua taharuki kwani watu waliokuwa kwenye uwanja wakisubiri maneno kutoka kwa mgombea mwenza huyo, walishitushwa na uamuzi wa kwenda kwenye kituo cha afya hivyo kuwafanya wamfuate.
Baada ya kufika kituoni hapo, alipokewa na Kaimu Mganga Mfawidhi, Dk. Renatus Simon, na kumweleza jitihada zinazofanywa katika kuboresha sekta ya afya.
“Mheshimiwa mgombea mwenza, ninapenda kukuarifu kuwa tunajitahidi kuboresha huduma za afya ikiwemo ya mama na mtoto, hivyo tunakukaribisha utembelee wodi hii na kuwaona wagonjwa,” alisema kisha kuongoza msafara kwenda wodini.
Baada ya kufika alikwenda moja kwa moja na kupita kila kitanda kilichokuwa na mgonjwa, wengi wao wakiwa kinamama waliojifungua muda mfupi uliopita.
Hatimaye alifika katika kitanda cha Irene Daudi (20), aliyejifungua mtoto wa kiume na kukibeba kichanga hicho kwa dakika kadhaa.
Hatua hiyo iliibua furaha na vigelegele kwa baadhi ya watu wakiwemo naibu mawaziri Ummy Mwalimu (Katiba na Sheria), Angella Kairuki (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Mahadhi Juma Mahadhi (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa), Anne Killango Malecela (Elimu na Mafunzo ya Ufundi) na Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Amina Makilagi.
Alipomaliza kuwaona wazazi na watoto hao, Samia alikwenda moja kwa moja kwenye chumba cha kujifungulia na kupata maelezo machache.
Baada ya hapo, Samia alikwenda moja kwa moja uwanjani kwa ajili ya mkutano wake wa kwanza wa kampeni wa hadhara, ambao ulihudhuriwa na mamia ya watu kutoka sehemu mbalimbali za wilaya ya Same.
Ziara katika kituo hicho ilimfanya Mbunge wa Same Magharibi, anayetetea kiti hicho, Dk. David Mathayo, ambaye muda mwingi alikuwa akionyesha furaha isiyo kifani huku baadhi ya wananchi wakiimba ‘Mathayo usilale bado mapambano’ huku yeye akipunga mkono na kutabasamu.
“Mimi ni mama na ni mzazi kwa sababu nimeingia leba mara nne na pia ni bibi kwa sasa. Nayajua matatizo ya kinamama wakati wa kujifungua, hivyo hilo ni suala la kipaumbele kwangu pindi tutakapofanikiwa kuingia madarakani,”alisema.
Samia aliahidi kuwa baada ya CCM kushinda katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, atahakikisha suala la afya ya mama na mtoto analipatia kipaumbele.
UMMY AMNADI
Akizungumza kabla ya Samia kuhutubia, Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM Taifa, Ummy Mwalimu, alisema mgombea mwenza aliamua kwenda kutembelea wagonjwa hususan wazazi kutokana na kutambua matatizo ya wanawake.
“Ni mwanamke mwenzetu kama sisi na alikwenda ‘leba’ (kujifungua), hivyo anayajua vyema matatizo ya kinamama. Kutokana na hali hiyo nawaomba wanawake wenzangu tusimwangushe. Tuichague CCM kwa kumpa kura Dk. John Magufuli (mgombea urais) na Samia ambaye ni mgombea mwenza wake.
“Hii inaonyesha kuwa kama atafanikiwa kuwa Makamu wa Rais, atachukulia kwa uzito mkubwa matatizo ya wanawake, hivyo tusifanye mchezo kuichagua CCM kwa sababu tutakuwa na mwanamke wa kwanza kuwa Makamu wa Rais,”alisema.
Naye Angella Kairuki, ambaye ni Kamanda wa Vijana wa CCM Wilaya ya Same, alisema Watanzania hawana budi kuichagua CCM ili ilete maendeleo makubwa, yakiwemo ya ujenzi wa viwanda ambavyo vitapunguza tatizo la ajira kwa wananchi wengi, wakiwemo vijana.
No comments:
Post a Comment